Sunday, October 8, 2017

UAE INANUNUA KWA SIRI SILAHA ZA UTAWALA WA KIZAYUNI WA ISRAEL

UAE inanunua kwa siri silaha za utawala wa Kizayuni wa Israel
Umoja wa Falme za Kiarabu, UAE au Imarati, inanunua kwa siri silaha za utawala wa Kizayuni wa Israel.
Gazeti la Kizayuni la Maariv limeandika katika toleo lake la Jumamosi kuwa, kwa muda mrefu utawala wa Israel umekuwa ukiiuzia kwa siri Imarati silaha mbali na kushirikiana kiuslama na kijeshi na nchi hiyo ya Kiarabu.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, Metai Kokhafi, moja kati ya  wafanyabiashara mashuhuri wa Israel amekuwa akiongoza mkakati huo wa kuiuzia Imarati silaha. Kokhafi aliwahi kukodi ndege na kuwabeba majenarali Waisraeli hadi Abu Dhabi kutia saini mikataba ya silaha na UAE.
Gazeti hilo limeongeza kuwa, Israel pia ina uhusiano mzuri wa kijeshi na kiusalama na Misri na imepangwa kuwa pande mbili zifanye mazoezi ya pamoja ya kijeshi pamoja na Ugiriki na Cyprus katika siku za usoni.
Katika miezi ya hivi karibuni baadhi ya watawala wa nchi za Kiarabu wamekuwa wakizungumza kuhusu kuwepo na uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni wa Israel.  Hivi karibuni mfalme wa Bahrain alisema wakati umefika wa kuanzishwa uhusiano kamili wa kidiplomasia baina ya nchi za Kiarabu na Israel.
Saudi Arabia na UAE zimekuwa zikiongoza jitihada za wazi na za nyuma ya pazia za kuanzisha uhusiano na utawala wa Israel.
Nchi Hizo za Kiarabu zinapuuza ukweli kuwa, utawala haramu wa Israel unakalia kwa mabavu ardhi za Palestina hasa Msikiti wa Al Aqsa ambao ni kibla cha kwanza cha Waislamu mbali na kuendeleza jinai zisizo na kikomo dhidi ya Wapalestina wanaopigania ukombozi wa ardhi zao.

No comments:

Post a Comment