Kwa mara nyingine tena, Marekani imekataa
kutia saini makubaliano ya kupiga marufuku silaha za nyuklia ikisisitiza
kuwa Washington haina mpango kabisa wa kujiunga na makubaliano hayo
yanayoungwa mkono wa washindi wa tunzo ya Nobel.
Muda mchache tu baada ya
kutangazwa washindi wa tunzo ya amani ya Nobel mwaka 2017, msemaji wa
Ikulu ya Marekani (White House) alisema, hakuna mabadiliko yoyote katika
msimamo wa Marekani wa kukataa kujiunga na makubaliano ya kupiga
marufuku silaha za nyuklia. Alisema, Marekani inaamini kuwa makubaliano
hayo hayawezi kuleta amani duniani na si tu hayawezi kupelekea
kuangamizwa silaha za atomiki, lakini pia hayana uwezo wa kutia nguvu
usalama wa nchi za dunia.
Itakumbukwa kuwa, tunzo ya amani ya
Nobel mwaka 2017 iliyotolewa siku ya Ijumaa, imekwenda kwa Kampeni ya
Kimataifa ya Kuangamiza Silaha za Nyuklia (ICAN). Kampuni hiyo imetoa
mchango mkubwa katika kutiwa saini makubaliano hayo na nchi 122 mwezi
Julai mwaka huu. Hata hivyo makubaliano hayo ni ya kimaonyesho zaidi
kulikoni kuwa ya uhakika. Sababu yake ni kwamba nchi nane zenye silaha
za nyuklia yaani Marekani, Russia, Uingereza, Ufaransa, China, India,
Pakistan na Korea Kaskazini pamoja na utawala wa Kizayuni wa Israel,
zimekataa kutia saini makubaliano hayo.
Taarifa zinasema kuwa Marekani inamiliki
vichwa elfu nne vya nyuklia hivi sasa. Wamarekani wanadai kuwa, lengo
lao la kujilimbikizia silaha za nyuklia za mauaji ya umati, ni kujilinda
mbele ya nchi nyingine zenye silaha hizo za maangamizi ya halaiki. Hata
hivyo madai hayo hayana ukweli kwani Marekani ndiyo nchi pekee duniani
ambayo imewahi kutumia silaha za nyuklia katika historia nzima ya
mwanadamu. Katika Vita vya Pili vya Dunia, Marekani ilishambulia kwa
nyuklia miji ya Hiroshima na Nagasaki nchni Japan kwa madai ya
kuwalazimisha viongozi wa nchi hiyo wasalimu amri. Ukatili huo wa
Marekani umewafanya kuwa wahanga maelfu kwa maelfu ya viumbe wakiwemo
wanadamu. Ripoti zinaonesha kuwa hivi sasa Marekani inamiliki bomu
lijulikanalo kwa jina la B61 na sasa hivi inalifanyia marekebisho bomu
hilo kwa gharama zilizosawa na dola bilioni kumi. Bi Dianne Feinstein,
seneta wa Marekani kutoka chama cha Democrats anaamini kuwa, silaha za
kiistratijia zilizoko katika maghala ya silaha nchini Marekani ni nyingi
mno ikilinganishwa na mahitaji ya nchi hiyo na waitifaki wake.
Wachambuzi wa mambo wanasema kuwa,
Marekani haiwezi kabisa kujiunga na mikataba na makubaliano ya
kuangamiza silaha za nyuklia duniani, bali kitu pekee kinachotegemewa
kutoka kwa dola hilo la kibeberu ni kushadidisha majaribio yake ya
nyuklia, jambo ambalo linazichochea nchi nyingine duniani kujilimbikizia
silaha za kisasa zaidi za nyuklia na za maangamizi ya umati. Fauka ya
hayo, rais wa Marekani, Donald Trump alisema waziwazi wakati wa kampeni
za uchaguzi kwamba hatosita kufanya mashambulizi ya nyuklia akilazimika
kufanya hivyo.
Hivi sasa jeshi la Marekani imejikita
zaidi katika kutengeneza mabomu madogo madogo yenye athari hafifu kidogo
ya nyuklia na kuyafanyia majaribio katika nchi mbalimbali za dunia kama
za Mashariki ya Kati. Pamoja na kukhafifishwa huko, lakini mabomu hayo
bado yanafanya uharibifu mkubwa. Sasa hivi si tu juhudi za kuangamiza
silaha za nyuklia hazijafanikiwa, lakini baya zaidi ni kwamba madola ya
kibeberu kama vile Marekani yanazidi kujilimbikizia silaha hizo angamizi
na kuzifanya kuwa za hatari zaidi. Nukta ya kuzingatiwa hapa ni kwamba
iwapo silaha hizo zitaingia mikononi mwa watu wasioaminika au magenge ya
kigaidi, hakuna mtu yeyote anayeweza kutabiri ukubwa wa hatari na
madhara yanayoweza kusababishwa na jambo hilo duniani.
No comments:
Post a Comment