Mfalme wa Qatar Sheikh Tamim bin Hamad Al
Thani amesema Iran ndio njia pekee ya kupitishia chakula kwa ajili ya
wananchi wa Qatar waliowekewa mzingiro; na akaongeza kwamba Saudi Arabia
na nchi nyengine tatu za Kiarabu zinakula njama ya kuubadilisha utawala
katika nchi yake.
Amir wa Qatar ameyasema hayo katika mahojiano na kanali ya
televisheni ya CBS ya Marekani. Akijibu suali kuhusu dai kwamba Saudia
na nchi nyengine tatu za Kiarabu zinaituhumu Doha kuwa ina urafiki wa
kupita kiasi na Tehran, Sheikh Tamim Al Thani amesema: Iran ni jirani wa
Qatar na serikali ya Doha ina uhusiano mpana wa kisiasa na Iran kuliko
ilivyo na Saudia na waitifaki wake.
Mfalme wa Qatar amekumbusha matukio yaliyojiri miaka 21 nyuma na
njama zilizofanywa kwa madhumuni ya kumpindua baba yake Shiekh Hamad bin
Khalifa Al Thani na kuongeza kuwa: historia imeonyesha kuwa hapo kabla
pia Saudi Arabia imefanya kila njia ili kuubadilisha utawala nchini
Qatar.
Kuhusiana na kuwepo ofisi za kundi la kigaidi la Taliban mjini Doha,
Mfalme wa Qatar ameeleza kuwa: Marekani ilitutaka tuwapokee Taliban na
kuliruhusu kundi hilo lifungue ofisi yake mjini Doha ili Marekani iweze
kufanya mazungumzo nalo.
Mbali na kutangaza utayari wa kufanya mazungumzo ya ana kwa ana na
nchi nne zilizoiwekea vikwazo nchi yake ili kutatua mgogoro uliopo baina
ya Doha na nchi hizo, Sheikh Tamim Al Thani amesema: Qatar inataka
kumalizwa hitilafu zilizopo, lakini hakuna kitu chenye hadhi ya juu
zaidi kuliko heshima na mamlaka ya kujitawala nchi hiyo.
Tangu tarehe 5 Juni mwaka huu, Saudi Arabia, Imarati (UAE), Bahrain
na Misri zimevunja uhusiano wao wa kidiplomasia na Qatar kwa sababu ya
misimamo ya Doha ambayo haiwiyani na sera za utawala wa Riyadh. Mbali na
kuiwekea vikwazo, nchi hizo nne zimeifungia Qatar pia mipaka yao ya
nchi kavu, baharini na angani.../
No comments:
Post a Comment