Hatimaye baada ya takribani wiki moja ya
changamoto, mivutano na uingiliaji wa jeshi hatimaye Rais Robert Gabriel
Mugabe wa Zimbabwe ameng'atuka madarakani. Mugabe amechukua hatua hiyo
baada ya Bunge kuanzisha mchakato wa kumsaili kwa lengo la kumuuzulu.
Kujiuzulu Mugabe kumehitimisha karibu miongo minne ya utawala
wake nchini Zimbabwe. Pamoja na hayo japokuwa kujiuzulu kwake
kumewafurahisha Wazimbabwe wengi wakiwemo wanachama na wafuasi wa chama
chake tawala cha ZANU-PF lakini wako pia waliohuzunishwa. Ni kama
alivyosema Terence Mukupe, mbunge na mwanachama wa Zanu-pf ya kwamba:
"wabunge wa chama tawala hawakutaka mwisho wa rais wao uwe kama hivi.
Sisi tunampenda rais, lakini wakati ulikuwa umeshafika wa yeye
kujistaafisha mwenyewe. Waliomzunguka walikuwa wakimshauri vibaya sana.
Tunasikitika sana amefikia ukingoni namna hivi".
Robert Mugabe aliingia madarakani nchini Zimbabwe mwaka 1980 akiwa
anajulikana kama shakhsia mashuhuri zaidi wa mapambano dhidi ya ukoloni
na harakati za kupigania uhuru wa nchi yake. Mugabe alikuwa pia mmoja wa
shakhsia wakubwa wa mapambano dhidi ya ubaguzi wa rangi na mfumo wa
Apathaidi katika nchi jirani na Zimbabwe ya Afrika Kusini.
Robert Mugabe aliongoza mapambano dhidi ya wakoloni hadi nchi yake
ikapata uhuru; na akiwa kiongozi wa mapambano ya ukombozi wa Zimbabwe,
akawa waziri mkuu wa kwanza wa taifa hilo changa wakati huo. Mara baada
ya kushika madaraka, kwa kutumia kaulimbiu ya umoja alianzisha sera ya
kuleta maridhiano nchini. Waziri Mkuu huyo wa Zimbabwe aliamua kukabidhi
nyadhifa na vyeo muhimu kwa raia wazungu. Kutokana na hatua yake hiyo,
katika kipindi cha karibu muongo mmoja Zimbabwe ilipata mafanikio mazuri
kiuchumi, ikapiga hatua kuelekea kwenye ustawi kwa kujenga mashule,
vituo vya afya na tiba pamoja na kuwajengea nyumba raia wazalendo weusi
ambao ndio wanaounda idadi kubwa ya watu wa nchi hiyo.
Pamoja na hayo, kuwakandamiza wapinzani na kutekeleza sera za chama
kimoja zilikuwa miongoni mwa siasa za Mugabe zilizokosolewa sana na
wapinzani. Katika hali kama hiyo, umri mkubwa alionao, uingiliaji wa mke
wake Grace na kampeni zake za kutaka kutwaa madaraka, hali mbaya ya
uchumi na vilevile kufichuliwa ufisadi uliofanywa na baadhi ya jamaa wa
Mugabe na wanachama wa chama chake cha Zanu-pf yote hayo yalishadidisha
upinzani dhidi ya kiongozi huyo.
Hivi sasa baada ya Mugabe kuondoka madarakani, hali ya kisiasa nchini
Zimbabwe imebadilika. Kwa mujibu wa habari mbalimbali Emmerson
Mnangagwa, makamu wa rais ambaye alitimuliwa na Mugabe na ambaye sasa
amechaguliwa kuwa mwenyekiti wa Zanu-pf, ndiye atakayeshika hatamu za
urais wa nchi. Wachambuzi wengi wanaamini kuwa Mnangagwa ataendeleza
siasa za Mugabe, tab'an kwa kutegemea nguvu za jeshi. Pamoja na hayo
watu wengi wana wasiwasi wa kutokea hali ya kukomoana na ulipizaji
visasi wa ndani ya chama na kuvurugika hali ya kisiasa ya Zimbabwe.
Kiasi kwamba kwa kuchelea hali hiyo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa
Antonio Guterres ametoa wito kwa Wazimbabwe wote "kudumisha utulivu na
uvumilivu".
Kurejesha uthabiti wa kisiasa, kujiepusha na sera za kutawala kijeshi
na kidikteta, kustawisha maelewano na nchi za eneo na nje ya eneo,
kuboresha hali ya uchumi na kuitishwa uchaguzi mkuu katika mwaka ujao wa
2018 katika mazingira tulivu na kwa kuheshimu sheria ni miongoni mwa
matarajio muhimu zaidi waliyonayo wananchi; matarajio ambayo kama
hayatotimizwa si hasha yakawafanya Wazimbabwe wengi watamani kurejea
tena kwenye enzi za Mugabe.../
No comments:
Post a Comment