Thursday, November 2, 2017

RAIS MUGABE ATAKA KUREJESHWA HUKUMU YA KIFO NCHINI ZIMBABWE

Rais Mugabe ataka kurejeshwa hukumu ya kifo nchini Zimbabwe
Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe ametoa mwito wa kurejeshwa hukumu ya kifo baada ya watu 50 kutuma maombi ya kujaza nafasi iliyo wazi ya mtu wa kutekeleza adhabu ya kunyongwa.
Shirika la habari la AFP limeripoti kuwa, Mugabe ametoa wito huo hii leo Alkhamisi katika mji mkuu Harare, wakati wa mazishi ya veterani mashuhuri aliyepigania uhuru wa nchi hiyo ambapo ameongeza kuwa, "Nahisi kuna haja turejeshe hukumu ya kifo. Watu wanacheza na kifo kwa kuteleleza mauaji ya kiholela."
Hukumu ya kifo ambayo ipo katika vitabu vya sheria ya nchi hiyo haijatekelezwa tangu mwaka 2005, baada ya mtu aliyekuwa akitekeleza adhabu hiyo kuaga dunia.
Mashirika ya kutetea haki za binadamu ikiwemo Amnesty International yamekuwa yakiitaka Zimbabwe ipige marufuku hukumu ya kifo, ambayo inawakabili wafungwa 92.
Rais Mugabe wa Zimbabwe
Mugabe mwenye umri wa miaka 93 amekuwa akiiongoza Zimbabwe, koloni la zamani la Uingereza tangu nchi hiyo ilipopata uhuru mwaka 1980.
Baadhi ya wakosoaji wa serikali ya Zimbabwe wamekuwa wakimuona Mugabe kama kiongozi dikteta mwenye kuiongoza nchi hiyo kwa mkono wa chuma, huku akiwa na kauli ya mwisho kwenye mihimili yote ya serikali.

No comments:

Post a Comment