Friday, November 17, 2017

UMASIKINI UNACHOCHEA MIMBA ZA UTOTONI TANZANIA

Utafiti: Umasikini unachochea mimba za utotoni Tanzania
Imeelezwa kuwa, umasikini na kipato cha chini cha baadhi ya familia nchini Tanzania ndicho chanzo cha mimba za utotoni katika jamii ya nchi hiyo ya Afrika Mashariki.
Hayo yameelezwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Jukwaa la Utu wa Mtoto (CDF), Koshuma Mtengeti katika warsha ya siku moja ya kutambulisha mradi na shirika hilo kwa wadau iliyofanyika mkoani Dodoma. Kwa mujibu wa shirika hilo, utafiti uliofanywa na shirika hilo kwa kusaidiana na mashirika mengine, umebaini kwamba, umasikini wa familia husababisha familia zenye maisha magumu kupambana kwa bidii kutafuta chakula na mavazi ya watoto wao.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Jukwaa la Utu wa Mtoto ameeleza kuwa, utafiti wa Demografia ya Afya Tanzania wa 2016 (TDHS) unaonesha kwamba, asilimia 36 ya wasichana wa umri wa kati ya miaka 20-24 waliolewa kabla ya kufikia miaka 18. 
Maandamano ya kupinga ndoa za utotoni nchini Nigeria
Hayo yanajiri katika hali ambayo, kumekuweko na kampeni ya kimataifa ya kukabiliana na ndoa za utotoni hasa barani Afrika.
Mwezi uliopita nchi ya Senegal ilikuwa mwenyeji wa mkutano uliokuwa na lengo la kuongeza hatua za kutokomeza ndoa za utotoni katika nchi za Afrika Magharibi na Kati. Inaelezwa kuwa, wazazi ambao hali zao ni duni kimaisha, mara nyingi huwaozesha watoto wao mapema ili kupunguza mzigo wa ulezi, wakati huo huo, baadhi ya mila na desturi zinatajwa kuwa nazo zina mchango katika hilo.

No comments:

Post a Comment