Mivutano ya kisiasa inaonekana kupamba moto
zaidi leo nchini Kenya huku vyombo vya usalama vikilinda maeneo muhimu
ya jiji la Nairobi kabla ya kuapishwa Rais Uhuru Kenyatta hii leo kwa
ajili ya kipindi cha awamu ya pili.
Kenyatta
ambaye alishinda uchaguzi wa marudio wa tarehe 26 Oktoba uliosusiwa na
kambi ya upinzani, anaapishwa leo huku chama kikuu cha upinzani cha NASA
kikiwataka wafuasi wake kususia sherehe hiyo na badala yake
wakusanyike katika uwanja wa Jacaranda katika eneo la Embakasi mjini
Nairobi kwa kile kinachosemekana ni kuomboleza mauaji ya wafuasi wa
kinara wa kambi ya upinzani, Raila Odinga, waliouawa na maafisa wa
polisi katika ghasia za uchaguzi wa rais.
Watu
zaidi ya 70 waliuawa katika vurugu za kisiasa msimu huu wa uchaguzi,
wengi wao wakiwa wameuawa kwa kupigwa risasi na polisi.
Jumamosi iliyopita kamanda wa polisi mjini Nairobi, Japhet Koome
alisema kuwa muungano wa upinzani wa NASA haujaitaarifu polisi kuhusu
mkutano huo.
Koome alisisitiza kuwa jeshi la polisi litakabiliana na mtu yeyote atakayefanya mkutano bila ya kuliarifu jeshi hilo.
Rais Uhuru Kenyatta amewataka Wakenya kuungana na kufanya kazi pamoja baada ya ushindani wa kisiasa ili kulijenga taifa hilo.
Viongozi wa nchi kadhaa za kigeni wamealikwa katika sherehe ya kuapishwa Rais Uhuru Kenyatta.
No comments:
Post a Comment