Uhispania imekataa miito ya mazungumzo na mamlaka ya
jimbo la Catalonia ambalo Jumapili liliendesha kura ya maoni yenye
utata, ambayo viongozi wa jimbo hilo wanasema matokeo yanayowapa idhini
ya kujitangazia uhuru
Viongozi wa jimbo la Catalonia wanatishia juu ya uwezekano wa kujitangazia uhuru wiki ijayo
Wito wa mazungumzo kati ya pande hizo mbili ulikuwa umetolewa na
Umoja wa Ulaya, lakini mvutano umezidi kushamiri, baada ya kiongozi wa
Catalonia, Carles Puigdemont kulaani uingiliaji kati wa mfalme wa
Uhispania Felipe VI, na baada ya serikali mjini Madrid kutupilia mbali
uwezekano wowote wa mazungumzo.
Tangazo la ofisi ya waziri mkuu
wa Uhispania, Mariano Rajoy, limesema kwamba katika demokrasia ipo njia
moja tu ya mazungumzo, nayo ni kufuata sheria. Ujumbe huo umesisitizwa
katika kauli ya naibu waziri mkuu Soraya Saenz de Santamaria,
aliyemshambulia vikali Puigdemont.
Soraya Saenz de Santamaria, Naibu Waziri Mkuu wa Uhispania
De
Santamaria amesema, ''Kila ujumbe unaotolewa na bwana Puigdemont ni
mvutano mpya, na njia isiyoelekea kokote. Kwa sababu hakuna demokrasia
nje ya sheria, hakuna haki nje ya sheria. Kwa muda mrefu bwana
Puigdemont anaishi nje ya sheria, nje ya hali halisi, nje ya fikra
sahihi''.
Catalonia kujitangazia uhuru wiki ijayo?
Huku
viongozi wa Catalonia wakiendelea na shinikizo lao la kutaka kujitenga
kutoka Uhispania, kiongozi wa jimbo hilo, Puigdemont, amesema sera za
serikali ya Uhispania ni za hatari. Na katika kikao cha bunge la jimbo
hilo jana, wabunge wanaounga mkono kujitenga wametaka kikao rasmi
Jumatatu ijayo, kujadili matokeo ya kura ya Jumapili iliyopita.
Vyanzo
kutoka ndani ya serikali ya jimbo hilo, vimelieleza shirika la habari
la AFP kuwa kulingana na mwenendo ulivyo, yumkini Catalonia ikatangaza
uhuru wake katika kikao hicho cha bunge.
Bila shaka hatua hiyo
inaweza kuupeleka mzozo kati ya Catalonia na serikali kuu ya mjini
Madrid katika hatua mbaya zaidi. Serikali hiyo, pamoja na mahakama,
vinaichukulia kura ya maoni ya Jumapili kuwa kinyume cha sheria.
Siogopi kukamatwa na kufungwa: Puigdemont
Carles Puigdemont, kinara wa harakati za kujitenga kwa Catalonia
Katika
mahojiano yake na gazeti la Bild la Ujerumani, kiongozi wa Catalonia
Puigdemont amesema hana hofu yoyote ya kuweza kukamatwa na kuwekwa jela.
''Siogopi tena kitu chochote kinachofanywa na serikali ya Uhispania'',
amesema kiongozi huyo, akikiri kwamba uwezekano wa kufungwa upo.
Hata
hivyo, ingawa serikali ya Uhispania imesema Puigdemont amevunja sheria,
hakuna dhamira yoyote ya serikali hiyo, wala ya mahakama, iliyoelezwa
kuhusiana na kumkamata, Puidemont.
Uchunguzi wa kura za maoni
uliofanywa kabla ya kura ya Jumapili, ulionyesha kwamba asilimia 40 tu
ya watu wa Catalonia, ndio wanaounga mkono jimbo hilo lenye mamlaka ya
ndani kujitenga na Uhispania na kujitangaza kama Jamhuri huru.
No comments:
Post a Comment