Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imelaani vikali
hujuma ya kigaidi wakati wa Sala ya Ijumaa msikitini katika mkoa wa
Sinai Kaskazini nchini Misri.
Katika taarifa kupitia ukurasa wake wa Twitter, Waziri wa Mambo
ya Nje ya Iran Mohammad Jawad Zarif amesema ugaidi hauheshimu thamani
za Kiungu na kibinadamu.
Zarif ameongeza kuwa: "Kwa mara nyingine ugaidi umetoa pigo kwa taifa
azizi la Misri na kwa mara nyingine kuthibitisha kuwa hautafautishi
mahali hata ndani ya msikiti na maeneo mengine ya ibada."
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amelaani vikali hujuma hiyo ya kigaidi
na kumuomba Mwenyezi Mungu awarehemu mashahidi na kuwapa majeruhi nafuu
ya haraka.
Jana Waislamu wasiopungua 235 wameuawa na wengine zaidi ya 110
kujeruhiwa katika shambulizi la magaidi wakufurishaji dhidi ya msikiti
mmoja wa Twariqa katika Peninsula ya Sinai nchini Misri.
Duru za polisi nchini humo zimesema genge la kigaidi limeushambulia
Msikiti wa al-Rawdhah ulioko katika mji wa Bir al-Abd, yapata kilomita
40 kutoka mji wa Al-Arish, makao makuu ya mkoa wa Sinai Kaskazini.
Rais Abdulfattah al-Sisi wa Misri sanjari na kulaani hujuma hiyo,
ameitisha mkutano wa dharura na vyombo vya usalama huku akitangaza siku
tatu za maombolezo ya kitaifa, kufuatia ukatili huo wa magaidi.
No comments:
Post a Comment