Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu
(Bunge la Iran) amezungumzia mazungumzo yake ya hivi karibuni na maspika
wa mabunge ya nchi zilizoshiriki katika mkutano wa Umoja wa Mabunge
Duniani mjini Saint Petersburg, Russia na kusema kuwa, maspika wa
mabunge yote yaliyoshiriki kwenye mkutano huo wana wasiwasi na dukuduku
na vitendo vya kiuadui vya Wamarekani.
Shirika la habari la IRIB
limemnukuu Ali Larijani akisema hayo leo na kuongeza kuwa, katika
matamshi yake ya hivi karibuni, rais wa Marekani, Donald Trump ameonesha
sura halisi ya nchi yake lakini tab'an amelaumiwa na dunia nzima.
Amesema, maneno yasiyo na msingi
yaliyotolewa na rais wa Marekani yanaonesha namna alivyoshindwa
kuwakinaisha watu, hivyo, badala ya kutumia lugha ya mantiki, ameropoka
mambo yasiyo na msingi.
Itakumbukwa kuwa, tarehe 13 mwezi huu wa
Oktoba, rais wa Mareekani alitoa tuhuma zisizo na msingi dhidi ya Iran
na alisema pia kuwa, hatounga mkono ripoti nane zilizotolewa na Wakala
wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki IAEA zinazothibitisha kuwa Iran
imeheshimu kikamilifu makubaliano ya nyuklia ya JCPOA.
Akiwa mjini Saint Petersburg, Dk Ali
Larijani, Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu alionana na maspika
wenzake kadhaa kama vile wa Iraq, Mexico, Vietnam na Uturuki na
kujadiliana nao masuala mbalimbali ya pande mbili na masuala tata ya
eneo hili.
Mkutano wa siku tano waa Umoja wa
Mabunge Duniani ambao ulishirikisha ujumbe mbalimbali wa mabunge kutoka
zaidi ya nchi 150 ulianza siku ya Jumamosi mjini Saint Petersburg,
Russia chini ya kaulimbiu "Kueneza Utamaduni na Amani Kupitia Mijadala
ya Kidini na Kikaumu."
No comments:
Post a Comment