Monday, December 11, 2017

DUNIA IMEUNGANA KUMLAANI DONALD TRUMP

Iran: Dunia imeungana kumlaani Donald Trump
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran leo amezungumza na waandishi wa habari kuhusiana na masuala mengi tofauti ikiwemo ziara ya waziri wa mambo ya nje wa Uingereza hapa mjini Tehran, suala la Quds, Yemen na masuala mengine mbalimbali.
Akijibu swali la mwandishi wa Radio Tehran kuhusiana na ziara ya waziri wa mambo ya nje wa Uingereza hapa Iran ambayo imekwenda sambamba na hatua ya rais wa Marekani la kuitangaza Quds kuwa mji mkuu wa Israel, Bahram Qassemi amesema, ziara ya Boris Johnson waziri wa mambo ya nje wa Uingereza hapa Tehran ilikuwa imepangwa tangu zamani na haina uhusiano wowote na hatua hiyo ya Donald Trump.
Donald Trump analaaniwa katika kila kona ya dunia

Vile vile amesema, dunia nzima imeungana hivi sasa kumlaani Donald Trump kwa hatua yake hiyo na nchi nyingi za dunia zikiwemo za Kiarabu zinaendelea kukabiliana na uchokozi huo wa rais wa Marekani kwa njia mbalimbali.
Amma kuhusiana na msimamo wa Iran kuhusu Yemen, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema, msimamo wetu kuhusu Yemen haujabadilika na hautobadilika, kwanza sera zetu ni kutoingilia masuala ya ndani ya nchi nyingine lakini pia tutaendelea kufanya juhudi za kuwatangazia walimwengu dhulma wanayofanyiwa wananchi wa Yemen.
Amma kuhusiana na hatua ya Bahrain kutuma ujumbe wake kwenda kuonana na viongozi wa utawala wa Kizayuni katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu, Qasemi amesema, ziara hiyo haina maana, ni kosa na ni kitendo cha aibu ambacho kimeonesha sura halisi ya baadhi ya nchi za Kiarabu zinazoiunga mkono Israel inayozikaliwa kwa mabavu ardhi za Wapalestina kikiwemo Kibla cha Kwanza cha Waislamu.

No comments:

Post a Comment