Jumuiya ya Madaktari Wasio na Mipaka (MSF)
imeripoti kuwa mapigano makali yangali yanaendelea katika mkoa wa Ouham
kaskazini mwa Jamhuri ya Afrika ya Kati.
Taarifa iliyotolewa na jumuiya hiyo ya kimataifa ya tiba, mbali
na kueleza wasiwasi uliopo kutokana na kuendelea mapigano
yaliyochanganyika na vitendo vya ukatili kwenye maeneo mabalimbali ya
mkoa wa Ouham imeongeza kuwa watu wasiopungua wawili waliuawa na wengine
21 walijeruhiwa katika mapigano yaliyotokea wiki iliyopita baina ya
makundi mawili hasimu.
Kwa mujibu wa duru zenye mfungamano na Umoja wa Mataifa mapigano hayo
yalihusisha kundi la waasi wa Kikristo la Anti-Balaka na wanamgambo wa
kundi la wabeba silaha liitwalo Harakati ya Kizalendo kwa ajili ya
Jamhuri ya Afrika ya Kati (MPC) ambalo limeundwa na baadhi ya waasi wa
zamani wa harakati ya Seleka.
Jamhuri ya Afrika ya Kati imekuwa ikishuhudia mapigano na machafuko
tangu aliyekuwa rais wa nchi hiyo François Bozizé alipoondolewa
madarakani Machi 24, mwaka 2013 na harakati hiyo.
Licha ya kufanyika uchaguzi wa rais mnamo mwezi Machi mwaka uliopita
wa 2016 uliomleta madarakani rais wa sasa Faustin-Archange Touadéra,
hata hivyo serikali ya Bangui inayoongozwa na kiongozi huyo hadi sasa
imeshindwa kurejesha amani na uthabiti nchini humo.
Wakati Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres alipofanya
safari nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati katikati ya mwezi uliopita wa
Oktoba aliashiria kuwa anakusudia kutoa wito wa kuongezwa askari wa
ziada 9,000 katika operesheni za kulinda amani nchini humo hasa kwa
ajili ya kuwalinda raia.../
No comments:
Post a Comment