Rais wa Marekani, Donald Trump amewasili China ambapo
atakutana na Rais wa nchi hiyo Xi Jinping, huku ajenda kuu ya mazungumzo
yao ikiangazia zaidi mzozo wa silaha za nyuklia wa Korea Kaskazini na
masuala ya kibiashara.
Donald Trump na Xi Jingping wakiwa na wake zao
Trump amewasili leo kwenye mji mkuu wa China, Beijing akiwa na mkewe
Melania na kupokelewa kwa bendi ya jeshi kabla ya kuelekea Forbidden
City ambako kuna makumbusho ya kasri la kifalme, mji ambao anakutana na
Rais Xi pamoja na mkewe Peng Liyuan.
Saa chache kabla ya kuwasili
mjini Beijing, Trump aliitolea wito China kusaidia katika kukabiliana
na uchokozi unaofanywa na Korea Kaskazini kutokana na mpango wake wa
nyuklia. Ikulu ya Marekani imesema Trump ataitumia ziara hiyo kuiomba
China kusitisha uhusiano wake wa kifedha na Korea Kaskazini na kuheshimu
vikwazo vya Umoja wa Mataifa. China ni mshirika mkubwa wa kibiashara na
Korea Kaskazini.
Akiwa Korea Kusini kiongozi huyo wa Marekani
alizitaka China na Urusi kusaidia kuiwekea shinikizo Korea Kaskazini
kusitisha kutengeneza silaha za nyuklia na kuileta nchi hiyo katika meza
ya mazungumzo. Akizungumza katika Bunge la Korea Kusini mjini Seoul,
Trump ametoa onyo kali kwa kiongozi wa Korea Kaskazini, Kim Jong Un
ambapo amemtaka asiwadharau na wala asiwajaribu.
''Hatuwezi
kuruhusu Marekani au washirika wetu kushambuliwa. Hatuwezi kuruhusu miji
ya Marekani itishiwe na silaha za maangamizi. Hatutoogopa. Na
hatutoruhusu ukatili mwingine ujirudie katika historia, kwenye ardhi hii
ambayo tuliipigania na kufa kwa ajili ya kuilinda,'' alisema Trump.
Trump akilihutubia bunge la Korea Kusini
Rais
Trump amezitaka Urusi na China kusitisha uhusiano wowote na Korea
Kaskazini, ukiwemo ule wa kidiplomasia. Aidha, amesema muda wa kutoa
sababu na visingizio umekwisha na kwamba sasa ni wakati wa kuwa imara,
kwani mtu anayetaka amani lazima asimame imara wakati wote.
Wizara
ya mambo ya nje ya China imesisitiza kwamba nchi hiyo imewahi
kutekeleza kikamilifu maazimio ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa
kuhusu Korea Kaskazini, lakini imesema itachunguza iwapo kuna shughuli
ambazo zinakiuka maazimio hayo. Kwa mujibu wa wizara hiyo, China bado
ina matumaini ya kuutatua mzozo uliopo kwa njia ya mazungumzo.
Kwa
upande wa masuala ya kibiashara, Trump bado yuko katika shinikizo kubwa
kutoka kwa mashirika ya biashara ya Marekani katika kutatua malalamiko
ya kibiashara na China. Marekani imeishutumu China kwa kurudia ahadi
yake ya kufungua masoko yake. Wiki iliyopita Trump alisema kulikuwa na
hasara ya kibiashara ya Dola bilioni 347 kati ya nchi hiyo na China na
kwamba hatua hiyo ni mbaya na inatia aibu.
China ni kituo cha
tatu cha ziara ya siku 12 ya Trump barani Asia ambayo itamfikisha pia
Vietnam na Ufilipino. Tayari kiongozi huyo wa Marekani ameizuru Japan na
Korea Kusini.
No comments:
Post a Comment