Wednesday, November 15, 2017

RAIS ROBERT MUGABE WA ZIMBABWE AONDOLEWA MADARAKANI

Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe aondolewa madarakani
Jeshi la Zimbabwe limemuondoa madarakani rais wa nchi hiyo Robert Gabriel Mugabe.
Kwa mujibu wa shirika la habari la Reuters jeshi limetangaza kuwa Mugabe na familia yake wako kwenye kizuizi cha nyumbani na kuongeza kuwa jeshi hilo litawapandisha kizimbani wale liliowataja kama "wahalifu" waliomzunguka kiongozi huyo ambao wamesababishia madhara na hasara za kiuchumi na kijamii nchi hiyo.
Sambamba na hayo ofisi ya rais wa Afrika Kusini imetangaza kuwa Mugabe mwenyewe amezungumza kwa njia ya simu na rais wa nchi hiyo Jacob Zuma na kumueleza kwamba amezuiliwa nyumbani kwake lakini yuko salama.
Duru za serikali zimeripoti kuwa Waziri wa Fedha Ignatius Chombo ambaye ni mmoja wa viongozi wa mrengo unaojulikana kama G40 unaomuunga mkono mke wa Mugabe Bi Grace amewekwa kizuizini na jeshi.
Grace Mugabe
Imeelezwa kuwa hatua ya jeshi kuingilia kati masuala ya kisiasa na uongozi nchini Zimbabwe imelenga kumzuia Rais Mugabe kumfanya mkewe Grace mrithi wa urais baada yake.
Aliyekuwa makamu wa rais wa Zimbabwe  Emmerson Mnangagwa amesema hakuna mapinduzi ya kijeshi yaliyotokea nchini humo na kwamba mchakato wa mapokezano ya madaraka umo katika hali ya kufanyika pasi na kutokea umwagaji damu wowote.
Hayo yanajiri huku chama kikuu cha upinzani cha MDC kikitoa wito wa kurejeshwa demokrasia nchini kwa msingi wa kuheshimu katiba.
Askari wa jeshi wakiwa kando ya magari ya deraya kandokando ya mji wa Harare
Chama hicho kimeeleza kuwa kina matumaini kwamba uingiliaji kati wa jeshi utapelekea kuundwa serikali ya kidemokrasia, yenye uthabiti na ya kuiletea Zimbabwe maendeleo.
Hatua iliyochukuliwa hivi karibuni na Mugabe mwenye umri wa miaka 93 ya kumuuzulu  makamu wake Emmerson Mnangagwa iliitumbukiza Zimbabwe kwenye mgogoro na mvutano ambao haujawahi kushuhudiwa.
Hapo jana jeshi lilichukua hatua, kwanza ya kulidhibiti jengo la televisheni ya taifa na kisha kusambaza magari mengi ya deraya katika barabara za kandokando ya mji mkuu Harare.
Jeshi la Zimbabwe limechukua hatua hiyo huku kamanda wake mkuu akiwa ameshaonya hapo kabla kwamba wanajeshi wanaweza kuchukua hatua ya kuingilia kati endapo mwenendo wa kuwauzulu na kuwavua nyadhifa zao viongozi ndani ya chama tawala ZANU-PF utaendelea.../

No comments:

Post a Comment