Maelfu ya watu wameandamana katika mitaa ya Barcelona,
Uhispania, baada ya mahakama nchini humo kuamuru viongozi wawili wa
jimbo la Catalonia lenye utawala wa ndani kutiwa mbaroni. Catalonia
yataka kujitenga.
Msemaji wa mji wa Barcelona amesema kiasi ya waandamanaji 200,000
waliokuwa wameshika mishumaa mikononi mwao walisikika wakipaza sauti za
kudai uhuru kabla ya kukaa kimya kwa dakika chache. Maandamano mengine
ya watu waliokuwa wameshika mishumaa mikononi yalifanyika katika miji
mingine ya jimbo la Catalonia kupinga kushikiliwa kwa viongozi wawili wa
jimbo hilo ambao ni Jordi Cuixart na Jordi Sanchez wanaotuhumiwa kwa
makosa ya uchochezi.
Mmmoja wa waandamanaji aliyefahamika kwa
jina la Elias Houriz alisikika akisema " Wanataka tuogope ili
tusifikirie juu ya uhuru wetu lakini hiyo itakuwa ni kinyume chake kwani
tunazidi kuwa na mwamuko kadiri siku zinavyosonga na mwishoni
tutafikia lengo letu" mwisho wa kumnukuu.
Naye kocha wa kilabu ya
Manchester City inayoshiriki ligi kuu ya kandanda ya England, Pep
Guardiola anayetokea pia katika jimbo la Catalonia alisema ushindi wa
timu yake hapo jana dhidi ya Napoli hapo jana usiku katika michuano ya
kilabu bingwa barani Ulaya ameutoa maalumu kama ishara ya kuwaunga mkono
viongozi wawili waliotiwa mbaroni na kutaka waachiwe huru haraka.
Guadiola ambaye amewahi kuinoa kilabu ya Barcelona alisema utaifa ni
muhimu kuliko kitu kingine chochote.
Maandamano hayo ya jana
yamefanyika huku muda ukizidi kukaribia kabla ya hapo kesho Alhamisi
ambayo ni tarehe iliyowekwa na serikali kuu ya mjini Madrid inayomtaka
kiongozi wa jimbo la Catalonia Carles Puigdemont kutamka wazi iwapo
anakusudia au kutokusudia kutangaza rasmi uhuru wa jimbo la Catalonia
kufuatia kura ya maoni iliyofanyika Oktoba 1 ambayo ilipigwa marufuku na
serikali ya mjini Madrid kwa maelezo kuwa ni kinyume cha katiba.
Puigbemont ataka majadiliano na Waziri Mkuu Mariano Rajoy
Kiongozi wa Catalonia ,Carles Puigdemont
Hata
hivyo kiongozi huyo amekataa hadi sasa kuitikia mwito huo akimtaka
Waziri Mkuu wa Uhispania Mariano Rajoy kukaa naye pamoja katika meza ya
majadiliano jambo ambalo Rajoy hakubaliani nalo hali ambayo inaweza
kuzidisha mgogoro wa kisiasa nchini humo ikiwa ni mara ya kwanza tangu
ilipojikomboa kutoka katika utawala wa kiimla mwaka 1977.
Hayo
yanajiri huku pia wabunge 50 katika bunge la nchi hiyo wakiwemo
wanaotoka katika jimbo la Catalonia wakibeba mabango ndani ya bunge hilo
kushinikiza kuachiwa huru viongozi waliotiwa mbaroni wakiwataja kuwa ni
wafungwa wa kisiasa.
Wakati huohuo sekta ya utalii ambayo ni
moja ya sekta zinazochangia kwa kiwango kikubwa uchumi wa nchi hiyo
inaonekana kuathirika kutokana na kukosekana kwa uthabiti tangu
kufanyika kura hiyo ya maoni hiyo ikiwa ni kwa mujibu wa Waziri Mkuu
Mariano Rajoy wakati alipolihutubia bunge la nchi hiyo akitetea hatua ya
serikali yake inayochukua katika kushughulikia mgogoro huo.
Mji wa Barcelona ambao ni mji mkuu wa Catalonia ni moja ya miji ambayo inatembelewa na watalii wengi nchini humo kila mwaka.
No comments:
Post a Comment