Khalid bin Farhan Al Saud, Mwanamfalme ambaye
amejitenga na utawala wa Aal-Saud, amesema kuwa kabla ya kuomba hifadhi
ya kisiasa nchini Ujerumani, kwa muda mrefu alikuwa akiishi kwa
wasiwasi na mashaka mengi nchini Saudia.
Farhan Al Saud ambaye ni mpinzani
wa utawala wa Saudia ameyasema hayo katika mahojiano na kanali moja ya
televisheni ya Ujerumani ambapo amezungumzia kutokuwepo uhuru wa
kujieleza na ukiukwaji haki za binadamu uliokithiri nchini humo. Amesema
kuwa, baada ya kupinga utawala wa Aal-Saud na kuwasilisha malalamiko ya
kuwepo uhuru wa kiraia, alikumbwa na mashinikizo na udhia mkubwa kiasi
kwamba alilazimika kujiuzulu jeshini na kutoroka nchi.
Mwanamfalme huyo wa utawala wa Aal-Saud
sambamba na kusisitiza kuwa, haogopi kitu chochote amesema zaidi ya
mapendekezo 50 yamewasilishwa kwake kutoka ubalozi wa Saudia nchini
Ujerumani yakimtaka aandike taarifa ya kuomba msamaha kwa Mfalme Salman
bin Abdulaziz Al Saud lakini amekataa kufanya hivyo. Khalid bin Farhan
Al Saud ameashiria pia njama za viongozi wa Saudia za kumuwekea
mashinikizo na hata ikiwezekana kumtia mbaroni kwa kumtumia dada yake
anayeitwa 'Ibtisam' na anaeshikiliwa katika kifungo cha nyumbani nchini
Saudia na kusema kuwa, watawala wa ukoo wa Aal-Saud kwa mara kadhaa
walimtisha kwamba ikiwa hatoacha kufichua machafu ya utawala wa kifalme
wa Saudia, watamuua dada yake.
Kwa mujibu wa takwimu na ripoti za ndani
nchini Saudia, zaidi ya wanaharakati wa kisiasa na wanasheria elfu 30
wanashikiliwa katika jela mbalimbali za utawala huo wa Aal-Saud.
No comments:
Post a Comment