Kwa mara nyingine suala la namna ya
Washington inavyotakiwa kukabiliana na Korea Kaskazini, limeibua tofauti
kati ya Rais Donald Trump na Waziri wake wa Mambo ya Nje Rex W.
Tillerson.
Muda mfupi baada ya Tillerson
kuzungumza mjini Beijing, China kuhusiana na uwepo wa mtandao wa
mawasiliano ya moja kwa moja na serikali ya Korea Kaskazini, Rais Donald
Trump amesema kuwa, kufanya mazungumzo na Pyongyang ni kupoteza wakati.
Katika ukurasa wake wa Twitter, Trump alimueleza Waziri wake wa Mambo
ya Nje kwa kuandika kuwa: "Nimeshamwambia Rex Tillerson, Waziri wetu
mzuri sana wa Mambo ya Nje kwamba anapoteza muda wake kwa kujaribu
kuzungumza na Mtu Mdogo wa Makombora". Mwisho wa kunukuu.
Katika wiki za hivi karibuni na katika
miamala isiyo ya kimantiki wala kidiplomasia, Trump alimtaja Kim
Jong-Un, Kiongozi wa Korea Kaskazini kuwa 'Mtu wa Makombora.' Matamshi
hayo aliyatoa katika hali ambayo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani
alikuwa amefanya safari nchini China ambapo kwa mara ya kwanza alikiri
kuwepo mawasiliano kati ya serikali ya Marekani na Pyongyang. Akiongea
na waandishi wa habari, Tillerson alisema kuwa Washington inatumia
mawasiliano hayo kwa ajili ya kufahamu misimamo ya Korea Kaskazini kwa
minajili ya kutatua mgogoro wa sasa wa eneo la Peninsula ya Korea.
Kuongezeka mzozo wa eneo la Korea, kumeenda sambamba na kuibuka tofauti
za ndani katika serikali ya Washington kuhusiana na kadhia hiyo.
Hata hivyo ifahamike kuwa, tofauti kati
ya marais wa Marekani na mawaziri wao, ni jambo la kawaida. Pamoja na
hayo hakujawahi kushuhudiwa tofauti kubwa kama za sasa kiasi cha
kumfanya Rais Donald Trump aamue kuandika katika ukurasa wake wa Twitter
akiieleza dunia kuhusiana na uwepo wa tofauti kati yake na waziri wake
huyo wa masuala ya kigeni. Matamshi na maoni rasmi ya Trump kupitia
mtandao wa Twitter yanaonyesha kwamba rais huyo wa Marekani ameazimia
kuanzisha vita haribifu vya silaha za nyuklia katika eneo la mashariki
mwa Asia na ni kwa ajili hiyo ndio ameepusha aina yoyote ya mazungumzo
yenye lengo la kuzuia kutokea vita hivyo. Hii ni katika hali ambayo duru
za kidiplomasia na hata za kijeshi nchini humo, kwa akali zimeweka wazi
misimamo yao rasmi katika kufuatilia njia za amani za utatuzi wa
mgogoro wa eneo la Peninsula ya Korea.
Kundi hilo linaamini kuwa, rais wa sasa
wa Marekani ambaye hana aina yoyote ya uzoefu wa kisiasa na kiusalama,
anakusudia kuitumbukiza nchi hiyo katika vita vya nyuklia na Korea
Kaskazini, vita ambavyo vitasambaa hadi Japan, Korea Kusini, China na
Russia. Ni kwa msingi huo ndio maana weledi hao wanafanya juhudi za
kufungua milango ya mazungumzo ya amani na Pyongyang. Hata hivyo ili
kujaribu kujionyesha kuwa naye ni mwanasiasa, Trump na katika kujaribu
kuvutia uungaji mkono wa Wamarekani na hata wa baadhi ya washirika wake
nje ya nchi, anaendelea kupiga ngoma ya vita dhidi ya Korea Kaskazini
sambamba na kusisitiza kuwa mazungumzo na Pyongyang ni jambo lisilokuwa
na faida yoyote. Ala kulli hal, misimamo hasi ya Rais Donald Trump dhidi
ya Korea Kaskazini ndiyo imeifanya nchi hiyo ya Asia kujiimarisha zaidi
kwa silaha za nyuklia na makombora ya balestiki suala ambalo kwa upande
mwingine linaendelea kumtia hasira rais huyo wa Marekani.
No comments:
Post a Comment