Katika muendelezo wa wimbi jipya la
kamatakamata ambalo halijawahi kushuhudiwa nchini Saudia kwa madai ya
kufanyika mageuzi na kupambana na ufisadi viongozi wa ngazi ya juu wa
kijeshi wametiwa nguvuni nchini humo.
Hayo ni kwa mujibu wa baadhi ya
magazeti mashuhuri ya Uingereza ambayo yametangaza kwamba, katika hali
ambayo Mohammad Bin Salman Al Saud anadai kufanya marekebisho nchini
Saudia, uhalisia wa mambo ni kwamba mrithi huyo wa kiti cha ufalme
anapambana na wapinzani wake tu.
Chanzo kimoja ndani ya ukoo wa kifalme
wa Aal-Saud ambacho hakikutaka kutaja jina lake kimefichua kwamba, hadi
sasa viongozi 14 wa ngazi ya juu wa gadi ya taifa na Wizara ya Ulinzi ya
Saudia ambao wamestaafu, wametiwa nguvuni kwa tuhuma za kushiriki
katika kutia saini mikataba ya kifedha inayotia shaka. Kukamatwa
viongozi hao wa kijeshi kumeifanya idadi ya watu waliokamatwa katika
wiki za hivi karibuni ndani ya taifa hilo, kupindukia 200 ambapo kati
yao ni mawaziri wanne na wanamfalme 11 akiwemo Mrithi wa Kiti cha Ufalme
wa zamani wa nchi hiyo.
Baadhi ya maafisa wa jeshi wamefichua
kwamba kutiwa mbaroni kwa makamanda hao wa kijeshi kumetokana na
kushindwa kwao katika vita dhidi ya Yemen. Gazeti la Wall Street Journal
limeandika kwamba, Mohammad Bin Salman Al Saud ambaye ameanzisha kile
kinachotajwa kuwa ni kupambana na ufisadi wa kiuchumi nchini humo, mbali
na kuwatia mbaroni mamia ya shakhsia wakubwa wakiwamo wanamfalme na
matajiri wakubwa wa nchi hiyo, pia amefunga maelfu ya akaunti za watu
hao. Baadhi ya vyanzo vya habari vimeandika kwamba, Bin Salman
ametoa sharti la kuingizwa karibu asilimia 70 ya utajiri wao
serikalini kama njia ya wao kuachiliwa huru.
No comments:
Post a Comment