Umoja wa Mataifa umepinga sharti lililotolewa
na muungano vamizi wa nchi za Kiarabu unaofanya mauaji na umwagaji
mkubwa wa damu nchini Yemen ambao umekataa kufungua bandari ya al
Huydadah hadi pale matakwa yao ya kiuadui yatakapokubaliwa.
Kwa kweli hivi sasa hakuna watu wa
nchi yoyote duniani walio na hali ngumu zaidi kushinda Wayemen. Hakuna
mgogoro wowote ulioko duniani ambao hauko pia huko Yemen. Mashambulio ya
kikatili ya Bani Saud ni ya kila siku nchini humo. Hakuna matumaini
yoyote ya maisha nchini Yemen. Mabomu ya Aal Saud yanachukua roho za
Wayemen kila siku huku njaa na magonjwa yakipigana vikumbo katika
kuchukua roho za raia wasio na ulinzi wa nchi hiyo. Hali ni mbaya kiasi
kwamba hata hakuna takwimu za kina za watu wanaokufa na kujeruhiwa kila
leo katika nchi hiyo ya Kiislamu, lakini hata kama tutakubaliana na hizo
hizo takwimu zinazotolewa na Umoja wa Mataifa basi tutaona ni kiasi
gani Saudi Arabia na wenzake wanafanya ukatili wa kutisha katika nchi
hiyo ya Kiarabu. Kwa mujibu wa takwimu hizo, zaidi ya watu elfu nane
wameshauawa na makumi ya maelfu ya wengine wamejeruhiwa. Wahanga wa
ukatili huo ni wa rika tofauti, kuanzia viajuza hadi vitoto vichanga,
wanawake kwa wanaume. Shirika la Kimataifa la Msalaba Mwekundu limesema
kuwa, kwa siku watu elfu saba wanaambukizwa ugonjwa wa kipindupindu na
kila siku mamia ya raia wa nchi hiyo wanapoteza maisha. Njaa ni nduli wa
tatu anayechukua roho za watu huko Yemen pembeni mwa vita na maradhi.
Mazingira ya hivi sasa yanasambaza
harufu ya kifo kila sekunde nchini Yemen. Mgogoro wa nchi hiyo unakuwa
mkubwa sekunde baada ya sekunde kutokana na nchi hiyo maskini kuzingirwa
kila upande na kushambuliwa kila siku kwa kila aina ya silaha hata
zilizopigwa marufuku. Hivi sasa njia zote za kuwafikishia misaada
wananchi wa nchi hiyo zimefungwa. Hadi hivi sasa kumekuwa kukitolewa
tahadhari za kutokea maafa makubwa ya kibinadamu ambayo yatakuwa makubwa
zaidi duniani katika miongo kadhaa iliyopita. Lakini pamoja na hayo, na
kutokana na uungaji mkono wa kila upande wa Marekani, serikali ya
Saudia imekuwa ikipuuza tahadhari zote zinazotolewa. Mark Lukok,
ni Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya misaada ya
kibinadamu. Alisema wiki iliyopita kwamba kama misaada ya binadamu
haitafikishwa kwa wananchi wa Yemen haraka iwezekanavyo, basi ukame
ambao haujawahi kutokea katika miongo kadhaa ya hivi karibuni duniani,
utatokea nchini humo.
Bila ya shaka ni kwa sababu hiyo ndio
maana Umoja wa Mataifa umeitaka Saudi Arabia kufungua haraka bandari ya
al Hudaydah huko Yemen. Hata hivyo utawala wa kidikteta wa Bani Saud
umekataa bali umezidi kung'ang'ania msimamo wake wa kuifunga kabisa
bandari hiyo ambayo ndiyo njia pekee ya kuwafikishia misaada wananchi wa
Yemen. Saudi Arabia inadai kuwa bandari hiyo ilikuwa inatumika kufanya
magendo ya silaha nchini Yemen, lakini imeshindwa kutoa ushahidi wa
kuthibitisha madai hayo. Wachambuzi wa mambo wanasema kuwa, kitendo cha
Saudi Arabia cha kuifunga bandari hiyo ni ushahidi tosha kwamba ukatili
wa wavamizi wa Yemen umeshindwa katika medani za vita na sasa wameamua
kumalizia hasira zao kwa wananchi wa kawaida.
Wachambuzi hao wanasema, hatua hiyo ya
Saudia ni kujaribu kuishinikiza harakati ya Answarullah na waitifaki
wake ili wakubali mapatano, baada ya kushindwa njama zote za maadui hao
za kuidhibiti San'a, mji mkuu wa Yemen. Amma swali linalojitokeza habari
ni kwamba, Umoja wa Mataifa ni mkweli kiasi gani katika mwito wake kwa
Saudia wa kuitaka ifungue bandari ya al Hudaydah huko Yemen? Inabidi
tusubiri na kuona ni kiasi gani umoja huo utaweza kuushinikiza ukoo wa
Aal Saud katika suala hilo ndipo tutakapoweza kujua ukweli wa Umoja wa
Mataifa katika mwito wake huo.
No comments:
Post a Comment