Sunday, November 19, 2017

KUSAMBARATISHWA KIKAMILIFU DAESH (ISIS) NCHINI IRSQ

Kusambaratishwa kikamilifu DAESH (ISIS) nchini Iraq
Mabadiliko yanayojiri kwenye medani za vita nchini Iraq yanabainisha kusambaratishwa na kutokomezwa Daesh (ISIS) nchini humo; na kushindwa kikamilifu kundi hilo la kigaidi na kitakfiri ambako ni sawa na kupata mafanikio makubwa Wairaqi katika mapambano dhidi ya magaidi kumeakisiwa sana na duru mbalimbali za habari.
Vikosi vya jeshi la Iraq siku ya Ijumaa viliukomboa mji wa Rawah kutoka kwenye makucha ya magaidi wa Daesh. Kufuatia kukombolewa mji huo kulikochukua muda wa saa kadhaa tu, Waziri wa Mambo ya Ndani wa Iraq Qasim Al-Araji alitangaza kuwa kundi la kigaidi na ukufurishaji la Daesh limesha sambaratishwa kikamilifu nchini humo. Rawah ilikuwa miongoni mwa ngome za mwisho za Daesh ndani ya ardhi ya Iraq. Hivi sasa magaidi wa kundi hilo la ukufurishaji hawana mji mwengine wowote muhimu wa Iraq wanaoushikilia na kuukalia kwa mabavu isipokuwa wanaishia kuzunguka zunguka na kuranda randa kwenye maeneo ya mbali na katika baadhi ya vijiji.
Waziri wa Mambo ya Ndani wa Iraq, Qassim Al-Araji
Mnamo mwaka 2014, kwa uungaji mkono wa kifedha na kijeshi wa Marekani na waitifaki wake wa Magharibi na wa Kiarabu ikiwemo Saudi Arabia, kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh liliishambulia Iraq, likayavamia na kuyakalia kwa mabavu baadhi ya maeneo ya kaskazini na magharibi mwa nchi hiyo. Lakini tangu wakati huo hadi sasa, jeshi la Iraq lilkisaidiwa na vikosi vya kujitolea vya wananchi limeweza kuyakomboa maeneo hayo kutoka kwenye makucha ya kundi hilo; na kimsingi kundi hilo limeshasambaratishwa kikamilifu nchini humo.
Wapiganaji wa jeshi la kujitolea la wananchi la Al Hashdu-Sha'abi
Hata hivyo baada ya kushindwa kijeshi kundi la kigaidi na ukufurishaji la Daesh, suali la kujiuliza hivi sasa ni je, kwa ushindi huo, Wairaqi sasa wataweza kupumua na kupata salama ya kuepukana na shari ya ugaidi? Au kundi hilo la kigaidi na kitakfiri litaanzisha mbinu nyengine mpya na kuendelea kuwaandamana wananchi wa Iraq kwa hujuma na jinai zake za kinyama? Kwa kuzingatia kuwa mashambulio ya kigaidi yalishadidi hivi karibuni katika nchi za Iraq na Syria, tunaweza kusema kuwa baada ya kushindwa kijeshi na kupoteza maeneo waliyokuwa wakiyashikilia kwa mabavu, magaidi wa kundi la kitakfiri la Daesh wameshaainisha mkakati wanaokusudia kuutekeleza mnamo siku zijazo. Ili kufifisha kushindwa kwake kijeshi, kundi la Daesh (ISIS) limeanzisha mbinu na mkakati wa kuvuruga usalama, kwa kushadidisha mashambulio ya kujitoa mhanga ya miripuko ya mabomu pamoja na mauaji ili kuvuruga amani na uthabiti nchini Iraq, sambamba na kupanua wigo wa harakati zake katika nchi nyengine ikiwemo Afghanistan, Libya na kwengineko. Harakati za aina hiyo ni muendelezo wa njia na misimamo ya kufurutu mpaka iliyoanzishwa mwaka 2004 na Abu Mus'ab Az-Zarqawi kwa njia ya kuanzisha mauaji na kuwalenga raia; na baada ya kushadidi hitilafu baina ya Wairaqi ikaandaa mazingira ya kuzaliwa Daesh kutoka kwenye tumbo la Al-Qaeda na kupelekea hatimaye mwaka 2014 kushambuliwa na kukaliwa kwa mabavu kirahisi miji mbalimbali ya ardhi ya Iraq.
Magaidi wa kundi la ukufurishaji la Daesh
Leo hii baada ya miaka mitatu ya vita na mapigano makali ya kujitolea mhanga, yaliyowagharimu roho nyingi za watu na kuwasababishia pia uharibifu mkubwa, Wairaqi wameweza kuyakomboa maeneo yote ya ardhi yao yaliyokuwa yamevamiwa na kushikiliwa kwa mabavu na Daesh; hata hivyo ushindi huo wa kijeshi dhidi ya magaidi wenye misimamo ya kufurutu mpaka sio mwisho wa mapambano, bali inapasa ifanyike kazi ya kuing'oa na kuitokomeza mizizi ya misimamo hiyo hatari. Katika hali kama hiyo, inavyoonekana, baada ya kulisambaratisha kijeshi kikamilifu kundi la Daesh nchini Iraq, vita na mapambano yajayo yatakuwa ni ya kitaarifa na kiintelijinsia ambayo hayatotegemea askari na vifaru pekee; bali yatategemea zaidi unasaji wa taarifa za kiintelijinsia. Katika mazingira ya sasa ambapo magaidi wa kundi la kitakfiri la Daesh wamesha sambaratishwa kikamilifu nchini Iraq, Marekani, ambayo inahisi njama na mipango yake iliyokuwa imepanga dhidi ya Iraq na eneo kwa jumla imevurugika, hivi sasa inashughulika kupanga njama na mikakati mingine mipya ya kiadui. 
Mji wa Rawah uliokuwa ngome ya mwisho muhimu ya Daesh nchini Iraq
Ukweli ni kwamba kundi la kigaidi na ukufurishaji la Daesh limeshafutwa kwenye ramani ya Iraq, na hilo limewezekana kwa baraka na nafasi ya uongozi wa juu wa kidini na kwa kujitolea mhanga vikosi vya Iraq hususan vya jeshi la kujitolea la wananchi la Al Hashdu-Sha'abi. Na hii ni katika hali ambayo jeshi hilo la wananchi lingali linaendelea kuandamwa na njama na tuhuma za Marekani. Kutokana na matukio yaliyojiri huko Iraq wananchi wanapaswa kuwa macho zaidi katika kipindi kinachoanza hivi sasa cha baada ya kusambaratishwa Daesh nchini humo.../

No comments:

Post a Comment