Thursday, October 5, 2017

TRUMP AKATAA KUZUNGUMZIA 'UMILIKI WA BUNGUKI' LICHA YA MAUAJI YA LAS VEGAS


Trump akataa kuzungumzia 'umiliki wa bunduki' licha ya mauaji ya Las Vegas
Licha ya makumi ya watu kuuawa na mamia ya wengine kujeruhiwa katika hujuma ya ufyatuaji risasi siku chache zilizopita nchini Marekani, lakini Rais Donald Trump wa nchi hiyo amekataa katakata kuzungumzia uwezekano wa kuangaliwa upya sheria ya raia kumiliki silaha nchini humo.
Alipowatembelea wahanga wa shambulizi la Las Vegas jana Jumatano, Trump alimwambia mwandishi wa habari kuwa: "Taifa lipo katika majonzi linaomboleza. Suala hilo (umiliki wa silaha) hatuwezi kulizungumzia kwa sasa.
Hii ni licha ya wabunge wa nchi hiyo akiwemo Jacky Rosen wa Nevada wa chama cha Democrat kusisitiza kuwa huu ndio wakati mwafaka wa kulizungumzia suala hilo hususan baada ya ukatili wa Las Vegas. 
Watu wasiopungua 59 waliuawa na wengine zaidi ya 500 kujeruhiwa baada ya mtu wa miaka 64 kwa jina la Stephen Paddock, kuwaminia risasi akiwa katika gorofa ya 32, usiku wa kuamkia Jumatatu  karibu na eneo la Mandalay Bay katika mji wa anasa wa Las Vegas nchini Marekani.

Baadhi ya watetezi wa uhuru wa kumiliki silaha US wanaamini kuwa ni haki ya dhati ya mtu na sehemu ya msingi ya historia na utamaduni wa nchi hiyo
Kwa mujibu wa Kituo cha Takwimu za Mashambulio ya Bunduki Marekani, kati ya Januari mwaka jana 2016 hadi Disemba 29 mwaka huo,  jumla ya matukio 57,371 ya ufyatuaji risasi yaliripotiwa katika maeneo mbalimbali ya Marekani ambayo yalisababisha watu 14,859 kuuawa na wengine 30,315 kujeruhiwa.
Hivi karibuni, gazeti la Washington Times liliandika kupitia ripoti maalumu kuwa, kwa wastani watu 88 hupoteza maisha kila siku nchini Marekani katika matukio ya utumiaji silaha moto yakiwemo ya watu wanaojiua

No comments:

Post a Comment