Ujumbe wa Umoja wa Afrika nchini Somalia
(AMISOM) umetangaza kuwa utaondoa askari 1,000 kutoka Somalia hadi
kufikia mwishoni mwa mwaka huu.
Mwakilishi wa Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika nchini
Somalia, Francisco Madeira amesema kuwa AMISOM imeanza kupunguza idadi
ya askari wake nchini humo na kwamba kufikia tarehe 31 Disemba askari
1000 wa kikosi hicho watakuwa wameondoka katika ardhi ya Somalia.
Madeira amesisitiza umuhimu wa kuwepo umoja kati ya raia na jeshi
nchini Somalia dhidi ya ugaidi na kusema jeshi peke yake haliwezi
kuwashinda magaidi bila ya msaada ya raia. Amewataka Wasomalia wote
kushirikiana kwa ajili ya kuwafukuzia mbali wapiganaji wa kundi la
kigaidi la al Shabab.
Kikosi cha majeshi ya Umoja wa Afrika cha AMISOM ambacho kiliundwa
kupitia azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kimekuwa
kikiisaidia serikali ya Somalia kupambana na magaidi wa kundi la al
Shabab tangu mwaka 2007.
Kikosi hicho kinaundwa na askari elfu 22 kutoka nchi za Uganda, Kenya, Djibouti, Burundi na Ethiopita.
Magaidi wa al Shabab wamezidisha mashambulizi ya kujilipua kwa mabomu
katika wiki za hivi karibuni husuan katika mji mkuu wa Somalia,
Mogadishu.
No comments:
Post a Comment