Kenya imeitaka jamii ya kimataifa iongeze
zaidi usaidizi wake kwa Kikosi cha Umoja wa Afrika cha Kulinda amani
Somalia, AMISOM ili kiweze kushughulikia kwa kina vitisho vya usalama
kabla ya kuanza kutekelezwa mpango wa kupunguza idadi ya askari wake.
Ombi
hilo limo katika hotuba ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Kenya Balozi Amina
Mohammed wakati akihutubia kikao cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa
jijini New York, Marekani siku ya Ijumaa.
Amesema
ili kuimarisha mafanikio yaliyokwishapatikana, Kenya inaunga mkono
azimio la Baraza la Usalama kuhusu msingi ya AMISOM. Aidha amesema zaidi
ya yote kuna haja ya kuwepo msaada wa kuwezesha ujenzi mpya wa Somalia,
kukiwemo kuwezesha serikali kutoa huduma za msingi.
Kwingineko katika hotuba yake, Balozi Amina
amezungumzia pia mabadiliko ya tabianchi akisema kuwa pamoja na
kusababisha mizozo ya rasilimali za maji na ardhi, yanagharimu asilimia 3
ya pato la ndani la taifa kila mwaka.
Hali
kadhalika Waziri huyo wa Mambo ya Nje wa Kenya amezungumza kuhusu suala
la wakimbizi kwa kutambua kuwa Kenya tangu miaka ya 60 imehifadhi
wakimbizi kutoka nchi jirani ikiwemo Somalia, hatua ambayo imekuwa na
changamoto nyingi zikiwemo za kiusalama.
Amesema ni kwa mantiki hiyo ndipo mwaka 2013 Kenya ilitia saini
makubaliano ya pande tatu baina yake, shirika la Umoja wa Mataifa la
kuhudumia wakimbizi, UNHCR na serikali ya Somalia kwa lengo la kuwezesha
wakimbizi kurejea nyumbani kwa hiari.
No comments:
Post a Comment