Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Kenya, Wafula Chebukati,
amewataka maafisa wa Tume hiyo waliotajwa kuvuruga uchaguzi mkuu
uliobatilishwa kuachia nafasi zao. Amewatuhumu pia wanasiasa kwa
kuizingira Tume hiyo.
Siku nane kabla ya kufanyika uchaguzi mpya wa urais hali ya wasiwasi
imetanda juu ya iwapo uchaguzi huo utafanyika kwenye mazingira bora na
ya kuaminika kama ilivyoamualiwa na mahakama ya Juu. Mwenyekiti wa Tume
hiyo Wafula Chebukati ameelezea wasiwasi wake kuhusu mshikamano wa
maafisa kwenye Tume hiyo suala ambalo limeigawa tume hiyo na kuliweka
taifa katika njiapanda. Chebukati ameeleza kuwa mapendekezo yake yote ya
kuhakikisha kuwa uchaguzi unaendeshwa kwa njia huru na ya haki yamekuwa
yakipigwa teke na makamishna wenzake.
Upande wa upinzani umekuwa
ukishinikiza kuondolewa kwa Afisa mkuu mtendaji wa Tume hiyo Ezra
Chiloba na maafisa wengine sita waondoke afisini, hatua ambayo
haijatekelezwa. "Katika hali kama hiyo ni vigumu kutoa hakikisho kwa
uchaguzi huru, wa haki na wa kuaminika, Bila ya mageuzi muhimu katika
sektariati ya tume uchaguzi huru na wa haki utavurugwa hivyo nawaomba
maafisa waliotajwa kavuruga uchaguzi uliopita kungatuka na kuruhusu
kikundi nilichobuni kufanya kazi," amesema Chebukati.
Kwenye
mkutano na wanahabari Chebukati amesema kuna nafasi ya kunusuru utendaji
kazi wa tume hiyo iwapo makamisha wote wataweka tofauti zao kando na
kuweka maslahi ya taifa mbele. Huku wengi wakitarajia kuwa angejiuzulu,
Chebukati alishikilia kuwa hatajiuzulu. Hata hivyo alikuwa mwepesi wa
kusema kuwa hatakuwa sehemu ya kikundi kitakachovuruga uchaguzi ujao kwa
manaufaa ya muda mfupi. Amewaonya wanasiasa ambao wanawatisha maafisa
wake. "Nawapa wanasiasa wote kadi ya njano, sitaruhusu vitisho kwa
maafisa wangu, sitaruhusu kuingiliwa kwa tume yangu tena. Wakenya
wanalipa pesa kubwa kugharamia uchaguzi huu. Na kama mwenye wajibu
sintoacha pesa za wakenya na washirika wetu zipotee," ameahidi
mwenyekiti huyo.
Kenyatta ataka watu waiombee nchi
Kiongozi wa upinzani Raila Odinga amesusia uchaguzi
Akigusia
suala la kamishna Roslyn Akombe aliyejiuzulu mapema leo, Chebukati
amemtaja Akombe kuwa mmoja wa watumishi wakakamavu waliojitolea kuhudumu
kwenye Tume hiyo. Amelaumu tume kwa kushindwa kutoa mazingira
yanayostahili kwa kamishna huyo, sababu iliyomfanya ajiuzulu. Wakati huo
huo rais Uhuru Kenyatta na naibu wake William Ruto wameendelea na
kampeni zao, huku wakiwataka wafuasi wao kujitokeza kwa wingi kurejesha
chama cha Jubilee mamlakani kwa kipindi kingine cha miaka mitano. Wawili
hao wamesema kuwa hawataruhusu kiongozi wa upinzani Raila Odinga
kusitisha mchakato wa uchaguzi mpya wa urais. "Wewe Bwana Odinga
kwasababu tumekubali haki ya kukaa nyumbani, kwanini unafikiria kuwa
wewe uko na haki ya kukataza wakenya wale ambao wanataka kupiga kura
wapige kura, hiyo hatuwezi kukubali," amesema Kenyatta.
Naye
Makamu wa Rais William Ruto akaongezea, "Sasa huyu mtu wa vitendawili
anasema kuwa atasimamisha uchaguzi, kama Uhuru Kenyatta ambaye ni amiri
jeshi mkuu wa majeshi yote ya Kenya, hawezi kusimamisha uchaguzi, sasa
mtu wa vitendawili na uganga ataweza, aache mzchezo."
Ili
kujikwamua katika mzozo wa sasa, taifa litahitaji vitendo na nia nzuri
zaidi ya matamshi kutoka kwa wanasiasa ambao wanavutia upande wao kwani
kwa sasa taifa limegawanyika. Mapema Rais Kenyatta aliwataka wakenya wa
dini zote kutenga siku ya Jumapili kuombea taifa huku wachambuzi wa
masuala ya siasa wakimtaka kuketi meza moja na Odinga kwa mazungumzo.
No comments:
Post a Comment