Polisi jijini Dar es Salaam Tanzania
imetangaza habari ya kukamatafa maguruneti saba na kusema inaamini
kwamba yangelitumiwa na watu wahalifu nchini humo.
Kwa
mujibu wa Kamanda wa Polisi kanda ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa,
jeshi hilo la polisi pia limefanikiwa kuua watuhumiwa watano wa uhalifu
katika matukio mawili tofauti na kwamba katika operesheni hizo mbali na
kukamata maguruneti hayo, limefanikiwa kukamata bunduki aina ya SMG
iliyofutwa namba, magazini yenye risasi 16, maganda 10 ya risasi za SMG
pamoja na pikipiki ambazo polisi wanasema zilikuwa zinatumiwa na
wahalifu hao kufanyia uhalifu.
Jeshi hilo limebainisha kwamba, silaha
hizo zimekamatwa na askari waliokuwa doria majira ya usiku eneo la
Msongola wilayani Ilala jijini Dar es Salaam, ambapo awali polisi hao
walikuwa wakiwafuatilia washukiwa hao wa uhalifu waliokuwa wamepanda
pikipiki moja wakiwa watatu.
Aidha Kamanda wa Polisi, Lazaro
Mambosasa amesema kuwa, baada ya watuhumiwa hao watatu kubaini kuwa
walikuwa wakifuatiliwa na polisi waliamua kuongeza mwendo na kuingia
barabara ya vumbi ambako walifyatua risasi.
Kamanda Mambosasa amesema, askari
waliwazidi nguvu watuhumiwa hao na kuwapiga risasi na kuanguka chini
pamoja na pikipiki hiyo. Katika tukio jingine, polisi wa Tanzania wameua
watu wawili baada ya kuwatuhumu kufanya ujambazi eneo la Mbagala
Zakheim ambako walipokea taarifa kutoka kwa wananchi kuwa watu hao
walipanga kuvamia maduka ya Tigo-Pesa na M-Pesa katika eneo hilo.
No comments:
Post a Comment