Umoja wa Mataifa umewataka wananchi wa
Zimbabwe kudumisha amani na utulivu katika kipindi hiki baada ya Rais
Robert Mugabe kutangaza kujiuzulu hapo jana.
Antonio Guterres, Katibu Mkuu wa
Umoja wa Mataifa amewataka wananchi wa nchi hiyo kudumisha amani na
utulivu katika kipindi hiki inachopitia nchi yao baada ya kiongozi wa
nchi hiyo kujiuzulu.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa
amezitaka tawala zote kuheshimu matakwa ya wananchi. Rais Robert Mugabe
wa Zimbabwe hatimaye jana alisalimu amri na kukubali kujiuzulu kufuatia
mashinikizo ya kila upande ya kumtaka aachie madaraka.
Jacob Mubenda, Spika wa Bunge la
Zimbabwe alitangaza jana kwamba, amepokea barua ya kujiuzulu kutoka kwa
kiongozi huyo mkongwe mwenye umri wa miaka 93.
Katika barua hiyo ya kujiuzulu, Mugabe alisema anajiuzulu kwa hiari,
ili kupisha mapokezano ya uongozi kwa njia ya amani, baada ya kuiongoza
nchi hiyo ya kusini mwa Afrika kwa karibu miongo minne.
Baada ya Spika wa Bunge la Zimbabwe
kutoa tangazo la kujiuzulu kwa Mugabe, wananchi wa taifa hilo
walijitokeza mabarabarani kwa shangwe, nderemo na vifijo kusherehekea
habari hiyo.
Jeshi la Zimbabwe Jumatano lilitangaza
Jumatano iliyopita kwamba, Mugabe na familia yake wapo katika kifungo
cha nyumbani na kisha kumuondoa uongozini. Jeshi la Zimbabwe lilichukua
hatua hiyo kama radiamali kwa hatua ya siku kadhaa zilizopita
iliyochukuliwa na Mugabe ya kumuuzulu aliyekuwa Makamu wake Emmerson
Mnangagwa ili aweze kumrithisha nafasi hiyo mkewe Bi Grace Mugabe.
No comments:
Post a Comment