Vitendo vya ukatili na unyanyasaji dhidi ya
wanawake katika nchi za Magharibi na hasa Marekani vimefikia kiwango cha
kutia wasiwasi kinyume na inavyodaiwa huku ikiripotiwa kwamba kila siku
wanawake 600 hufanyiwa vitendo vya ukatili nchini humo.
Kwa mujibu wa shirika la habari la IRNA jitihada nyingi
zinafanywa na makundi na asasi mbalimbali ili kupunguza kiwango cha
vitendo vya ukatili na unyanyasaji dhidi ya wanawake nchini Marekani
lakini takwimu za mauaji, ubakaji na unyanyasaji dhidi ya wanawake
nchini humo zinatia wasiwasi.
Wanaharakati wa haki za binadamu nchini Marekani wanaitakidi kuwa
nchi hiyo sio tu inapaswa kuziangalia upya sheria zake kuhusu ukatili
dhidi ya wanawake, watoto wadogo wa kike na hata wa kiume lakini pia
inatakiwa izingatie na kulipa umuhimu zaidi suala la usalama katika
mazingira ya kazi, maskulini, makanisani, kwenye kambi za jeshi pamoja
na klabu za michezo na burudani.
Wakati huohuo ripoti kutoka nchini Marekani zinaeleza kuwa bunge la
nchi hiyo linaandaa mpango kwa ajili ya wafanyakazi wake wa kike ili
waweze kukabiliana na ubakaji na vitendo vya ukatili vinavyowaandama.
Ripoti hiyo imekumbusha kuwa katika kipindi cha chini ya mwezi mmoja,
shakhsia kadhaa maarufu wa kisiasa, wa tasnia ya filamu, michezo na
vyombo vya habari wamekabiliwa na tuhuma za kuwanyanyasa kijinsia
wanawake.
Hayo yanajiri huku John Conyers, mkuu wa kamati ya vyombo vya
mahakama ya Baraza la Wawakilishi la Marekani akitangaza kujiuzulu
wadhifa wake huo kutokana na kashfa ya masuala ya maadili.../
No comments:
Post a Comment