Kamanda wa Boko Haram atiwa mbaroni, wenzake 4 wauawa, mateka 212 wakombolewa
Jeshi la Nigeria limetangaza kuwa,
limewakomboa raia wengine 212 waliokuwa wakishikiliwa mateka na
wanachama wa kundi la kigaidi la Boko Haram katika msitu wa Sambisa.
Msemaji wa jeshi la Nigeria, Sani
Usman amesema kuwa, jeshi la nchi hiyo limefanikiwa pia kumtia mbaroni
mmoja wa makamanda wa Boko Haram, Amman Judee na kuwaua wapiganaji wanne
wa kundi hilo la kigaidi.
Amesema kuwa, kamanda huyo wa Boko Haram
aliyetiwa mbaroni anaendelea kusailiwa. Kwa mujibu wa jeshi la Nigeria,
watu 212 waliokombolewa kutoka mikononi mwa wapiganaji wa Boko Haram ni
kundi la pili kukombolewa na jeshi la nchi hiyo katika kipindi cha
chini ya wiki moja.
Siku ya Jumamosi jeshi la Nigeria
liliwakomboa raia wengine 30 waliokuwa wakishikiliwa na wanamgambo wa
Boko Haram ambapo lilifanikiwa pia kuwauwa wanachama 11 wa kundi hilo la
kigaidi katika kijiji cha Bama huko Borno kaskazini mashariki mwa
Nigeria.
Baadhi ya duru zinaripoti kwamba, jeshi
la Nigeria limepata mafanikio makubwa katika siku za hivi karibuni
katika vita na operesheni zake dhidi ya wanamgambo wa Boko Haram.
Mashambulizi ya genge la kigaidi la Boko
Haram yalianza mwaka 2009 kaskazini na kaskazini mashariki mwa Nigeria
na hadi hivi sasa zaidi ya watu 20 elfu wameshauwa kutokana na machafuko
yaliyosababishwa na kundi hilo.
Kundi la Boko Haram limekuwa likifanya
jinai za kila namna ikiwa ni pamoja na kuteka nyara watu pamoja na
wasichana na kuwapiga mnada kama bidhaa.
No comments:
Post a Comment