Monday, October 30, 2017

AMIR WA QATAR: IRAN NDIO NJIA PEKEE YA KUPITISHIA CHAKULA NA DAWA KATIKA KIPINDI CHA MZINGIRO

Amir wa Qatar: Iran ndio njia pekee ya kupitishia chakula na dawa katika kipindi cha mzingiro
Mfalme wa Qatar Sheikh Tamim bin Hamad Al Thani amesema Iran ndio njia pekee ya kupitishia chakula kwa ajili ya wananchi wa Qatar waliowekewa mzingiro; na akaongeza kwamba Saudi Arabia na nchi nyengine tatu za Kiarabu zinakula njama ya kuubadilisha utawala katika nchi yake.
Amir wa Qatar ameyasema hayo katika mahojiano na kanali ya televisheni ya CBS ya Marekani. Akijibu suali kuhusu dai kwamba Saudia na nchi nyengine tatu za Kiarabu zinaituhumu Doha kuwa ina urafiki wa kupita kiasi na Tehran, Sheikh Tamim Al Thani amesema: Iran ni jirani wa Qatar na serikali ya Doha ina uhusiano mpana wa kisiasa na Iran kuliko ilivyo na Saudia na waitifaki wake.
Mfalme wa Qatar amekumbusha matukio yaliyojiri miaka 21 nyuma na njama zilizofanywa kwa madhumuni ya kumpindua baba yake Shiekh Hamad bin Khalifa Al Thani na kuongeza kuwa: historia imeonyesha kuwa hapo kabla pia Saudi Arabia imefanya kila njia ili kuubadilisha utawala nchini Qatar.
Amir wa Qatar akimlaki Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Mohammad Javad Zarif alipotembelea Qatar hivi karibuni
Kuhusiana na kuwepo ofisi za kundi la kigaidi la Taliban mjini Doha, Mfalme wa Qatar ameeleza kuwa: Marekani ilitutaka tuwapokee Taliban na kuliruhusu kundi hilo lifungue ofisi yake mjini Doha ili Marekani iweze kufanya mazungumzo nalo.
Mbali na kutangaza utayari wa kufanya mazungumzo ya ana kwa ana na nchi nne zilizoiwekea vikwazo nchi yake ili kutatua mgogoro uliopo baina ya Doha na nchi hizo, Sheikh Tamim Al Thani amesema: Qatar inataka kumalizwa hitilafu zilizopo, lakini hakuna kitu chenye hadhi ya juu zaidi kuliko heshima na mamlaka ya kujitawala nchi hiyo.
Tangu tarehe 5 Juni mwaka huu, Saudi Arabia, Imarati (UAE), Bahrain na Misri zimevunja uhusiano wao wa kidiplomasia na Qatar kwa sababu ya misimamo ya Doha ambayo haiwiyani na sera za utawala wa Riyadh. Mbali na kuiwekea vikwazo, nchi hizo nne zimeifungia Qatar pia mipaka yao ya nchi kavu, baharini na angani.../

WATU 5 WAUAWA KATIKA MAANDAMANO DHIDI YA SERIKALI MJINI GOMA, KONGO DR

Watu 5 wauawa katika maandamano dhidi ya serikali katika mji wa Goma, Kongo DR
Maandamano ya wananchi ya kupinga serikali yaliyozusha makabiliano baina yao na polisi jana Jumatatu katika wilaya za Madjengon na Mabanga katika mji wa Goma mkoani Kivu ya Kaskazini nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo yamesababisha vifo vya watu watano.
Maandamano hayo ambayo yalijiri jana jioni yaliitishwa na makundi ya wanaharakati wa kupigania demokrasia na mengineyo kama sehemu ya mgomo mkubwa unaoshinikiza kuondoka madarakani Rais Joseph Kabila na kudhihirisha hasira za wananchi kwa kushindwa kuendeshwa uchaguzi wa rais huko Kongo ili kumchagua rais mpya. Waandamanaji walichoma moto matairi ya gari na hivyo kusababisha msongamano wa magari katika barabara za mji wa Goma. Maandamano mengine kama hayo yanatazamiwa kufanywa siku chache zijazo.
Rais Joseph Kabila wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo 
Mgogoro wa kisiasa Kongo DR umesababishwa na hatua ya Rais Joseph Kabila wa nchi hiyo kukataa kuachia madaraka baada ya muhula wake kumalizika mwezi Disemba mwaka jana. Uchaguzi mkuu ulipangwa kufanyika nchini humo kabla ya kumalizika mwaka huu chini ya makubaliano yaliyofikiwa kati ya serikali ya Kinshasa na mrengo wa upinzani. Hata hivyo imeelezwa kuwa kushindwa kutekelezwa hatua hiyo si jambo la kushangaza kwa kuzingatia kuwa Tume ya Uchaguzi ya Kongo mwezi Julai mwaka huu ilitangaza kuwa kuna uwezekano uchaguzi huo usifanyike mwaka huu kutokana na kuwepo matatizo ya bajeti na kuendelea machafuko nchini humo.

UHURU KENYATA ATANGAZWA RASMI MSHINDI WA UCHAGUZI WA RAIS KENYA ULIOSUSIWA NA MPINZANI WAKE

Uhuru Kenyatta atangazwa rasmi mshindi wa uchaguzi wa rais Kenya uliosusiwa na mpinzani wake
Mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka ya Kenya IEBC Wafula Chebukati amemtangaza Uhuru Kenyatta, mgombea urais kwa tiketi ya chama cha Jubilee Rais mteule na mgombea wake mwenza William Ruto kuwa Naibu Rais mteule baada ya kupata ushindi wa kishindo katika uchaguzi wa marudio wa rais uliofanyika siku ya Alkhamisi.
Akitangaza matokeo hayo jioni ya leo, Chebukati alisema uchaguzi huo ulikuwa huru, halali na wa haki.
Kwa mujibu wa matokeo yaliyotangazwa na mwenyekiti huyo wa IEBC, Kenyatta amejinyakulia kura 7,483,895 ambazo ni sawa na asilimia 98.27 ya kura zote halali zilizopigwa katika uchaguzi huo wa rais ambao ulisusiwa na mpinzani wake mkuu Raila Odinga.
Mwenyekiti wa IEBC, Wafula Chebukati
Zoezi la kutangaza matokeo limefanyika bila kujumuisha majimbo 25 ya mkoa wa Nyanza ambayo yalishindwa kupiga kura siku ya Alkhamisi kutokana na fujo na machafuko yaliyokwamisha upigaji kura katika majimbo hayo.
Chebukati amesisitiza kuwa masharti yaliyokuwa yamewekwa na Mahakama ya Juu iliyofuta matokeo ya uchaguzi wa rais wa Agosti 8 kwa ajili ya uchaguzi wa marudio yametekelezwa, hivyo uchaguzi huo ni halali, huru na wa haki.
Aidha amesema uchaguzi wa marudio wa rais umeendeshwa na timu mpya iliyojumuisha wafanyakazi wa IEBC kutoka kila pembe ya nchi. Ameongeza kuwa hali katika majimbo 25 ya mkoa wa Nyanza ilisababisha uchaguzi ushindwe kufanyika katika maeneo hayo.
Akizungumza mapema leo, Naibu Mwenyekiti wa IEBC Consolata Nkatha alisema kura za maeneo ambayo uchaguzi haukufanyika hazitoathiri matokeo rasmi ya uchaguzi huo.
Raila Odinga
Mgombea urais kwa tiketi ya muungano wa upinzani wa NASA Raila Odinga alisusia uchaguzi wa marudio akitaka pamoja na mambo mengine kutimuliwa maafisa waandamizi wa tume ya uchaguzi na kubadilishwa wachapishaji wa karatasi za kupigia kura na watayarishaji wa teknolojia itakayotumika katika mchakato wa uchaguzi huo.
Hayo yanajiri huku Wakenya wakisubiri kwa hisia tofauti msimamo wa kiongozi huyo wa upinzani ambao ameahidi kuutangaza baada ya rais Kenyatta kutangazwa rasmi mshindi wa uchaguzi wa marudio.../

Saturday, October 28, 2017

WAFUNGWA ZAIDI YA ELFU MOJA WA JELA YA TORA MISRI WAANZA MGOMO WA KULA

Wafungwa zaidi ya elfu moja wa jela ya Tora Misri waanza mgomo wa kula
Wafungwa wa jela yenye ulinzi mkali ya Tora mjini Cairo Misri wameanza mgomo wa kula chakula wakipinga mazingira mabaya yanatotawala jela hiyo.
Zaidi ya wafungwa elfu moja wa jela hiyo maarufu kwa jina la Jela la Nge wamenza mgomo wa kula wakilalamikia kunyimwa haki zao za kimsingi ikiwa ni pamoja na kuzuiwa jamaa zao kuwatembelea, kunyimwa huduma za afya na kadhalika.
Wakili Usama Biyumi anayeshughulikia kesi za wafungwa kadhaa wa jela hiyo amesema kuwa, ukatili wa idara ya jela hiyo dhidi ya wafungwa unaongezeka siku baada ya siku licha ya matakwa ya kukomeshwa mienendo hiyo.
Anesema kuwa maafisa wa jela hiyo wamekuwa wakizuia kuingizwa chakula kwa wafungwa na kupewa vyakula visivyokuwa salama.
Familia za wafungwa mbele ya jela ya Tora, Cairo
Biyumi ameongeza kuwa, mgomo huo ulianzishwa siku kadhaa zilizopita na baadhi ya wafungwa, na wafungwa wengine wa jela hiyo wamejiunga na wenzao hao baada ya matakwa yao kukataliwa na idara ya jela hiyo.
Wafungwa wa jela hiyo wananyimwa haki za kimsingi na manyanyaso yanashadidi zaidi kwa wafungwa wa kisiasa ambao wanashikiliwa katika seli zenye giza totoro na wanazuiwa kuzungumza na wenzao.
Misri imekuwa ikikosolewa na mashirika ya kimataifa ya kutetea haki za binadamu kutoka na ukatili na manyanyaso yanayofanywa dhidi ya wafungwa katika jela za nchi hiyo. 

MAGHALA YA NYUKLIA YA MAREKANI; CHANZO CHA UKOSEFU WA AMANI DUNIANI

Maghala ya nyuklia ya Marekani; chanzo cha ukosefu wa amani duniani
Makamu wa Rais wa Marekani ameyataja maghala ya silaha za nyuklia za nchi hiyo kuwa suala linalopelekea kuwepo amani duniani.
Akiwa ziarani kukitembelea kituo cha jeshi la anga cha Minot, Mike Pence Makamu wa Rais wa Marekani amesema hakuna nguvu duniani inayopelekea kuwepo amani sawa na maghala ya silaha za nyuklia za Marekani. 
Mike Pence, Makamu wa Rais wa Marekani 
Matamshi hayo yametolewa katika hali ambayo Marekani inatambulika ulimwenguni kama nchi pekee inayotumia silaha za nyuklia vitani. Miaka 70 iliyopita Wamarekani waliishambulia kwa mabomu ya nyuklia miji miwili ya Hiroshima na Nagasaki huko Japan na kusababisha vifo vya  raia wa nchi hiyo zaidi ya laki tatu baada ya kupitia mateso na masaibu chungu nzima. Kabla ya wakati huo, hakukuwa na silaha yoyote ya kivita iliyotengenezwa na binadamu iliyosababisha mauaji ya kutisha kama hayo. Mashambulizi hayo ya nyuklia yalizua hofu kubwa duniani kwa kadiri kwamba kwa mara ya kwanza katika historia, mwanadamu alikumbwa na wasiwasi wa kuangamizwa dunia nzima. 
Sehemu ya mji wa Hiroshima ulivyosambaratishwa na mashambulizi ya nyuklia ya Marekani 
Miaka minne tu baada ya Marekani kufanya mashambulio hayo ya nyuklia huko Japan, Umoja wa Kisovieti ulilifanyia jaribio bomu lake la kwanza la nyuklia na ni baada ya hapo ndipo kukaanza zama za ushindani wa silaha za nyuklia duniani. Ushindani huo mkubwa uliendelea na kuzifanya nchi mbili za Marekani na Urusi ya zamani mwezi Oktoba mwaka 1962 kukaribia kupigana vita vya nyuklia. Wakati huo kama Urusi ya zamani isingezirejesha karibu na Cuba meli zake zilizokuwa zimebeba makombora ya nyuklia, labda Rais wa wakati huo wa Marekani John F. Kennedy  angeamuru kupiganwa vita vya nyuklia; vita ambavyo katika masaa yake ya awali vingeweza kuua kwa uchache watu milioni 400. Marekani pekee hivi sasa imerundika katika maghala yake ya silaha, silaha za nyuklia ambazo zina uwezo wa kuiharibu dunia mara kadhaa. Hata kama Marekani katika miaka 70 iliyopita haijatumia silaha za aina hiyo, lakini imehusika kwa njia ya moja kwa moja au isiyo ya moja kwa moja katika kuenea kwa silaha hizo hatari. Dunia sasa inahofia makabiliano ya kinyuklia kati ya Marekani na Korea ya Kaskazini ambayo yanaweza kusababisha maafa makubwa kati ya pande mbili. 
Hasa ikitiliwa maanani kuwa amani ya dunia anayoikusudia Pence haitokani na uadilifu na ridhaa ya jamii, bali inatokana hofu ya Marekani kutekeleza mashambulizi ya nyuklia dhidi ya nchi nyingine. Kuwepo hofu na wasiwasi wa kusambaratika kikamilifu madola makubwa duniani miaka 70 baada ya kumalizika Vita vya Pili vya Dunia kumezuia kuibuka migogoro kati ya madola hayo. Wakati huohuo nchi zilizokuwa zikimiliki nguvu za nyuklia kama Marekani zilihamisha uhasama na mashindano yao ya kijeshi kutoka ndani ya ardhi za nchi hizo na kuyahamishia katika maeneo yaliyobaki nyuma kimaendeleo na yale yaliyokuwa yakistawi huko Asia, Afrika na Amerika ya Latini. Watu wa maeneo hayo walipoteza maisha na kugharimika pakubwa kufuatia vita hivyo baina ya madola makuu duniani. Kwa ibara nyingine ni kuwa, amani iliyoipata Marekani kwa silaha zake za nyuklia na waitifaki wake wa Ulaya haijakuwa na natija nyingine ghairi ya kusababisha vita na umwagaji damu katika maeneo mengine ya dunia

BURUNDI YACHUKUA HATUA YA KUREFUSHA KIPINDI CHA URAIS WA NKURUNZIZA

Burundi yachukua hatua ya kurefusha kipindi cha urais wa Nkurunziza
Baraza la mawaziri la Burundi limeunga mkono mabadiliko ya katiba ambayo yatamruhusu rais wa sasa wa nchi hiyo kubakia madarakani hadi mwaka 2034, suala ambalo limeitumbukiza zaidi nchi hiyo katika mgogoro wa kisiasa.
Afisa mmoja wa ngazi ya juu wa serikali ya Bujumbura amewaambia waandishi habari kuwa baraza la mawaziri limepitisha rasimu ya sheria ya kurekebisha katiba.
Marekebisho yaliyopendekezwa yanataka kuondolewa kikomo cha muda wa mihula miwili na kuongeza muda wa urais kuwa miaka saba.
Iwapo mapendekezo hayo yatapasishwa na Bunge la Burundi kiongozi wa sasa wa nchi hiyo anaweza kubakia madarakani hadi mwaka 20134.
Maafisa wa serikali ya Burundi wanasema kuwa, wataitisha kura ya maoni ya kupasisha mapendelekezo hayo hapo mwakani.
Kambi ya upinzani nchini Burundi umepinga muswada huo ambao inasema umetayarishwa kwa siri kwa shabaha ya kumbakisha Mkurunzinza madarakani.
Makamu mwenyekiti wa chama cha upinzani cha FRODEBU, Leonce Ngendakumana amekosoa vikali hatua hiyo akisisitiza kuwa marekebisho ya katiba hayapasi kufanyika katika anga ya mivutano na ukosema wa amani.
Machafuko ya ndani Burundi yamesababisha vifo vya raia wasio na hatia
Burundi imekumbwa na machafuko ya ndani tangu mwezi Aprili mwaka 2015 wakati kiongozi wa sasa wa nchi hiyo Pierre Nkurunziza alipotangaza kuwa atagombea tena kiti cha rais. Mamia ya watu wameuawa na maelfu ya wengine wamelazimika kuwa wakimbizi kutokana na machafuko ya ndani.  

ISMAIL HANIYA: JARIBIO LA ISRAEL LA KUMUUA AFISA MKUU WA HAMAS LIMEFELI

Ismail Haniya: jaribio la Israel la kumuua afisa mkuu wa HAMAS limefeli
Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina HAMAS amesema utawala wa Kizayuni wa Israel ndio umehusika katika jaribio la mauaji lililofeli dhidi ya afisa wa ngazi ya juu wa harakati hiyo.
Ismail Haniya aliyasema hayo jana Ijumaa, alipomtembelea Tawfiq Abu Na'im, Mkurugenzi Mkuu wa Vikosi vya Usalama wa Ndani vya HAMAS, aliyelazwa katika Hospitali ya Dar al-Shifa katika Ukanda wa Gaza, baada ya jaribio la mauaji dhidi yake.
Kiongozi huyo wa HAMAS amesema: "Vyombo vya Palestina vitawaadhibu waliohusika na jaribio hilo la mauaji, tunaamini kuwa utawala wa ghasibu wa Israel na washirika wake ndio waliohusika katika jaribio hilo la ukatili lililogonga mwamba."
Taarifa ya Waizara ya Mambo ya Ndani ya HAMAS imesema Abu Na'im alipata majeraha baada ya gari lake kushambuliwa kwa bomu katika kambi ya wakimbizi ya Nuseirat mapema hiyo jana.
Ismail Haniya, kiongozi wa HAMAS
Ismail Haniya amesema kamwe utawala wa Kizayuni wa Israel hauwezi kuvunja umoja na mshikamano wa Wapalestina na ni kosa kudhani kuwa njama kama hizi zinaweza kuwafanya Wapalestina waachane na jitihada zao za kukomboa ardhi zao zinazokaliwa kwa mabavu. 
Mapema mwezi huu, kiongozi huyo wa HAMAS sambamba na kuashiria hatua zilizochukuliwa hivi karibuni na harakati hiyo ya muqawama za kuondoa hitilafu kati yake na harakati ya Fat'h na juhudi ilizofanya kwa ajili ya kufikiwa maridhiano ya kitaifa baina ya Wapalestina, alibainisha kuwa: zama za hitilafu za ndani zimepita; na harakati ya HAMAS imeshaamua kulipa gharama zozote zinazoilazimu kwa ajili ya kufanikisha maridhiano rasmi ya kitaifa.

HALI YA KIBINADAMU YEMEN INASHTUA, SAUDIA YAENDELEZA HUJUMA

Hali ya kibinadamu Yemen inashtua, Saudia yaendeleza hujuma
Mkuu wa misaada ya kibinadamu katika Umoja wa Mataifa amesema hali ya kibinadamu nchini Yemen ni ya kushtua huku Saudi Arabia ikiendeleza hujuma dhidi ya nchi hiyo.
Akizungumza na waandishi wa habari katika mji mkuu wa Yemen, Sana'a, Mark Lowcock ambaye Jumamosi ya leo amemaliza safari ya siku tano nchini Yemen amesema kuwa, njia pekaa ya kumaliza vita Yemen ni kupitia mchakato wa kisiasa.
Lowcock amesema hali ya kibinadamu inazidi kuzorota huku ugonjwa wa kipindupindu ukienea kwa kasi ambayo haijawahi kushuhudiwa duniani. Amesema Yemen inakabiliwa na ukosefu mkubwa zaidi wa chakula duniani na kwamba idadi kubwa ya watu wamelazimika kuwa wakimbizi.
Watoto ni waathirika wa hujuma ya Saudia nchini Yemen
Vita vamizi vya Saudia na waitifaki wake dhidi ya Yemen vilianzishwa mwezi Machi mwaka 2015 kwa kisingizio cha kutaka kumrejesha madarakani rais wa nchi hiyo aliyejiuzulu na kuitoroka nchi Abd Rabbuh Mansur Hadi. Vita hivyo vingali vinaendelea kwa mwaka wa tatu sasa bila ya utawala wa Aal Saud na waitifaki wake kufikia malengo haramu waliyokusudia. Watu zaidi ya 13,000 , wengi wakiwa ni wanawake na watoto, wameuawa katika hujuma ya Saudia nchini Yemen.

UHURU KENYATTA AONGOZA KWA 96%, ODINGA ATAKA UCHAGUZI MPYA NDANI YA SIKU 90

Uhuru Kenyatta aongoza kwa 96%, Odinga ataka uchaguzi mpya ndani ya siku 90
Rais Uhuru Kenyatta anaongoza kwa asilimia 96 katika matokeo ya awali ya uchaguzi wa marudio wa urais uliofanyika Alkhamisi iliyopita nchini Kenya.
Matokeo ya awali ya Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka ya Kenya (IEBC) yanaonyesha kuwa Uhuru Kenyatta anaendelea kuongoza kwa kura zaidi ya milioni 7.
Wagombea wengine wanaomfuata kwa pamoja wamepata chini ya asilimia 5 ya kura zilizohesabiwa kufikia sasa.
Wananchi wa Kenya Alkhamisi walielekea kwenye masanduku ya kupigia kura katika uchaguzi wa marudio wa urais kufuatia kutenguliwa ule wa awali uliofanyika Agosti 8 mwaka huu.
Jana Ijumaa, Raila Odinga, kinara wa muungano wa NASA ambao umebadilishwa jina na sasa litafahamika kama Vuguvugu la Mageuzi NRM alisema kujitokeza idadi ndogo ya watu katika uchaguzi huo ni ishara tosha kuwa kulikuwa na uchakachuaji katika uchaguzi wa Agosti 8, huku akisisitiza kuwa lazima uchaguzi mwingine ufanyike ndani ya siku 90.
Raila Odinga
Mahakama ya Juu ya Kenya ilitengua matokeo ya uchaguzi huo wa rais kwa hoja kwamba IEBC ilifanya baadhi ya makosa katika mchakato wa uchaguzi. Muungano wa upinzani (Nasa) umewahimiza wafuasi wake kutoshiriki uchaguzi huo baada ya kiongozi wa muungano huo Raila Odinga kujiondoa katika kinyang'anyiro hicho.  
Katika hatua nyingine, IEBC imetangaza kuakhirisha tena zoezi la upigaji kura lililotazamiwa hii leo, katika kaunti nne za Kisumu, Migori, Homa Bay na Siaya, ambazo ni ngome za NASA, ambazo siku ya Alhamisi wakazi wake hawakupiga kura kwa sababu za kiusalama.

RAIS ROUHANI: IRAN INA HAMU YA KUONGEZA KIWANGO CHA UHUSIANO NA USHIRIKIANO WAKE NA TANZANIA

Rais Rouhani alipoonana na balozi wa Tanzania, Bw. Mbarouk Nassor Mbarouk Rais Rouhani alipoonana na balozi wa Tanzania, Bw. Mbarouk Nassor Mbarouk
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, Tanzania ni lango muhimu la kuingilia eneo la mashariki mwa Afrika na kwa kuzingatia kuwa Iran ina nafasi na uwezo mkubwa katika sekta mbalimbali na jambo hilo linaufanya wajibu wa kuimarishwa uhusiano wa nchi mbili kuwa na umuhimu wa kieneo.
Rais Rouhani amesema hayo leo Jumamosi hapa Tehran wakati alipopokea hati za utambulisho za Balozi  mpya wa Tanzania Bw. Mbarouk Nassor Mbarouk na kusisitiza kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ina hamu ya kuona kiwango cha uhusiano na ushirikiano wake na Tanzania kinakuwa kikubwa.
Mheshimiwa Rais pia amesema, kuna nyuga nyingi za kustawisha uhusiano wa Iran na Tanzania kama vile sekta ya madini na nishati na kwamba Jamhuri ya Kiislamu ya Iran iko tayari kuipatia Tanzania uzeofu wake katika masuala mbalimbali.
Kwa upande wake, Balozi Mbarouk ameashiria namna Tanzania inavyolipa umuhimu mkubwa suala la kuimarisha uhusiano wake wa Iran katika sekta tofauti na kusema: Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imepiga hatua nzuri katika nyuga nyingi na tofauti; za kisayansi, kiufundi na kiteknolojia hususan sekta na nishati na kwamba anaamini kuwa, Tanzania inaweza kufaidika na uzoefu wa Iran katika mambo tofauti.

Saturday, October 21, 2017

MAREKANI YAZIDI KUJIKITA KIJESHI AFRIKA; IDADI YA ASKARI WAKE BARANI HUMO YAONGEZEKA MARA TATU

Marekani yazidi kujikita kijeshi Afrika; idadi ya askari wake barani humo yaongezeka mara tatu
Gazeti la Kifaransa la Le Monde limeripoti kuwa Marekani imepanua wigo wa uingiliaji wake kijeshi katika nchi za Afrika kwa kuongeza idadi ya askari wake walioko kwenye nchi za bara hilo.
Kwa mujibu wa gazeti hilo, katika muendelezo wa sera za Washington za kudhamini maslahi yake, idadi ya askari wa Marekani wanaopelekwa katika nchi za Afrika kwa anuani ya "utoaji mafunzo, uratibu wa majeshi ya nchi za Kiafrika na kushiriki katika mapambano dhidi ya makundi ya kigaidi" imeongezeka mara tatu katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita.
Ramani ya vituo vya vijeshi na vinginevyo vya Marekani barani Afrika
Le Monde limeongeza kuwa, katika harakati inayolenga kudhamini manufaa na maslahi yake barani Afrika, Marekani imekuwa ikivuruga uthabiti ndani ya nchi za bara hilo ili kuongeza idadi ya vikosi vya jeshi lake, kiasi kwamba baada ya Mashariki ya Kati, bara Afrika limekuwa eneo la pili lenye uingiliaji mkubwa zaidi wa kijeshi wa Marekani duniani.
Kwa mujibu wa viongozi wa Marekani, kati ya askari elfu nane wa kikosi maalumu cha nchi hiyo ambao tangu ulipoanza mwaka huu wa 2017 wametumwa katika pembe mbalimbali za dunia, zaidi ya askari 1,300 wako barani Afrika na wengine karibu 5,000 wako katika eneo la Mashariki ya Kati.../

SHAMBULIO LA MOGADISHU, SOMALIA YAFIKIA 358 WALIOUAWA

  • Idadi ya waliouawa katika shambulio la Mogadishu, Somalia yafikia 358
Idadi ya watu waliouawa katika shambulio la kigaidi la siku ya Jumamosi iliyopita katika mji mkuu wa Somalia, Mogadishu imeongezeka na kufikia 358.
Waziri wa Habari wa Somalia Abdurahman Othman ametangaza kuwa kuwa kwa mujibu wa taarifa za karibuni kabisa kuhusu waathirika wa shambulio la kigaidi la mjini Mogadishu, watu wasiopungua 358 wameuawa, 228 wamejeruhiwa na wengine 56 hawajulikani waliko hadi sasa.
Abdurahman Othman ameongeza kuwa majeruhi 122 wa shambulio hilo la kigaidi wamesafirishwa kupelekwa Uturuki, Sudan na Kenya kwa ajili ya kupatiwa matibabu.
Shambulio hilo la tarehe 14 Oktoba lililofanywa kwa kutumia lori lililotegwa bomu lilitokea katika eneo la kibiashara la Hodan lenye msongamano mkubwa wa watu katika mji mkuu wa Somalia, Mogadishu.
Baadhi ya waliouawa na kujeruhiwa katika shambulio hilo
Majengo na magari yaliyokuweko umbali wa mita mia kadhaa yaliharibiwa vibaya na mripuko mkubwa uliosababishwa na bomu hilo na watu wengi waliteketea kwa moto wakiwa hai au miili yao kukatika vipande vipande.
Kabla ya shambulio la siku ya Jumamosi iliyopita, shambulio kubwa zaidi la kigaidi kutokea nchini Somalia lilikuwa la mwezi Oktoba mwaka 2011 ambapo watu 82 waliuawa na wengine 120 walijeruhiwa.
Ijapokuwa hadi sasa hakuna mtu au kundi lolote lililotangaza kuhusika na shambulio hilo lakini viongozi wa serikali ya Somalia hawana shaka kuwa kundi la kigaidi na kitakfiri la Al Shabab ndilo lililofanya shambulio hilo...

Friday, October 20, 2017

POLISI KENYA: WATU 4 WAMEUAWA KATIKA MAPAMBANO YA UPINZANI

Polisi Kenya: Watu 4 wameuawa katika maandamano ya upinzani
Polisi ya kenya imesema kuwa watu wanne wameuawa katika maandamano ya upinzani nchini humo katika kipindi cha wiki mbili zilizopita huku uchaguzi wa rais wa marudio ukikaribia kufanyika wiki ijayo. Polisi ya Kenya imesema kuwa watu hao waliuawa katika mapigano yaliyotokea kati ya maafisa polisi na waandamanaji.
Polisi imeeleza kuwa, watu hao waliaga dunia kati ya tarehe 2 mwezi huu na siku ya Jumatatu iliyopita.
Itakumbukwa kuwa, mapema wiki hii Shirika la Msamaha Duniani (Amnesty International) liliituhumu polisi ya Kenya kuwa imeuwa watu 67 katika maandamano ya upinzani yaliyofanywa siku kadhaa baada ya kutangazwa matokeo ya uchaguzi mkuu wa nchi hiyo uliofanyika Agosti nane.
Mapambano ya polisi yasababisha kuuliwa waaandamanaji wafuasi wa upinzani 
Mahakama ya Juu ya Kenya ilitengua ushindi wa Rais Uhuru Kenyatta ikisema kuwa uchaguzi wa rais uligubikwa na kasoro na kuagiza uchaguzi wa marudio. Kiongozi wa muungano wa upinzani (Nasa) Raila Odinga ambaye hoja yake ya kupinga matokeo ya uchaguzi wa rais mahakamani ilipelekea kutenguliwa matokeo ya uchaguzi huo, ametangaza kujitoa katika uchaguzi wa marudio akisema kuwa uchaguzi huo una hatari ya kugubikwa na kasoro kama zile zilizojitokeza katika uchaguzi uliopita.

Thursday, October 19, 2017

RAIS PUTIN: MACHAFUKO ENEO LA MASHARIKI YA KATI YANASABABISHWA NA KUPENDA KUJITANUA KWA BAADHI YA PANDE

Rais Putin: Machafuko eneo la Mashariki ya Kati yanasababishwa na kupenda kujitanua kwa baadhi ya pande.
Rais Vladmir Putin wa Russia amesema kuwa, hali ya sasa ya eneo la Mashariki ya Kati imekuwa mbaya kutokana na njama za baadhi ya madola katika kulisukuma eneo hilo kuelekea kwenye maslahi yao binafsi.
Rais Putin aliyasema hayo Alkhamisi ya jana na kuongeza kuwa, baadhi ya madola yanafanya njama kupitia mapinduzi ya kijeshi na nguvu za kijeshi, kwa lengo la kuyaelekeza matukio ya eneo la Mashariki ya Kati kwenda upande wa maslahi yao binafsi. Amefafanua kuwa, hadi sasa baadhi ya nchi badala ya kupambana na ugaidi, zinajaribu kuvuruga usalama na amani ya eneo hilo. Rais Vladmir Putin ameongeza kuwa, katika uwanja huo Russia kwa kushirikiana na serikali halali ya Syria na baadhi ya nchi za eneo, zinapambana na magaidi kwa kufuata sheria za kimataifa.

Uhasama uliopo kati ya Marekani na Russia
Aidha Rais Putin ameashiria mgogoro wa eneo la Peninsula ya Korea na kusema kuwa, ni lazima mgogoro huo kutatuliwa kwa njia za amani. Akieleza kuwa, baadhi ya nchi zinatekeleza njama kupitia njia za kisiasa kwa ajili ya kudhamini maslahi yao ya kiuchumi, amesema kuwa, baadhi ya hatua za kisiasa zina malengo ya kibiashara na kwamba lengo la vikwazo vilivyopitishwa hivi karibuni na kongresi ya Marekani dhidi ya Russia, ni kuiondoa Moscow katika soko la nishati barani Ulaya.

LARIJANI: VITENDO VYA CHUKI VYA WAMAREKANI NI DUKUDUKU LA MABUNGE YOTE

Larijani: Vitendo vya chuki vya Wamarekani ni dukuduku la mabunge yote
Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge la Iran) amezungumzia mazungumzo yake ya hivi karibuni na maspika wa mabunge ya nchi zilizoshiriki katika mkutano wa Umoja wa Mabunge Duniani mjini Saint Petersburg, Russia na kusema kuwa, maspika wa mabunge yote yaliyoshiriki kwenye mkutano huo wana wasiwasi na dukuduku na vitendo vya kiuadui vya Wamarekani.
Shirika la habari la IRIB limemnukuu Ali Larijani akisema hayo leo na kuongeza kuwa, katika matamshi yake ya hivi karibuni, rais wa Marekani, Donald Trump ameonesha sura halisi ya nchi yake lakini tab'an amelaumiwa na dunia nzima.
Amesema, maneno yasiyo na msingi yaliyotolewa na rais wa Marekani yanaonesha namna alivyoshindwa kuwakinaisha watu, hivyo, badala ya kutumia lugha ya mantiki, ameropoka mambo yasiyo na msingi.
Dk Ali Larijani akihutubia mkutano wa Umoja wa Mabunge Duniani mjini Saint Petersburg, Russia

Itakumbukwa kuwa, tarehe 13 mwezi huu wa Oktoba, rais wa Mareekani alitoa tuhuma zisizo na msingi dhidi ya Iran na alisema pia kuwa, hatounga mkono ripoti nane zilizotolewa na Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki IAEA zinazothibitisha kuwa Iran imeheshimu kikamilifu makubaliano ya nyuklia ya JCPOA.
Akiwa mjini Saint Petersburg, Dk Ali Larijani, Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu alionana na maspika wenzake kadhaa kama vile wa Iraq, Mexico, Vietnam na Uturuki na kujadiliana nao masuala mbalimbali ya pande mbili na masuala tata ya eneo hili.
Mkutano wa siku tano waa Umoja wa Mabunge Duniani ambao ulishirikisha ujumbe mbalimbali wa mabunge kutoka zaidi ya nchi 150 ulianza siku ya Jumamosi mjini Saint Petersburg, Russia chini ya kaulimbiu "Kueneza Utamaduni na Amani Kupitia Mijadala ya Kidini na Kikaumu."

Wednesday, October 18, 2017

MAELFU WAANDAMANA MJINI BARCELONA

Maelfu ya watu wameandamana katika mitaa ya Barcelona, Uhispania, baada ya mahakama nchini humo kuamuru viongozi wawili wa jimbo la Catalonia lenye utawala wa ndani kutiwa mbaroni. Catalonia yataka kujitenga.
Spanien Barcelona Demonstration gegen Inhaftierung (-picture alliance/AP Photo/M. Fernandez)
Msemaji wa mji wa Barcelona amesema kiasi ya waandamanaji 200,000 waliokuwa wameshika mishumaa mikononi mwao walisikika wakipaza sauti za kudai uhuru kabla ya kukaa kimya kwa dakika chache.  Maandamano mengine ya watu waliokuwa wameshika mishumaa mikononi yalifanyika katika miji mingine ya jimbo la Catalonia kupinga kushikiliwa kwa viongozi wawili wa jimbo hilo ambao ni Jordi Cuixart na Jordi Sanchez wanaotuhumiwa kwa makosa  ya uchochezi.
Mmmoja wa waandamanaji aliyefahamika kwa jina la Elias Houriz alisikika akisema " Wanataka tuogope ili tusifikirie juu ya uhuru wetu lakini hiyo itakuwa ni kinyume chake kwani tunazidi kuwa na mwamuko kadiri siku zinavyosonga na  mwishoni tutafikia lengo letu" mwisho wa kumnukuu.
Naye kocha wa kilabu ya Manchester City inayoshiriki ligi kuu ya kandanda ya  England, Pep Guardiola anayetokea pia katika jimbo la Catalonia alisema ushindi wa timu yake hapo jana dhidi ya Napoli hapo jana usiku  katika michuano ya kilabu bingwa barani Ulaya ameutoa maalumu kama ishara ya kuwaunga mkono viongozi wawili waliotiwa mbaroni na kutaka waachiwe huru haraka.  Guadiola ambaye amewahi kuinoa kilabu ya Barcelona alisema  utaifa ni muhimu kuliko kitu kingine chochote.
Maandamano hayo ya jana yamefanyika huku muda ukizidi kukaribia kabla ya hapo kesho Alhamisi ambayo ni tarehe iliyowekwa na serikali kuu ya mjini Madrid  inayomtaka kiongozi wa jimbo la Catalonia Carles Puigdemont kutamka wazi iwapo  anakusudia au kutokusudia kutangaza rasmi uhuru wa jimbo la Catalonia kufuatia kura ya maoni iliyofanyika Oktoba 1 ambayo ilipigwa marufuku na serikali ya mjini Madrid kwa maelezo kuwa ni kinyume cha katiba.

Puigbemont ataka majadiliano na Waziri Mkuu Mariano  Rajoy
Spanien Carles Puigdemont Premier der Regionalregierung (Reuters/I. Alvarado) Kiongozi wa Catalonia ,Carles Puigdemont
Hata hivyo kiongozi huyo amekataa hadi sasa kuitikia mwito huo akimtaka Waziri Mkuu  wa Uhispania Mariano Rajoy kukaa naye pamoja katika meza ya majadiliano jambo ambalo Rajoy hakubaliani nalo hali ambayo inaweza kuzidisha mgogoro wa kisiasa  nchini humo ikiwa ni mara ya kwanza tangu ilipojikomboa kutoka katika utawala wa kiimla mwaka 1977.
Hayo yanajiri huku pia wabunge 50 katika bunge la nchi hiyo wakiwemo wanaotoka katika jimbo la Catalonia wakibeba mabango ndani ya bunge hilo kushinikiza kuachiwa huru viongozi waliotiwa mbaroni wakiwataja kuwa ni wafungwa wa kisiasa.
Wakati huohuo sekta ya utalii ambayo ni moja ya sekta zinazochangia kwa kiwango kikubwa uchumi wa nchi hiyo inaonekana kuathirika  kutokana na kukosekana kwa uthabiti tangu kufanyika kura hiyo ya maoni  hiyo ikiwa ni kwa mujibu wa Waziri Mkuu Mariano Rajoy wakati alipolihutubia bunge la nchi hiyo akitetea hatua ya serikali  yake inayochukua katika kushughulikia mgogoro huo.
Mji wa Barcelona ambao ni mji mkuu wa Catalonia  ni moja  ya miji ambayo inatembelewa na watalii wengi nchini humo kila mwaka.

IEBC: NI VIGUMU KUHAKIKISHA UCHAGUZI WA HAKI

Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Kenya, Wafula Chebukati, amewataka maafisa wa Tume hiyo waliotajwa kuvuruga uchaguzi mkuu uliobatilishwa kuachia nafasi zao. Amewatuhumu pia wanasiasa kwa kuizingira Tume hiyo.
Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Kenya, Wafula Chebukati (picture-alliance/AP Photo/S. A. Azim)
Siku nane kabla ya kufanyika uchaguzi mpya wa urais hali ya wasiwasi imetanda juu ya iwapo uchaguzi huo utafanyika kwenye mazingira bora na ya kuaminika kama ilivyoamualiwa na mahakama ya Juu. Mwenyekiti wa Tume hiyo Wafula Chebukati ameelezea wasiwasi wake kuhusu mshikamano wa maafisa kwenye Tume hiyo suala ambalo limeigawa tume hiyo na kuliweka taifa katika njiapanda. Chebukati ameeleza kuwa mapendekezo yake yote ya kuhakikisha kuwa uchaguzi unaendeshwa kwa njia huru na ya haki yamekuwa yakipigwa teke na makamishna wenzake.
Upande wa upinzani umekuwa ukishinikiza kuondolewa kwa Afisa mkuu mtendaji wa Tume hiyo Ezra Chiloba na maafisa wengine sita waondoke afisini, hatua ambayo haijatekelezwa. "Katika hali kama hiyo ni vigumu kutoa hakikisho kwa uchaguzi huru, wa haki na wa kuaminika, Bila ya mageuzi muhimu katika sektariati ya tume uchaguzi huru na wa haki utavurugwa hivyo nawaomba maafisa waliotajwa kavuruga uchaguzi uliopita kungatuka na kuruhusu kikundi nilichobuni kufanya kazi," amesema Chebukati.
Kwenye mkutano na wanahabari Chebukati amesema kuna nafasi ya kunusuru utendaji kazi wa tume hiyo iwapo makamisha wote wataweka tofauti zao kando na kuweka maslahi ya taifa mbele. Huku wengi wakitarajia kuwa angejiuzulu, Chebukati alishikilia kuwa hatajiuzulu. Hata hivyo alikuwa mwepesi wa kusema kuwa hatakuwa sehemu ya kikundi kitakachovuruga uchaguzi ujao kwa manaufaa ya muda mfupi. Amewaonya wanasiasa ambao wanawatisha maafisa wake. "Nawapa wanasiasa wote kadi ya njano, sitaruhusu vitisho kwa maafisa wangu, sitaruhusu kuingiliwa kwa tume yangu tena. Wakenya wanalipa pesa kubwa kugharamia uchaguzi huu. Na kama mwenye wajibu sintoacha pesa za wakenya na washirika wetu zipotee," ameahidi mwenyekiti huyo.
Kenyatta ataka watu waiombee nchi
Kiongozi wa upinzani Raila Odinga amesusia uchaguzi (Reuters/J. Okanga) Kiongozi wa upinzani Raila Odinga amesusia uchaguzi
Akigusia suala la kamishna Roslyn Akombe aliyejiuzulu mapema leo, Chebukati amemtaja Akombe kuwa mmoja wa watumishi wakakamavu waliojitolea kuhudumu kwenye Tume hiyo. Amelaumu tume kwa kushindwa kutoa mazingira yanayostahili kwa kamishna huyo, sababu iliyomfanya ajiuzulu. Wakati huo huo rais Uhuru Kenyatta na naibu wake William Ruto wameendelea na kampeni zao, huku wakiwataka wafuasi wao kujitokeza kwa wingi kurejesha chama cha Jubilee mamlakani kwa kipindi kingine cha miaka mitano. Wawili hao wamesema kuwa hawataruhusu kiongozi wa upinzani Raila Odinga kusitisha mchakato wa uchaguzi mpya wa urais. "Wewe Bwana Odinga kwasababu tumekubali haki ya kukaa nyumbani, kwanini unafikiria kuwa wewe uko na haki ya kukataza wakenya wale ambao wanataka kupiga kura wapige kura, hiyo hatuwezi kukubali," amesema Kenyatta.
Naye Makamu wa Rais William Ruto akaongezea, "Sasa huyu mtu wa vitendawili anasema kuwa atasimamisha uchaguzi, kama Uhuru Kenyatta ambaye ni amiri jeshi mkuu wa majeshi yote ya Kenya, hawezi kusimamisha uchaguzi, sasa mtu wa vitendawili na uganga ataweza, aache mzchezo."
Ili kujikwamua katika mzozo wa sasa, taifa litahitaji vitendo na nia nzuri zaidi ya matamshi kutoka kwa wanasiasa ambao wanavutia upande wao kwani kwa sasa taifa limegawanyika. Mapema Rais Kenyatta aliwataka wakenya wa dini zote kutenga siku ya Jumapili kuombea taifa huku wachambuzi wa masuala ya siasa wakimtaka kuketi meza moja na Odinga kwa mazungumzo.

ISRAEL YAPATWA NA PRESHA BAADA YA VISIMA VYOA MAFUTA VYA KIRKUK KUDHIBITIWA NA RERIKALI YA BAGHDAD

Israel yapatwa na presha baada ya visima vya mafuta vya Kirkuk kudhibitiwa na serikali ya Baghdad
Kiongozi wa eneo la Kurdistan Iraq anayechochewa na Israel kujitenga
Utawala haramu wa Kizayuni wa Israel umekumbwa na wasi wasi na wahka mkubwa kutokana na Wakurdi kuondolewa katika visima vya mafuta vya eneo la Kirkuk na kisha kudhibitiwa na jeshi la serikali kuu ya Iraq.
Visima vya mafuta vya eneo hilo, ndivyo vilivyokuwa vyanzo vikuu vya kudhamini mafuta ya utawala haramu wa Israel kutokea Kurdistan. Habari zaidi zinaeleza kuwa, kusonga mbele jeshi la Iraq katika mji wa Kirkuk na kudhibitiwa visima hivyo, kumeutia khofu kubwa utawala wa Kizayuni kwa kuwa hatua hiyo inahatarisha upatikanaji wa nishati ya mafuta kwa Tel Aviv.
Kanali ya Pili ya televisheni ya Israel sambamba na kuthibitisha habari hiyo imetangaza kuwa, visima vya mafuta vilivyodhibitiwa na jeshi la Iraq katika eneo la Kirkuk vilikuwa chanzo kikuu cha kudhaminiwa mafuta ya Israel. Ehud Yarri, mchambuzi mashuhuri wa Israel ameiambia kanali hiyo ya Kizayuni kwamba, mji wa Kirkuk wa Iraq, ni moja ya miji tajiri ya mafuta na muhimu sana kwa Iraq na kwamba jeshi la serikali ya Baghdad limeweza kuudhibiti mji huo bila ya vita. Mafuta ya eneo la Kurdistan nchini Iraq yalikuwa yanasafirishwa kwenda Israel kupitia mipaka ya Uturuki.
Jeshi la Iraq lilipodhibiti mambo huko la Kirkuk
Kwa mujibu wa duru za kuaminika, nusu nzima ya mafuta yaliyokuwa yakichimbwa katika visima vya mafuta vya eneo la Kirkuk mwaka 2017 ilitumwa kwenda Israel na ilikuwa ni mapipa laki tatu kwa siku. Ni kwa ajili hiyo ndio maana utawala wa Kizayuni wa Israel ulikuwa ukilichochea eneo la Kurdistan kujitenga na serikali kuu ya Baghdad.

POLISI TANZANIA WAUA WATUHUMIWA WATANO WA UJAMBAZI NA KUKAMATA MAGURUNETI SABA

Polisi Tanzania waua watuhumiwa watano wa ujambazi na kukamata maguruneti saba
Polisi jijini Dar es Salaam Tanzania imetangaza habari ya kukamatafa maguruneti saba na kusema inaamini kwamba yangelitumiwa na watu wahalifu nchini humo.
Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi kanda ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa, jeshi hilo la polisi pia limefanikiwa kuua watuhumiwa watano wa uhalifu katika matukio mawili tofauti na kwamba katika operesheni hizo mbali na kukamata maguruneti hayo, limefanikiwa kukamata bunduki aina ya SMG iliyofutwa namba, magazini yenye risasi 16, maganda 10 ya risasi za SMG pamoja na pikipiki ambazo polisi wanasema zilikuwa zinatumiwa na wahalifu hao kufanyia uhalifu.
Jeshi hilo limebainisha kwamba, silaha hizo zimekamatwa na askari waliokuwa doria majira ya usiku eneo la Msongola wilayani Ilala jijini Dar es Salaam, ambapo awali polisi hao walikuwa wakiwafuatilia washukiwa hao wa uhalifu waliokuwa wamepanda pikipiki moja wakiwa watatu.
Aidha Kamanda wa Polisi, Lazaro Mambosasa amesema kuwa, baada ya watuhumiwa hao watatu kubaini kuwa walikuwa wakifuatiliwa na polisi waliamua kuongeza mwendo na kuingia barabara ya vumbi ambako walifyatua risasi.
Kamanda Mambosasa amesema, askari waliwazidi nguvu watuhumiwa hao na kuwapiga risasi na kuanguka chini pamoja na pikipiki hiyo. Katika tukio jingine, polisi wa Tanzania wameua watu wawili baada ya kuwatuhumu kufanya ujambazi eneo la Mbagala Zakheim ambako walipokea taarifa kutoka kwa wananchi kuwa watu hao walipanga kuvamia maduka ya Tigo-Pesa na M-Pesa katika eneo hilo.

UGANDA YAPIGA MARUFUKU MAANDAMANO YA KUPINGA KUONDOLEWA KIPENGELE CHA UMURI KATIKA KATIKA KUGOMBEA URAIS

Kiongozi wa upinzani, Daktari Kiiza Besigye akipandishwa kwenye gari la polisi baada ya kusambaratishwa maandamano Kiongozi wa upinzani, Daktari Kiiza Besigye akipandishwa kwenye gari la polisi baada ya kusambaratishwa maandamano
Jeshi la polisi nchini Uganda leo (Jumatano) limepiga marufuku kile lilichokiita ni maandamano haramu ya kupinga mpango wa kuondoa kipengee ya umri katika kugombea urais. Juhudi za kuondoa kipengee hicho zina nia ya kumfungulia njia Rais Yoweri Museveni kuendelea kubakia madarakani bila ya kufungwa na kipengee hicho.
Muswada wa kuondoa kipengee cha umri wa kugombea urais kiliwasilishwa katika bunge la Uganda mwezi uliopoita na hivi sasa wabunge wanajadiliana na wananchi wa kawaida kutaka kujua maoni yao. Hata hivyo juhudi hizo zimekumbwa na upinzani kutoka sehemu mbalimbali.
Rais Yoweri Museveni wa Uganda

Msaidizi wa Inspekta Mkuu wa Polisi wa Uganda, Assuman Mugenyi amesema kuwa, majadiliano hayo yanaruhusiwa lakini si ruhusa kufanya maandamano yasiyo na kibali, kuchochea machafuko, kufanya kampeni za chuki, kutumia maneno ya kashfa na vitu kama hivyo.
Kwa kawaida wapinzani hawapewi vibali vya kuandamana nchini Uganda na hii ina maana kwamba maandamano yoyote ya wapinzani ni kinyume cha sheria.
Musenyi ametoa amri kwa maafisa wa polisi kuhakikisha kuwa wabunge wanafanya mashauriano hayo kwa utulivu na amani tena katika majimbo yao tu.
Jana usiku, polisi walifyatua mabomu ya kutoa machozi na kutumia risasi za plastiki kutawanya mamia ya wapinzani wa kufutwa kipengee cha umri kinachomzuia Museveni kugombea tena urais.
Winnie Kiiza, Mkuu wa Mrengo wa Upinzani katika bunge la Uganda

Rais Yoweri Kaguta Museveni amekuwa akiitawala Uganda kwa miaka 30 sasa. Umri wake hivi sasa ni miaka 73 wakati katiba ya Uganda imepiga marufuku mtu kugombea urais akiwa na umri wa miaka 75.
Mkuu wa mrengo wa upinzani katika bunge la Uganda, Winne Kiiza amesema kuwa, amri hiyo ya polisi ni kinyume cha katiba na ameahidi kukabiliana na amri hiyo kwa njia yoyote ile.
Hadi hivi sasa haijajulikana muswada huo utarejeshwa lini Bungeni kwa ajili ya kupigiwa kura.