Viongozi wa chama tawala nchini Zimbabwe cha
ZANU-PF wanatazamiwa kupitisha uamuzi wa kumuondoa uongozini Rais wa
nchi hiyo na kiongozi wa chama hicho Robert Gabriel Mugabe, ambaye
amekuwa akiiongoza nchi hiyo tangu ilipopata uhuru wake miaka 37
iliyopita. Hayo ni kwa mujibu wa duru mbili kutoka ndani ya chama hicho.
Kikao cha
dharura kamati kuu ya ZANU-PF kilitazamiwa kufanyika mapema leo
kufikiria uamuzi wa kumuondoa kwenye uongozi Mugabe mwenye umri wa miaka
93, siku chache baada ya jeshi kutwaa madaraka kwa lengo la kile
kilichotajwa kama kuwachukulia hatua "wahalifu" waliomzunguka kiongozi
huyo.
Wakati huohuo,
ikimnukuu kiongozi wa Kanisa Katoliki ambaye ni mpatanishi katika
mazungumzo na Mugabe, televisheni ya taifa ya Zimbabwe imetangaza kuwa
kiongozi huyo atakutana na makamanda wa jeshi hii leo.
Kamati kuu ya
chama tawala Zanu-pf inatazamiwa kumrejesha tena kwenye wadhifa wake
makamu mwenyekiti wa chama Emmerson Mnangagwa, ambaye kutimuliwa kwake
kama Makamu wa Rais na makamu mwenyekiti wa chama hicho kulipelekea
jeshi kuingilia kati na kutwaa madaraka ya nchi.
Mke wa Mugabe Grace, yeye anatazamiwa kuvuliwa uongozi wa tawi la wanawake la chama cha Zanu-pf.
Hayo yanajiri huku Rais Mugabe akiendelea kukataa kung'atuka
madarakani licha ya kushuhudia kwa macho yake kutokea nyumbani kwake
alikowekwa kizuzini jinsi uungaji mkono aliokuwa nao kutoka kwenye
chama, vyombo vya ulinzi na usalama pamoja na wananchi ukiyeyuka ndani
ya muda wa chini ya siku tatu tu.
Mpwa wa kiongozi
huyo Patrick Zhuwao amevieleza vyombo vya habari kuwa Mugabe na mkewe
"wako tayari kufa kwa kile wanachokiona kuwa ndio sahihi" kuliko kuachia
ngazi ili kuhalalisha kile alichokielezea kama mapinduzi ya kijeshi.
Hayo yanajiri
huku makumi ya maelfu ya wananchi wakimiminika kwenye barabara za miji
ya nchi hiyo hususan mji mkuu Harare kushinikiza kiongozi huyo ang'atuke
madarakani sambamba na kusherehekea kile wanachokieleza kama mwisho wa
enzi za miaka karibu 40 ya utawala wake…/
No comments:
Post a Comment