Wanajeshi wa Marekani walipotiwa nguvuni na Jeshi la Sepah baada ya kuingia katika maji ya Iran kinyume cha sheria
Kamati na Uhusiano wa Kimataifa ya Baraza la
Congress la Marekani imepasisha azimio dhidi ya miradi ya makombora ya
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ikiwa ni kuonesha chuki zake za wazi dhidi
ya Tehran.
Azimio hilo ambalo limewasilishwa
mbele ya baraza hilo na Ed Royce, mkuu wa kamati ya uhusiano wa
kimataifa ya Congress ya Marekani limeliwekea vikwazo Jeshi la Walinzi
wa Mapinduzi ya Kiislamu SEPAH kwa madai ya eti kuendesha miradi isiyo
halali ya kuimarisha makombora ya balestiki. Azimio hilo lililopewa jina
la "Sheria ya Makombora ya Balestiki ya Serikali ya Iran na Uwekaji
Vikwazo Kimataifa" limeifungulia njia serikali ya Marekani kuiwekea
vikwazo vipya Iran.
Hatua hiyo ya kamati ya uhusiano wa
kimataifa ya Congress ya Marekani imechukuliwa siku moja kabla ya
serikali ya rais wa Marekani, Donald Trump kutangaza msimamo wake
kuhusiana na namna ya kukabiliana na Iran pamoja na makubaliano ya
nyuklia yanayojulikana kwa jina maarufu la JCPOA. Baadhi ya wajumbe wa
Baraza la Congress la Marekani wanajaribu kuwa na msimamo mkali sawa na
wa Donald Trump dhidi ya Iran na wanafanya njama za kila namna
za kuhakikisha misimamo iliyo dhidi ya Iran inapata nguvu nchini
Marekani. Sasa baada ya kuona kuwa dunia nzima imekiri kwamba Iran haina
nia kabisa ya kumiliki silaha za nyuklia na imetekeleza kikamilifu
makubaliano ya JCPOA, maadui wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran nchini
Marekani wameamua kuulenga kikamilifu muundo wa ulinzi wa Iran. Katika
starijia za kiulinzi za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, miradi ya makombora
na kuimarisha miradi hiyo kunafanyika kwa lengo la kiulinzi tu kwa
ajili ya kuiweka salama Iran katika eneo hili lenye migogoro mingi la
magharibi mwa Asia.
Amma nukta ya kuzingatia hapa ni kwamba,
katika makubaliano ya nyuklia baina ya Iran na kundi la 5+1 (JCPOA),
hakuna hata mahala pamoja palipogusiwa miradi ya makombora ya Iran. Hata
azimio nambari 2231 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ambalo
limeunga mkono na kutia nguvu makubaliano ya JCPOA limeiomba tu Iran
isitengeneze makombora yanayokusudia kubeba vichwa vya nyuklia. Jamhuri
ya Kiislamu ya Iran inasisitiza kuwa utekelezaji wa azimio hilo la Umoja
wa Mataifa ni wajibu wa kisheria. Ndio maana katika uimarishaji wa
makombora yake, Iran inazingatia ustadi wa kulenga shabaha makombora
yake na si kubeba vichwa vya nyuklia. Kwa maneno mengine ni kuwa, lengo
la Iran si kuyafanya makombora yake yabebe vichwa vya nyuklia hivyo
Tehran haijishughulishi na upande huo, bali inazingatia uwezo mkubwa wa
makombora hayo ya kulenga shabaha kwa ustadi wa hali ya juu.
Katika upande mwingine, Iran iko katika
eneo ambalo baaadhi ya nchi zinatumia mamia ya mabilioni ya dola
kujilimbikizia silaha na zinaweka mikataba mikubwa mikubwa ya silaha na
Marekani na nchi za Ulaya, hivyo ni jambo la kawaida kabisa kwa Iran
nayo kuwekeza katika uwezo wake wa makombora. Si hayo tu, lakini kwa
makumi ya miaka sasa Iran imewekewa vikwazo vya silaha huku nchi za
Magharibi zikizishehenesha baadhi ya nchi za eneo hili marundo ya silaha
za kila namna. Sasa ni kichekesho kikubwa kuona nchi kama Marekani
inaisakama Iran kwa kujiimarisha kiulinzi wakati yenyewe Marekani kila
leo inawekeana na baadhi ya nchi za eneo hili la magharibi mwa Asia,
mikataba ya silaha ya mabilioni ya dola. Bila ya shaka yoyote ni haki ya
Iran ya kujiimarisha kiulinzi na kuhakikisha kwamba adui hafikirii
kabisa kuivamia kijeshi.
Hii ni kusisitiza kuwa hatua ya Jeshi la
Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu SEPAH ya kushambulia ngome za magaidi
wa Daesh nchini Syria kwa kutumia makombora yake ya masafa ya kati tena
kutokea nchini Iran imewathibitishia walimwengu kuwa, Jamhuri ya
Kiislamu ya Iran haina mchezo katika suala zima la kulinda usalama wake.
Tumalizie kwa kusema kuwa, vikwazo vya aina yoyote ile dhidi ya miradi
ya makombora ya Iran ni kinyume cha sheria, si mantiki, lakini muhimu
zaidi kuliko yote ni kwamba haviwezi kamwe kuizuia Iran kujiimarisha
kiulinzi na kujidhaminia usalama wake.
No comments:
Post a Comment