Jumuiya za kimataifa za kutetea haki za
binadamu zimepongeza hatua ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio
Guterres ya kuiweka Saudi Arabia na washirika wake katika orodha nyeusi
ya nchi na jumuiya zinazokiuka haki za watoto katika maeneo yenye vita.
Mkurugenzi
wa kitengo cha watoto katika shirika la kutetea haki za binadamu la
Human Rights Watch, Jo Becker amesema kuwa, uamuzi wa kuiweka Saudi
Arabia katika orodha nyeusi ya UN unapaswa kufuatiwa na hatua za
kivitendo za kuhakikisha kwamba, Riyadh na washirika wake wanaheshimu
sheria za kuwalinda watoto. Becker amesisitiza kuwa, umewadia wakati wa
muungano unaoongozwa na Saudia kukomesha kikamilifu mashambulizi yake
dhidi ya watu wa Yemen.
Wakati
huo huo mwakilishi wa shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty
International katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York
amesema shirika hilo limefurahi kuona Antonio Guterres akifanya
yaliyomshinda katibu Mkuu wa kabla yake wa Umoja wa Mataifa baada ya
kuona kuwa, idadi kubwa ya watoto wameuawa katika mashambulizi ya Saudia
na washirika wake huko Yemen.
Sherine Tadros amesisitzia kuwa, kuna ulazima wa kuwekwa marufuku ya
kuiuzia silaha Saudi Arabia na washirika wake katika vita dhidi ya watu
wa Yemen.
Mamia
ya watoto wadogo wameuawa, shule, hospitali na miundombuni kuvunjwa
kabisa katika mashambulizi yanayofanywa na Saudi Arabia na washirika
wake dhidi ya Yemen yanayoendelea kwa zaidi ya miaka miwili sasa.
No comments:
Post a Comment