Polisi ya kenya imesema kuwa watu wanne
wameuawa katika maandamano ya upinzani nchini humo katika kipindi cha
wiki mbili zilizopita huku uchaguzi wa rais wa marudio ukikaribia
kufanyika wiki ijayo. Polisi ya Kenya imesema kuwa watu hao waliuawa
katika mapigano yaliyotokea kati ya maafisa polisi na waandamanaji.
Polisi imeeleza kuwa, watu hao waliaga dunia kati ya tarehe 2 mwezi huu na siku ya Jumatatu iliyopita.
Itakumbukwa kuwa, mapema
wiki hii Shirika la Msamaha Duniani (Amnesty International) liliituhumu
polisi ya Kenya kuwa imeuwa watu 67 katika maandamano ya upinzani
yaliyofanywa siku kadhaa baada ya kutangazwa matokeo ya uchaguzi mkuu wa
nchi hiyo uliofanyika Agosti nane.
Mahakama ya Juu ya Kenya ilitengua
ushindi wa Rais Uhuru Kenyatta ikisema kuwa uchaguzi wa rais uligubikwa
na kasoro na kuagiza uchaguzi wa marudio. Kiongozi wa muungano wa
upinzani (Nasa) Raila Odinga ambaye hoja yake ya kupinga matokeo ya
uchaguzi wa rais mahakamani ilipelekea kutenguliwa matokeo ya uchaguzi
huo, ametangaza kujitoa katika uchaguzi wa marudio akisema kuwa uchaguzi
huo una hatari ya kugubikwa na kasoro kama zile zilizojitokeza katika
uchaguzi uliopita.
No comments:
Post a Comment