Wednesday, November 8, 2017

MAANDAMANO MENGINE YAZUKA CATALONIA

Mahakama ya katiba ya Uhispania imetoa maamuzi kwamba kura ya bunge la Catalonia ya hivi karibuni ya kutangaza uhuru kutoka Uhispania ilikuwa kinyume cha sheria. 
 Maamuzi hayo yaliyotolewa leo yamekuja wakati kuna maandamano makubwa ya wanaounga mkono kujitenga waliofunga barabara na njia za treni kama sehemu ya kugomea kufungwa kwa maafisa wa serikali ya Catalonia na wanaharakati wanaopigania kujitenga kabla na baada ya azimio la Oktoba 27.
 Mahakama imeanza kwa kusimamisha utekelezaji wa azimio la kujitenga la mwezi uliopita wakati ikiangazia uhalali wake kutokana na kupingwa na serikali ya Uhispania.
  Zaidi ya barabara 50 ikiwa ni pamoja na barabara kuu zilifungwa na kusababisha usumbufu mkubwa katika jimbo hilo linalokabiliwa na hali ya sintofahamu kutokana na hatua ya serikali yake kutaka kujitenga na Uhispania. Mzozo huo umeutikisa Umoja wa Ulaya unaosaka suluhu kufuatia hatua ya ghafla ya kujitoa kwa Uingereza na kuzua hofu ya machafuko na usumbufu usiokwisha kwenye taifa hilo.

No comments:

Post a Comment