Kutokana na kushadidi mashambulizi ya kigaidi
katika ardhi ya Somalia, ndege za kivita za Marekani kwa mara ya kwanza
zimefanya mashambulizi dhidi ya ngome za makundi ya kigaidi katika nchi
hiyo ya mashariki mwa Afrika.
Kundi la kigaidi la al Shabab
ambalo limetangaza utiifu wake kwa viongozi wa kundi la al Qaida
limekuwa likipigana na serikali ya Somalia kwa miaka kadhaa sasa. Kundi
hilo liliteka miji kadhaa ya Somalia ikiwemo sehemu kubwa ya mji mkuu
Mogadishu lakini Agosti mwaka 2011 lilifurushwa katika miji na maeneo
mengi ya nchi hiyo kutokana na mashambulizi makubwa ya jeshi la Somalia
likishirikiana na askari wa kulinda amani wa Umoja wa Afrika. Hata hivyo
kundi hilo la kigaidi bado linadhibiti miji kadhaa hususan maeneo ya
vijijini ya Somalia.
Katika miezi ya hivi karibuni kundi hilo limebadili mbinu zake kwa
kuzidisha mashambulizi ya kuvizia na kujilipua kwa mabomu badala ya
kukabiliana moja kwa moja na vikosi vya jeshi la serikali ya Somalia na
askari wa kulinda amani wa Umoja wa Afrika. Mfano wa wazi wa ukweli huo
ni shambulizi la wiki mbili zilizopita mjini Mogadishu ambalo limeua
karibu watu mia nne.
Kwa sasa Marekani, kama kawaida yake,
imeparamia wimbi la kupambana na ugaidi na kundi la al Shabab na kuanza
kuingilia moja kwa moja masuala ya ndani ya Somalia kwa kushambulia
baadhi ya maeneo ya kundi hilo. Tunapotupia jicho sera na siasa za
Marekani barani Afrika tunaona kuwa, japokuwa askari wa Marekani
wamekuwepo kwa miaka mingi katika nchi mbalimbali za Afrika lakini nchi
hiyo ilianzisha rasmi kambi na eneo lake la sita la kijeshi duniani
mwaka 2007 kwa kuanzisha ofisi ya Komandi ya Jeshi ya Marekani Barani
Afrika AFCOM kwa kifupi. Katika kipindi cha miaka kadhaa ya hivi
karibuni Marekani imekuwa ikichunga na kufuatilia harakati zote za
kijeshi barani Afrika na kufuatilia maslahi yake haramu katika nchi za
bara hilo kwa kutumia njia na mbinu mbalimbali kama kutuma washauri wa
masuala ya kijeshi na eti kutoa mafunzo kwa majeshi ya nchi za Kiafrika.
Miongoni mwa malengo hayo yanayohudumia maslahi ya Marekani ni
kufuatilia harakati za nchi wapinzani kama China na Russia huko Afrika,
kufuatilia maslahi ya kiuchumi na kibiashara na kutumia maeneo ya
kistratijia ya nchi za bara hilo kwa malengo ya kikoloni.
Mchambuzi Nick Turse anasema: Kwa
sasa Marekani ina vikosi vya jeshi katika nchi kadhaa za Afrika ambazo
hazina tatizo lolote la makundi ya kigaidi kama lile la Daesh. Kwa
msingi huo hatuwezi kusema kuwa operesheni zinazofanywa na wanajeshi hao
wa Marekani ni sehemu ya mapambano dhidi ya ugaidi kama wanavyodai
viongozi wa serikiali ya Washington".
Pamoja
na hayo Marekani imezidisha kasi ya kutuma majeshi yake barani Afrika
kwa kisingizio cha kupambana na ugaidi kama inavyoshuhudiwa katika nchi
kama Niger. Operesheni hizo zinaipa Marekani fursa ya kutimiza malengo
yake ya kisiasa, kiuchumi na kijeshi.
Seneta
Lindsay Graham wa Kamati ya Jeshi la Marekani anasema: Maana na hakika
ya vita imo katika hali ya kubadilika na sasa tunashuhudia hatua zaidi
barani Afrika.
Alaa
kulli hal, ripoti mbalimbali zinaonesha kuwa, Washington ni miongoni
mwa pande zilizoshiriki kuunda na kuanzisha makundi hatari ya kigaidi
kama Daesh, Al Qaida na Twaliban. Hivyo basi mashambulizi ya sasa dhidi
ya wapiganaji wa al Shabab ni ya kimaonyesho tu yanayofanyika kuwahadaa
walimwengu au kwa shabaha ya kutimiza malengo ya kikoloni ya nyuma ya
pazia.
No comments:
Post a Comment