Duru mpya ya mazungumzo ya amani ya Burundi
inaanza leo Jumatatu huko Arusha, kaskazini mwa Tanzania, na itaendelea
hadi Disemba 8.
Mazungumzo hayo yanaongozwa na Benjamin William Mkapa, Rais
mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye ni mpatanishi wa
Jumuiya ya Afrika Mashariki katika mgogoro wa kisiasa wa Burundi.
Muungano wa upinzani wa CNARED umesema hautashiriki katika mazungumzo
hayo ukisisitiza kuwa, mpatanishi wa mgogoro huo Benjamin Mkapa amekuwa
akiegemea upande wa serikali.
Wawakilishi wa serikali ya Burundi walikataa kushiriki mazungumzo ya
moja kwa moja na wawakilishi wa CNARED katika mazungumzo yaliyopita,
wakiwatuhumu kuhusika na jaribio lililofeli la mapinduzi dhidi ya
serikali ya Rais Pierre Nkurunziza mnamo Mei 14, 2015.
Burundi ilitumbukia katika machafuko mwishoni mwa mwezi Aprili mwaka
2015 baada ya chama tawala cha CNDD-FDD kumuidhinisha Nkurunziza
kugombea urais katika uchaguzi mkuu uliopita kwa mara ya tatu mfululizo.
Wapinzani waliitaja hatua ya Rais Nkurunziza kushiriki katika
uchaguzi huo kwamba ilikiuka katiba na hati ya makubaliano ya amani ya
Arusha lakini serikali ya Bujumbura ilisema haijakiuka sheria.
Kwa mujibu wa mashirika mbali mbali ya haki za binadamu, watu zaidi
ya elfu 2 wameuawa katika machafuko hayo, kiasi cha majaji wa Mahakama
ya Kimataifa ya Jinai ICC kuruhusu kuanzishwa uchunguzi kuhusu ukatili
na jinai dhidi ya binadamu uliofanywa katika kipindi cha kati ya mwaka
2015 na 2017. Ifahamike kuwa, Burundi ilijiondoa kwenye Mkataba wa Roma
uliounda mahakama hiyo ya mjini The Hague, Uholanzi.
No comments:
Post a Comment