Wednesday, November 15, 2017

NYUMA YA PAZIA LA MASHINIKIZO YA KUIONDOA IRAN NCHINI SYRIA

Nyuma ya pazia la mashinikizo ya kuiondoa Iran nchini Syria
Pamoja na kwamba Iran ni nchi iliyoko mstari wa mbele katika vita dhidi ya magaidi wakufurishaji nchini Syria, lakini waungaji mkono wa nyuma ya pazia wa magaidi wa Daesh (ISIS) hivi sasa wanafanya njama za kuhakikisha wanaandaa mazingira ya kurejea magaidi nchini humo kupitia kukabiliana waziwazi na kambi ya muqawama.
Siku chache zilizopita, Rex Tillerson, waziri wa mambo ya nje wa Marekani alisema: "Askari wa Iran, iwe ni wanajeshi wa Sepah au vikosi vinavyounga mkono na Iran, lazima viondoke katika ardhi ya Syria na kurejea makwao."
Akijibu madai hayo juzi Jumanne, Sergey Lavrov, waziri wa mambo ya nje wa Russia alisema kuwa, Iran iko kihalali nchini Syria na ni kwa ombi rasmi la serikali yenyewe ya nchi hiyo. Vile vile amekanusha uvumi wote ulioenezwa kwamba eti Moscow imeahidi kuwaondoa askari wa Iran nchini Syria.
Brigedia Jenerali Hossein Hamedani wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu aliyeuawa shahidi nchini Syria wakati akijitolea kutoa ushauri wa kijeshi wa kupambana na magenge ya kigaidi

Iran, Russia na Uturuki zimefanikiwa kupiga hatua kubwa katika utatuzi wa mgogoro wa Syria kupitia mazungumzo ya Astana na yumkini kama si mazungumzo hayo, leo hii magaidi wa Daesh (ISIS) wasingelikuwa wamedhoofishwa kiasi chote hiki.
Katika kukabiliana na mafanikio ya mazunungumzo hayo ambayo yamefanyika bila ya kushirikishwa upande wa Magharibi na Kiarabu ambao ni wa waungaji mkono wakuu wa magaidi huko Syria, upande huo umeamua kuishinikiza kambi halisi inayopambana na magaidi yaani Hizbullah ya Lebanon na Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu SEPAH kama njia ya kuidhoofidha kambi ya muqawama na kuwarejesha magaidi katika eneo hili.
Matamshi ya kutaka walinzi wa Haram waondoke nchini Syria yametolewa katika hali ambayo, hadi hivi sasa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imekuwa ikisema mara kwa mara kwamba kuweko washauri wake wa kijeshi nchini Syria kumefanyika kwa lengo la kuwasaidia wananchi wa nchi hiyo kupambana na magaidi tena kwa ombi rasmi la serikali ya Damascus.
Lau kama Tehran ingelituma wanajeshi huko Syria kwa ombi la Russia au Marekani ni wazi kwamba suala la kuondoa askari hao lingelihitajia idhini ya moja kati ya nchi hizo. Lakini wakati nchi huru kama Iran ambayo si tegemezi kwa nchi nyingine yoyote inapoitikia ombi la serikali halali ya nchi fulani la kuwasaidia wananchi wa nchi hiyo tena katika eneo hili, wakati huo hakuna nchi yoyote nyingine yenye haki ya kuitaka Tehran iondoke nchini humo.
Sergey Lavrov, waziri wa mambo ya nje wa Russia

Wale watu ambao hivi sasa wanapiga domo la kuitaka Iran iondoke Syria kwa madai kuwa magaidi wa Daesh wameshamalizwa nchini humo, wao ndio wanaopaswa kujibu ni kwa nini wana kambi zao za kijeshi katika eneo hili na kwa nini hawaondoi wanajeshi wao waliowamiminika katika kona mbalimbali za ukanda huu? Kwa mfano Washington inajigamba kuwa imelimaliza kundi la Taliban nchini Afghanistan baada ya kuwafurusha mjini Kabul na kwengineko, sasa kwa nini Marekani haiondoi kambi zake za kijeshi nchini humo bali kila leo inaongeza wanajeshi wake? Si hayo tu, lakini pia madola ya kibeberu kama Marekani yanapaswa kujibu ni kwa idhini ya nani yana wanajeshi na yanafanya mashambulizi ndani ya ardhi ya nchi huru ya Syria?
Ni jambo lililo wazi kwamba mashinikizo ya baada ya tawala za eneo hilo na mabwana zao wa nje ya ukanda huu, ya kuitaka Iran iondoke nchini Syria yanatokana na woga wao wa kuongezeka ushawishi wa Tehran katika fikra za walio wengi katika ulimwengu wa Kiislamu. Ushawishi huo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ndio uliopelekea kuundika vikosi vya kujitolea vya wananchi katika nchi za Iraq, Syria na Yemen na ni jambo lililo bayana kwamba maadamu vikosi hivyo vya kujitolea vingalipo, Magharibi na vibaraka wao wenye fikra mgando hawataweza kuhatarisha usalama na utulivu wa eneo hili.

No comments:

Post a Comment