Saturday, October 28, 2017

ISMAIL HANIYA: JARIBIO LA ISRAEL LA KUMUUA AFISA MKUU WA HAMAS LIMEFELI

Ismail Haniya: jaribio la Israel la kumuua afisa mkuu wa HAMAS limefeli
Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina HAMAS amesema utawala wa Kizayuni wa Israel ndio umehusika katika jaribio la mauaji lililofeli dhidi ya afisa wa ngazi ya juu wa harakati hiyo.
Ismail Haniya aliyasema hayo jana Ijumaa, alipomtembelea Tawfiq Abu Na'im, Mkurugenzi Mkuu wa Vikosi vya Usalama wa Ndani vya HAMAS, aliyelazwa katika Hospitali ya Dar al-Shifa katika Ukanda wa Gaza, baada ya jaribio la mauaji dhidi yake.
Kiongozi huyo wa HAMAS amesema: "Vyombo vya Palestina vitawaadhibu waliohusika na jaribio hilo la mauaji, tunaamini kuwa utawala wa ghasibu wa Israel na washirika wake ndio waliohusika katika jaribio hilo la ukatili lililogonga mwamba."
Taarifa ya Waizara ya Mambo ya Ndani ya HAMAS imesema Abu Na'im alipata majeraha baada ya gari lake kushambuliwa kwa bomu katika kambi ya wakimbizi ya Nuseirat mapema hiyo jana.
Ismail Haniya, kiongozi wa HAMAS
Ismail Haniya amesema kamwe utawala wa Kizayuni wa Israel hauwezi kuvunja umoja na mshikamano wa Wapalestina na ni kosa kudhani kuwa njama kama hizi zinaweza kuwafanya Wapalestina waachane na jitihada zao za kukomboa ardhi zao zinazokaliwa kwa mabavu. 
Mapema mwezi huu, kiongozi huyo wa HAMAS sambamba na kuashiria hatua zilizochukuliwa hivi karibuni na harakati hiyo ya muqawama za kuondoa hitilafu kati yake na harakati ya Fat'h na juhudi ilizofanya kwa ajili ya kufikiwa maridhiano ya kitaifa baina ya Wapalestina, alibainisha kuwa: zama za hitilafu za ndani zimepita; na harakati ya HAMAS imeshaamua kulipa gharama zozote zinazoilazimu kwa ajili ya kufanikisha maridhiano rasmi ya kitaifa.

No comments:

Post a Comment