Wabunge nchini Iran wamelaani vikali mauaji
yanayotekelezwa na Saudi Arabia dhidi ya raia wa Yemen huku wakisema
jinai hizo zimenyamaziwa kimya na vyombo vya habari vya magharibi.
Katika taarifa siku ya Jumatano, wabunge 191 wa Majlisi ya
Ushauri ya Kiislamu ya Iran wamesema katika zama hizi ambazo, madola ya
Magharibi, hasa Marekani, hudai kuwa watetezi wa haki za binadamu,
tunashuhudia jinai za kuogofya zikitekelezwa na Saudi Arabia dhidi ya
watu wanaodhulumiwa na wasio na ulinzi wa Yemen.
Wabunge wa Iran wametahadharisha kuwa Yemen inakabiliwa na maafa ya
kibinadamu ambayo yamesababishwa na hujuma ya Saudia dhidi ya nchi hiyo
sambamba na mzingiro wa anga, nchi kavu na bahari na hivyo kupelekea
misaada ya dharura kama dawa na chakuka kutowafikia Wayemen. Wabunge wa
Iran wamesema Saudi Arabia na waitifaki wake, hasa Marekani, wanabeba
dhima ya jinai dhidi ya watu wa Yemen.
Taarifa hiyo imeongeza kuwa: "Swali kubwa hapa ni kuwa, je, ni vipi
Saudi Arabia inawaua watu wasio na hatia kila siku kwa kutumia silaha
mbali mbali hatari huku wanaodai kutetea haki za binadamu wakiwa kimya,
bali hata wakiunga mkono jinai hizo?"
Wiki iliyopita Msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa alieleza
wasiwasi wake kuhusu hatua ya Saudi Arabia na washirika wake ya kufunga
kabisa mipaka ya Yemen kwa siku ya tano mfululizo na kusisitiza kuwa
Yemen inakabiliwa na baa kubwa zaidi la njaa kuwahi kushuhudiwa duniani
katika miongo ya hivi karibuni.
Saudi Arabia ikishirikiana na Marekani, Israel na nchi nyingine
kadhaa za Kiarabu ilianzisha mashambulizi ya pande zote dhidi ya Yemen
Machi mwaka 2015. Maelfu ya raia wasio na hatia wameuawa na mamilioni ya
wengine kuwa wakimbizi kutokana na mashambulizi hayo.
No comments:
Post a Comment