Wednesday, November 8, 2017

KENYA YAPINGA HATUA YA TANZANIA KUPIGA MNADA ZAIDI YA NG' OMBE 1,300

Kenya yapinga hatua ya Tanzania kupiga mnada zaidi ya Ng’ombe 1,300
Waziri wa Mambo ya Nje wa Kenya, Amina Mohamed ameilalamikia serikali ya Tanzania kufuatia hatua ya taifa hilo kuwapiga mnada zaidi ya ng’ombe 1,300 walioingia nchini humo kinyume na sheria.
Serikali ya Rais John Magufuli ilichukua hatua hiyo baada ya wafugaji kuingia nchini humo na mifugo yao wakitafuta lishe.
Hatua hiyo imekuja siku moja tu baada ya Rais Magufuli kusema kuwa taifa hilo sio shamba la mifugo wa taifa jirani.
Akizungumza katika mkoa wa Kagera ambako alikuwa katika ziara yake ya kikazi Magufuli alisema kwamba Tanzania sio shamba la kuchungia mifugo ya nchi jirani na kwamba ataichukulia mifugo hiyo hatua kali za kisheria. 
Rais wa Tanzania John Magufuli
Vilevile alizitaka nchi Jirani kuchukua hatua kama hiyo iwapo mifugo ya Tanzania wataingia katika mataifa hayo kinyume na sheria.
Hatua ya kuwapiga mnada ng’ombe hao imezua hisia kali miongoni mwa wafugaji wa Kenya baada ya wenzao waliokuwa na mifugo hao kukamatwa na kuzuiliwa kwa kuingia nchini humo kinyume na sheria.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Kenya, Amina Mohammed amenukuliwa akisema: ”Tulidhani kwamba mazungumzo ya kidiplomasia yangetatua mzozo huu, lakini tumeshindwa kufikia makubaliano.
Amesema: ”Historia ambayo tumekuwa nayo na Watanzania ni nzuri sana na kila kunapotokea tatizo tumekuwa tukitatua. Ni kwa sababu hiyo ambapo imekuwa hatua ya kushangaza miongoni mwa wafugaji wa Kenya”,
Bi Mohamed amesema kuwa Kenya imekuwa ikiwavumilia wafugaji wa nchi jirani ambao wamekuwa wakivuka mara kwa mara na kuingia katika eneo la Kajiado nchini Kenya.

No comments:

Post a Comment