Ofisi ya masuala ya haki za binadamu ya Umoja
wa Mataifa imeikosoa vikali serikali ya Burundi kwa kuwatishia
wataalamu wa uchunguzi wa umoja huo.
Rupert Colville, msemaji wa Zeid Ra'ad al-Hussein, Kamishna
Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa ameiandikia barua serikali
ya Bujumbura akiitaka iwaonye maafisa wake dhidi ya kutishia maisha ya
wajumbe wa Kamisheni ya Uchunguzi ya UN, waliotoa mwito wa kubebeshwa
dhima maafisa wa ngazi za juu wa Burundi wanaotuhumiwa kufanya jinai
dhidi ya binadamu.
Katika barua hiyo, Colville amesema Burundi kama nchi mwanachama wa
Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa inapaswa kushirikiana na
kuheshimu maamuzi ya chombo hicho.
Hivi karibuni, Burundi ilitangaza kuwa haitashirikiana na Mahakama ya
Kimataifa ya Jinai (ICC) katika uchunguzi wa jinai za kivita na ukatili
uliofanyika nchini humo katika kipindi cha miaka miwili iliyopita.
Novemba 9 mwaka huu, majaji wa mahakama hiyo waliruhusu kuanzishwa
uchunguzi kuhusu ukatili na jinai dhidi ya binadamu uliofanywa katika
kipindi cha kati ya mwaka 2015 na 2017 dhidi ya raia wa Burundi ndani au
nje ya nchi hiyo. Jinai hizo ni pamoja na mauaji, ubakaji, ukatili na
mateso yaliyoanza mwaka 2015 baada ya Rais wa Burundi, Pierre Nkurunziza
kutangaza nia yake ya kugombea kiti hicho kwa muhula wa tatu
mfululizo.
Ni vyema kuashiria hapa kuwa, Oktoba 26, Burundi ilijiondoa rasmi kwenye Mkataba wa Roma uliounda ICC.
No comments:
Post a Comment