Wananchi katika mji mkuu wa Jamhuri ya Afrika
ya Kati, Bangui wamebainisha ghadhabu zao baada ya mwanafunzi wa shule
kupoteza maisha katika ajali iliyohusisha gari la askari wa Mpango wa
Umoja wa Mataifa nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati MINUSCA.
Saa chache baada ya ajali hiyo, gari la Umoja wa Mataifa
lililokuwa likipita Bangui lilishambuliwa na watu wenye hasira na
kuchomwa moto hali iliyohatarisha maisha ya abiria waliokuwemo ambao
walinusurika kuuawa.
Pia gari la zimamoto lililotumwa na MINUSCA lilishambuliwa na umati
wa watu na kuharibiwa ambapo askari mmoja wa zimamoto alijeruhiwa.
Matukio haya mawili kwa mujibu wa MINUSCA yalifuatiwa na mashambulizi
mengine kadhaa dhidi ya magari ya mpango huo katika mji mzima wa Bangui.
MINUSCA inashirikiana na serikali, jeshi la polisi la nchi hiyo na
wadau wengine kuhakikisha utulivu unarejea katika mji huo mkuu wa
Jamhuri ya Afrika ya Kati.
MINUSCA imekaribisha taarifa ya serikali ya CAR baada ya tukio la
ajali ya bahati mbaya iliyokatisha maisha ya kijana mwanafunzi mjini
Bangui.
MINUSCA imesikitishwa na kifo hicho na kuungana na serikali kutoa
wito wa kudumisha utulivu miongoni mwa wananchi baada ya tukio hilo
kuzusha maandamano ya ghasia mjini Bangui dhidi ya Umoja wa Mataifa.
Katika tukio hilo waziri wa habari na msemaji wa serikali ya CAR
akaeleza kwamba MINUSCA ingependa kuwafahamisha kuwa gari lililomgonga
na kumuua mwanafunzi huyo ni mali yake lakini lilikuwa likiendeshwa na
mwanajeshi wa jeshi la Jamhuri ya Afrika ya Kati (FACA).
Hayo yanajiri katika hali ambayo ukosoaji dhidi ya wanajeshi hao wa
MINUSCA wapatao elfu 13 umeendelea kuongezeka kutokana na wananchi
kutoridhishwa na utendaji wa vikosi hivyo katika kuwalinda raia wa
Jamhuri ya Afrika ya Kati. Askari hao wanalaumiwa kwa kutozuia mauaji ya
Waislamu nchini humo.
Machafuko huko Jamhuri ya Afrika ya Kati (CAR) yalizuka mwaka 2013,
baada ya waasi wa Seleka kumuondoa madarakani aliyekuwa rais wa nchi
hiyo, François Bozizé. Baada ya rais Mwislamu, Michel Djotodia kuchukua
mamlaka, waasi na magaidi wa Kikristo wenye misimamo ya kufurutu ada wa
Anti-Balaka walianzisha mauaji ya kimbari dhidi ya jamii ya Waislamu,
ambapo maelfu ya Waislamu waliuawa na wengine wengi kuwa wakimbizi.
No comments:
Post a Comment