Thursday, October 5, 2017

KUONGEZEKA UKANDAMIZAJI NCHINI SAUDI ARABIA KATIKA KIVULI CHA MABADILIKO YA KIMAONYESHO YA AAL SAUD

Kuongezeka ukandamizaji nchini Saudi Arabia katika kivuli cha mabadiliko ya kimaonyesho ya Aal Saud
Utawala wa Aal Saud umewatia mbaroni watu kumi katika kuendelea siasa za kuwakandamiza wapinzani nchini humo.
Shirika rasmi la habari la Saudi Arabia  limeripoti habari ya kukamatwa wapinzani 26 nchini humo kwa kosa la kutuma jumbe na taarifa katika mitandao ya kijamii. Matukio mbalimbali yanaonyesha kuwa ukandamizaji nchini Saudia umeongezeka kwa lengo la kufifiza moyo na harakati za malalamiko nchini humo.
Katika mazingira hayo, utawala wa Aal Saud unatumia mbinu tofauti kukandamiza fikra za waliowengi na wakati huo huo kufanya kila uwezalo kufunika ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu na za kisiasa za wananchi wa nchi hiyo, unaofanywa na utawala huo. Matukio ya kimaonyesho yanayojiri nchini Saudia yanatekelezwa ili kudhihirisha sura mpya na tofauti kabisa na ile inayotambulika katika uga wa kimataifa kuhusiana na nchi hiyo. Wanawake wa Saudia kuruhusiwa kuendesha magari na wakati huohuo mufti wa dola kuwaruhusu wasafiri nje ya nchi bila ya ruhusa ya waume zao na mambo mengineyo, ni miongoni mwa uhuru wa kiraia uliotangazwa hivi karibuni na Saudi Arabia kwa maslahi ya wanawake na suala hilo kuzingatiwa na taasisi za kimataifa. 
Saudi Arabia imekuwa na rekodi mbaya sana ya ukiukaji wa haki za binadamu kimataifa. Aidha wachambuzi wa mambo wanaamini kuwa hatua ya watawala wa nchi hiyo kuondoa marufuku iliyokuwa inawazuia wanawake kuendesha magari imekusudiwa kuboresha sura yao katika ngazi za kimataifa baada ya kashfa ya mauaji ya kizazi wanayofanya huko Yemen na uungaji mkono wao kwa makundi hatari ya kigaidi duniani. 
Mauaji ya raia na kuharibiwa nyumba na miundo mbinu ya Yemen kutokana na uvamizi wa kijeshi wa Saudia
Hatua hizo za kimaonyesho za utawala wa Aal Saud  hazihusiani tu na masuala ya kijamii bali zinashuhudiwa pia katika sekta ya kiuchumi; ambapo zinatathminiwa kuwa eti ni katika ruwaza ya mwaka 2030 ya nchi hiyo iliyoainishwa hivi karibuni na Muhammad bin Salman, Mrithi wa Kiti cha Ufalme wa Saudi Arabia. Kwa kuzingatia misingi dhaifu ya kiuchumi ya Saudia chini ya utawala wa ukoo wa Aal Saud, weledi wa masuala ya kisiasa wanamini kuwa, nchi hiyo haina uwezo wa kujielekeza katika miradi na mipango yenye gharama kubwa. 
Muhammad bin Salman, Mrithi wa Kiti cha Ufalme wa Saudia  
Weledi hao wa mambo wanaamini pia kwamba utawala wa Aal Saud unawahadaa  raia wake kuwa unatekeleza mipango ya kukabiliana na matatizo ya kiuchumi, lengo likiwa ni kuwapotosha na kuwafanya wasizingatie matatizo makubwa ya kiuchumi yanayowakabili. 
Katika uga wa kisiasa pia utawala huo umefanya mabadliko ya kimaonyesho katika serikali ya nchi hiyo lengo kuu likiwa ni kuidhihirisha nchi hiyo kuwa inatekeleza marekebisho ya kisiasa. Hatua zinazochukulliwa sasa na utawala wa Aal Saudi zinaonyesha kuwa lengo halisi la utawala huo wa kiimla ni kuzuia mabadiliko ya kimsingi ambayo ni matakwa ya raia wa nchi hiyo. Mabadiliko hayo yanayodaiwa na wananchi wa Saudia yamekuwa chanzo cha kuibuka wimbi la malalamiko ya Wasaudia dhidi ya utawala wa kifalme wa nchi hiyo tangu mwaka 2011. Pamoja na kutekelezwa baadhi ya marekebisho ya kijamii kuhusiana na wanawake huko Saudia, lakini hakuna maratajio wala kushuhudiwa kuwekwa wazi mipango ya baadaye ya kufuta vizuizi na mbinyo katika uhuru wa kujieleza, kuasisiwa mirengo ya kisiasa na kupunguzwa ukandamizaji na mbinyo mkubwa unaoikabili jamii ya  waliowachache khususan Washia wa nchi hiyo. Kwa kuzingatia hayo ni wazi kuwa mabadiliko ya kimaonyesho ya hivi sasa huko Saudia hayakusudii kufikia lengo jingine isipokuwa kusafisha taswira chafu ya nchi hiyo katika ngazi za kimataifa.

No comments:

Post a Comment