Kwa akali watu 17 wameuawa na wengine wengi
kujeruhiwa na askari wa jeshi la Cameroon, wakati wa maandamano ya
kushinikiza kujitenga maeneo ambayo wakazi wake wanazungumza Kiingereza,
katikati mwa nchi.
Shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International
limesema watu hao wameuawa na maafisa usalama wa nchi hiyo katika
machafuko na maandamano kwenye majimbo mawili yanayotaka kujtenga na
serikali kuu ya Yaunde.
Amnesty imesema raia wawili wa Nigeria ni miongoni mwa watu waliouawa
katika ghasia hizo baina ya waandamanaji na askari wa Cameroon.
Awali, shirika la habari la AFP liliripoti kuwa, miongoni mwa
wanaharakati waliouawa katika maandamano ya Jumapili ni wafungwa watano
waliokuwa wakijaribu kutoroka jela.
Raia wachache wa Cameroon wanaozungumza lugha ya Kiingereza wamekuwa
wakifanya maandamano ya mara kwa mara tangu Novemba mwaka jana
wakilalamikia kutengwa na serikali ya nchi hiyo.
Wafanyakazi wengi wa umma katika maeneo hayo pia wamekuwa wakifanya
mgomo kulalamikia kile wanachokitaja kama ubaguzi, ambapo wanasema raia
wa Cameroon wanaozungumza Kifaransa ndio wanaopewa nafasi za ajira.
No comments:
Post a Comment