Malefu ya watu wameandamana Jumamosi katika miji
mbalimbali ya Uhispania wakishinikiza kufanyika majadiliano kumaliza
mgogoro wa jimbo la kaskazini-mashariki la Catalonia, linalotaka
kujitenga.
Wakiwa wamebeba mabango yenye ujumbe usemao "Hablamos?" na "Parlem?" -
maneno ya Kikatalan na Kihispania yanayomaanisha "Tunaweza kuzungumza?"
- waandamanaji hao walikusanyika majira ya saa sita mchana nje ya kumbi
za miji ya Madrid na Barcelona, na pia katika miji ya Zaragoza, Seville
na Bilbao.
"Ahsanteni kwa kuujaza uwanja wa Cibeles mjini Madrid
na kumbi kadhaa za miji kote Uhispania. Sasa tuwaache wanasiasa wafanye
kazi yao, hicho ndicho tunachowalipia mishahara," waliandika waandaji
wa maandamano hayo kwenye ukurasa wao wa Facebook.
Hashtag ya
#parlemhablemos ndiyo mada iliyohanikiza kwenye mtandao wa Tweeter.
Kabla ya maandamano ya Jumamosi, ambako watu waliombwa kuvaa nguo nyeupe
kuepusha kaulimbiu au nyimbo za vyama, waandaaji walisambaza ilani
iliosoma: "Tunajua inawezekana kuishi pamoja. Uhispania ni bora kuliko
watawala wake na imeonyesha hili mara nyingi."
"Tulikuwa na
wasiwasi kuhusu mwelekeo wa kisiasa katika siku hizi zilizopita.
Zilikuwa zinaelekea kwenye mkwamo," mmoja wa waandaji wa maandamano hayo
Pablo Fernandez aliliambia shirika la habari la Ujerumani dpa.
Watu wakishiriki maandamano kuunga mkono majadiliano katika uwanja mjini Barcelona, Uhispania Oktoba 7, 2017.
Mjini
Madrid, kulikufanyika pia mkutano wa kupinga kujitenga katika eneo la
Plaza de Colon, ulioandaliwa na wakfu wa kizalendo wa ulinzi wa taifa la
Uhispania wa DENAES. Mkutano huo ulihudhiriwa na watu karibu 50,000,"
kwa mujibu wa duru rasmi. Watu walikuwa wakiimba nyimbo za "Idumu
Uhispania," "Adumu Mfalme" na "Catalonia pia ni Uhispania."
Maandamano kuendelea Jumapili
Maandamano
mengine makubwa ya kupinga uhuru wa Catalonia yamepangwa kufanyika siku
ya Jumapili mjini Barcelona yakiitwa "Inatosha! Turudi kutumia akili."
Maandamano hayo yaamepangwa kufungwa kwa hotuba ya mwandishi habari
alieshinda tuzo ya amani ya Nobel na mwandishi vitabu Mario Vargas
Llosa.
Oktoba 1, Catalonia iliitisha kura ya maoni kuamua juu ya
uhuru wake ambapo asilimia 90 ya walioshiriki waliunga mkono kujitenga
na Uhispania, ingawa uitikiaji wa kura hiyo ulikuwa ni asilimia 43 ya
watu wanaostahili kupiga kura.
Tangu wakati huo, Uhispania
imetumbukia katika mgogoro mkubwa zaidi wa kisiasa kuwahi kuikumba
katika kipindi cha miongo kadhaa, huku serikali ya jimbo la Catalonia
ikionekana kutangaza uamuzi wa upande mmoja wa uhuru licha ya hatua hiyo
kupigwa marufuku na Mahakama ya Katiba ya Uhispania na serikali kuu
mjini Madrid.
Mjini
Madrid, waandamanaji wakipeperusha bendera za Uhispania wakati wa
maandamano yalioitishwa na Wakfu wa DENAES wa ulinzi wa taifa la
Uhispania, katika uwanja wa Colon, 07.10.2017.
Merkel, Juncker wazungumzia mgogoro huo
Kansela
wa Ujerumani Angela Merkel na rais wa Halmashauri kuu ya Umoja wa Ulaya
Jean-Claude Juncker waliujadili mzozo huo katika mazungumzo kwa njia ya
simu siku ya Ijumaa.
Mashaka yatokananyo na mzozo huo
yameyalaazimu makampuni kadhaa ya kibiashara na mabenki kuhamisha
shughuli zake nje ya Catalonia na kuzipeleka katika maeneo mengine ya
Uhispania katika siku za karibuni.
Kikao cha bunge la jimbo la
Catalonia kilichokuwa kimepangwa kufanyika siku ya Jumatatu, na ambacho
kilitarajiwa kuhusisha tangazo la upande mmoja la uhusu, kimefutwa baada
ya kupigwa marufu na mahakama ya juu ya nchi hiyo.
Serikali ya
Uhispania na polisi yake wamekosolewa vikali kutokana na ukandamizaji wa
vurugu wa polisi siku ya kura, ambayo ilikuwa tayari imetangazwa kuwa
haramu na mahakama ya katiba, na ilikuwa imepingwa vikali na serikali
kuu mjini Madrid.
No comments:
Post a Comment