Friday, October 13, 2017

URUSI YAIONYA MAREKANI DHIDI YA KUBATILISHA MAKUBALIANO YA MRADI WA KINUKLEA WA IRANI

Urusi imeionya Marekani dhidi ya kujitoa katika makubaliano ya kimataifa ya mradi wa nuklea wa Iran. Katika wakati ambapo walimwengu wanasubiri kusikia kitakachosemwa na rais Donald Trump baadae hii leo , viongozi wa Urusi wanatahadharisha na kusema madhara yatakuwa makubwa kupita kiasi pindi rais Trump akijitoa katika makubaliano hayo. Msemaji wa ikulu ya Urusi ameutaja uwezekano wa Iran kujitoa pia katika makubaliano hayo, hali ambayo anasema itaathiri usalama na utulivu kote ulimwenguni. Naye waziri wa mambo ya nchi za nje Sergei Lavrow amemhakikishia waziri mwenzake wa Iran, Urusi itaendelea kuheshimu makubaliano yaliyofikiwa. Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Ujerumani Sigmar Gabriel pia ameonya dhidi ya hatari ya uamuzi wa upande mmoja wa kubatilisha makubaliano kuhusu mradi wa nyuklea wa Iran. Rais wa Marekani Donald Trump anatarajiwa kuzungumzia kuhusu mkakati wake kuelekea Iran baadae leo usiku. Akipinga kwa mara nyengine tena kuuidhinisha, bunge la Marekani Congress litabidi lizingatie uwezekano wa kutangaza upya vikwazo dhidi ya Iran.

No comments:

Post a Comment