Rais Muhammadu Buhari wa Nigeria amesema
kuwa, raia wote wa nchi hiyo ambao wamekwama huko Libya watarejeshwa
nyumbani na kusaidiwa kurejelea maisha ya kawaida.
Akizungumzia video za karibuni
ambazo zimekuwa zikiwaonesha Waafrika wakiuzwa kwenye mnada wa watumwa
nchini Libya, Rais Buhari amesema inasikitisha sana kwamba "baadhi ya
raia wa Nigeria wanauzwa kama mbuzi kwa dola kadhaa huko Libya".
Rais wa Nigeria ameonekana pia kushangaa
iwapo raia wa Libya walijifunza lolote la maana tangu kuondolewa
madarakani kwa Kanali Muammar Gaddafi mwaka 2011.
''Walichojifunza pekee ni kuwapiga watu
risasi na kuua. Hawakujifunza kuwa mafundi wa umeme, mafundi wa mabomba
au ufundi wowote ule," amesema.
Hayo yanajiri katika hali ambayo, radiamali mbalimbali zimeendelea
kutolewa kuhusiana na taarifa za kuweko biashara ya utumwa nchini Libya.
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa
limetoa mwito wa kuendeshwa vita dhidi ya magendo ya binadamu na
biashara ya utumwa katika bara la Afrika.
Filippo Grandi, Kamishna Mkuu wa Shirika
la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa UNHCR amesema, kuna haja ya
kukabiliana na biashara ya utumwa na vitendo vingine vya ukiukaji wa
haki za binadamu vinavyofanywa dhidi ya wahajiri wanaopitia Libya wakiwa
na nia ya kuelekea barani Ulaya kutafuta maisha mazuri.
Itakumbukwa kuwa, hivi kkaribuuni,
televisheni ya CNN ilirusha hewani mubashara mnada wa kuuza Waafrika
huko nchini Libya ambapo kila mtu alikuwa akiuzwa kwa dola zisizopungua
400 za Kimarekani.
No comments:
Post a Comment