Makamu wa Rais wa Zimbabwe aliyepigwa kalamu
nyekundu hivi karibuni na Rais Robert Mugabe aliyetangaza kujiuzulu hapo
jana amerejea nchini akitokea Afrika Kusini.
Emmerson Mnangagwa alifutwa kazi wiki mbili zilizopita na
kukimbia nchi akihofia usalama wake. Mwanasiasa huyo alipigwa
kalamu kutokana na kile wadadisi wa mambo walikitaja kuwa ni hatua ya
Mugabe mweye umri wa miaka 93 kumsafishia njia mkewe Grace Mugabe,
arithi kiti chake.
Wananchi wa Zimbabwe mjini Harare wamebeba mabango yenye picha za
Mnangagwa zilizoambatana na jumbe zisemazo: Karibu nyumbani shujaa wetu;
Uliahidi utarejea na kweli umerejea, karibu sana. Baadhi ya picha za
mwanasiasa huyo zilikuwa na jina lake la utani la "Mamba".
Jacob Mudenda, Spika wa Bunge la nchi hiyo amesema maandalizi ya
kumuapishwa Mnangagwa Ijumaa ijayo ili kuchukua nafasi ya Mugabe
yanaelekea kukamilika.
Akiongea baada ya kukutana na Rais Jacob Zuma wa Afrika Kusini kabla
ya kuondoka nchini humo mapema leo, Mnangagwa amesema: "Taifa hili
halipaswi tena kushikwa mateka na mtu mmoja, ambaye yuko tayari kufia
ofisini kwa gharama yoyote ile."
Hapo jana Jumanne, Mugabe katika barua yake kwa Spika wa Bunge,
alisema amejiuzulu kwa khiari yake mwenyewe ili kupisha mapokezano ya
uongozi kwa njia ya amani, baada ya kuiongoza nchi hiyo ya kusini mwa
Afrika kwa miaka 37.
Baada ya Spika wa Bunge la Zimbabwe kutoa tangazo la kujiuzulu kwa
Mugabe, wananchi wa taifa hilo walijitokeza mabarabarani kwa shangwe,
nderemo na vifijo kusherehekea habari hizo.
No comments:
Post a Comment