Wednesday, November 29, 2017

KAMANDA WA BOKO HARAM ATIWA MBARONI, WENZAKE 4 WAUAWA, MATEKA 212 WAKOMBOLEWA

Kamanda wa Boko Haram atiwa mbaroni, wenzake 4 wauawa, mateka 212 wakombolewa
Jeshi la Nigeria limetangaza kuwa, limewakomboa raia wengine 212 waliokuwa wakishikiliwa mateka na wanachama wa kundi la kigaidi la Boko Haram katika msitu wa Sambisa.
Msemaji wa jeshi la Nigeria, Sani Usman amesema kuwa, jeshi la nchi hiyo limefanikiwa pia kumtia mbaroni mmoja wa makamanda wa Boko Haram, Amman Judee na kuwaua wapiganaji wanne wa kundi hilo la kigaidi.
Amesema kuwa, kamanda huyo wa Boko Haram aliyetiwa mbaroni anaendelea kusailiwa. Kwa mujibu wa jeshi la Nigeria, watu 212 waliokombolewa kutoka mikononi mwa wapiganaji wa Boko Haram ni kundi la pili kukombolewa na jeshi la nchi hiyo katika kipindi cha chini ya wiki moja.
Siku ya Jumamosi jeshi la Nigeria liliwakomboa raia wengine 30 waliokuwa wakishikiliwa na wanamgambo wa Boko Haram ambapo lilifanikiwa pia kuwauwa wanachama 11 wa kundi hilo la kigaidi katika kijiji cha Bama huko Borno kaskazini mashariki mwa Nigeria.
Wanamgambo wa kundi la kigaidi la Boko Haram
Baadhi ya duru zinaripoti kwamba, jeshi la Nigeria limepata mafanikio makubwa katika siku za hivi karibuni katika vita na operesheni zake dhidi ya wanamgambo wa Boko Haram.
Mashambulizi ya genge la kigaidi la Boko Haram yalianza mwaka 2009 kaskazini na kaskazini mashariki mwa Nigeria na hadi hivi sasa zaidi ya watu 20 elfu wameshauwa kutokana na machafuko yaliyosababishwa na kundi hilo.
Kundi la Boko Haram limekuwa likifanya jinai za kila namna ikiwa ni pamoja na kuteka nyara watu pamoja na wasichana na kuwapiga mnada kama bidhaa. 

RAIS BUHARI: RAIA WA NIGERIA WAMEKUWA WAKIUZWA KAMA MBUZI NCHINI LIBYA

Rais Buhari: Raia wa Nigeria wamekuwa wakiuzwa kama mbuzi nchini Libya
Rais Muhammadu Buhari wa Nigeria amesema kuwa, raia wote wa nchi hiyo ambao wamekwama huko Libya watarejeshwa nyumbani na kusaidiwa kurejelea maisha ya kawaida.
Akizungumzia video za karibuni ambazo zimekuwa zikiwaonesha Waafrika wakiuzwa kwenye mnada wa watumwa nchini Libya, Rais Buhari amesema inasikitisha sana kwamba "baadhi ya raia wa Nigeria wanauzwa kama mbuzi  kwa  dola kadhaa huko Libya".
Rais wa Nigeria ameonekana pia kushangaa iwapo raia wa Libya walijifunza lolote la maana tangu kuondolewa madarakani kwa Kanali Muammar Gaddafi mwaka 2011.
''Walichojifunza pekee ni kuwapiga watu risasi na kuua. Hawakujifunza kuwa mafundi wa umeme, mafundi wa mabomba au ufundi wowote ule," amesema.
Rais Muhamadu Buhari wa Nigeria
Hayo yanajiri katika hali ambayo, radiamali mbalimbali zimeendelea kutolewa kuhusiana na taarifa za kuweko biashara ya utumwa nchini Libya.
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limetoa mwito wa kuendeshwa vita dhidi ya magendo ya binadamu na biashara ya utumwa katika bara la Afrika.
Filippo Grandi, Kamishna Mkuu wa Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa UNHCR amesema,  kuna haja ya kukabiliana na biashara ya utumwa na vitendo vingine vya ukiukaji wa haki za binadamu vinavyofanywa dhidi ya wahajiri wanaopitia Libya wakiwa na nia ya kuelekea barani Ulaya kutafuta maisha mazuri.
Itakumbukwa kuwa, hivi kkaribuuni, televisheni ya CNN ilirusha hewani mubashara mnada wa kuuza Waafrika huko nchini Libya ambapo kila mtu alikuwa akiuzwa kwa dola zisizopungua 400 za Kimarekani. 

VIONGOZI WA ULAYA WAKUTANA NA WENZAO WA AFRIKA ABIDJAN

Viongozi wa Umoja wa ulaya wameanza mazungumzo yao pamoja na viongozi wenzao wa bara la Afrika kuhusu uhamaji, wakipania kuupatia ufumbuzi mzozo wa watu wanaoyatia hatarini maisha yao kwa lengo la kuingia barani Ulaya.
EU-Afrika-Gipfel in Abidjan (picture-alliance/dpa/M. Kappeler)
Viongozi kutoka Ufaransa, Ubeigiji, Luxemburg, wote wakiwa ni viongozi wa kiume wenye umri unaokurubia miaka 40 wanajaribu kujitenganisha na picha ya wakoloni wa zamani wa Afrika, wakitetea umuhimu wa kuendeleza biashara na kuwekeza katika miradi ya maendeleo na usalama barani humo pamoja na kushughulikia vyanzo vya uhamaji.
Uhamaji ndio mada kuu katika mkutano huu wa kilele mjini Abidjan, mji mkuu wa kibiashara wa Côte d'Ivoire, mada iliyopata nguvu kutokana na kanda ya video iliyotangazwa hivi karibuni na kituo cha televisheni cha CNN  na kuonyesha jinsi vijana wa kiafrika walivyokuwa wakiuzwa kama watumwa katika masoko ya mnada nchini Libya. Akizungumza kuhusu kisa hicho cha karaha, kansela Angela Merkel amesema:"Mada ya uhamaji kinyume na sheria inakamata nafasi muhimu katika bara lote la Afrika wakati huu tulio nao kwasabau kuna rirpoti zinazosema vijana wa kiafrika wamekuwa wakiuzwa kama watumwa nchini Libya. Na hiyo ndio sababu mada hiyo inazusha jazba kubwa katika mkutano huu. Kwa hivyo yameibuka masilahi ya pamoja ya kukomesha uhamaji kinyume na sheria na kuwafungulia njia watu kutoka Afrika kuweza kuja Ulaya kusoma au kujifunza kazi."
Kansela Angela Merkel akizungumza na mwenyeji wakle, rais Alassane Ouattara wa Côte d'Ivoire Kansela Angela Merkel akizungumza na mwenyeji wakle, rais Alassane Ouattara wa Côte d'Ivoire
Biashara ya watumwa ni uhalifu dhidi ya ubinaadam
Kansela Merkel amesema hayo mwanzoni mwa mkutano wa kilele wa viongozi wa Umoja wa ulaya na Afrika mjini Abidjan. Jana usiku rais wa Ufaransa Emmanuel Macron aliitaja biashara ya wahamiaji wa kiafrika kuwa "uhalifu dhidi ya ubinaadam. Macron amesema anataka nchi za Ulaya na zile za Afrika ziwasaidie watu waliokamwa nchini Libya ili waweze kurejeshwa makwao. Aliahidi kufafanua zaidi kuhusu juhudi hizo katika mkutano huu wa kilele ulioanza hivi punde mjini Abidjan.
Meli ya kuwaokoa wakimbizi wa Afrika wanaoelekea Ulaya kupitia bahari ya kati Meli ya kuwaokoa wakimbizi wa Afrika wanaoelekea Ulaya kupitia bahari ya kati
 Viongozi vijana wa Ulaya wanataka kuondokana na sura ya wakoloni wa zamani
Waziri mkuu wa ubeligiji, Charles Michel amewahimiza viongozi wenzake wa Ulaya washirikiane kwa dhati zaidi na wenzao wa Afrika katika suala la uhamaji na usalama, mada ya pili muhimu itakayojadiliwa katika mkutano huu wa kilele wa siku mbili mjini Abidjan.
Tunachokitaka ni mkakati utakaoleta manufaa kwa pande zote mbili amesema Michel mwenye umri wa miaka 41. Ameongeza kusema anatoka katika kizazi kinacholiangalia bara la Afrika kama mshirika, hakuna upenu katika kizazi chetu wa kufikiria yaliyotokea zamani" amesema waziri mkuu huyo wa Ubeligiji aliyefuatana na mwenzake wa Luxemburg Xavier Bettel, wakionyesha sura tofauti na ile ya walio watangulia.

Tuesday, November 28, 2017

UHURU KENYATTA AAPISHWA LEO NCHINI KENYA

Uhuru Kenyatta aapishwa kama rais wa Kenya
Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya ameapishwa kuiongoza nchi hiyo kwa muhula wa pili wa miaka mitano mjini Nairobi leo katika sherehe iliyohudhuriwa na maelfu ya wafuasi wake na viongozi kadhaa wa nchi za Afrika.
Rais Kenyatta amekula kiapo katika Uwanja wa Kasarani mjini Nairobi kufuatia ushindi wake katika uchaguzi wa marudio wa Oktoba 26 ambao ulisusiwa na kinara wa upinzani Raila Odinga kwa madai kuwa haukuwa huru na wa haki. Mahakama ya Kilele Kenya ilibatilisha uchaguzi uliokuwa umefanyika Agosti nane kwa msingi kuwa kulikuwepo na dosari.
Kati ya viongozi waliohudhuria sherehe hizo ni Waziri Mkuu wa Ethiopia Hailemariam Desalegn, Marais Paul Kagame wa Rwanda, Mohamed Abdullahi Mohamed wa Somalia, Salva Kiir wa Sudan Kusini, Ian Khama wa Botswana Yoweri Museveni wa Uganda, Omar Bongo wa Gabon, Egar Lungu wa Zambia, Ismaïl Omar Guelleh wa Djibouti, na Hage Geingob wa Namibia. Tanzania imewakilishwa na Makamu wa Rais Samia Suluhu baada ya Rais John Magufuli kukosa kuhudhuria kama ilivyotarajiwa. Katika hotuba yake, Rais Kenyatta ametangaza kwamba Mwafrika yeyote atapewa viza akifika katika kiingilio chochote mpakani au viwanja vya ndege Kenya.
Rais Kenyatta baada ya kuapishwa
Aidha Kenyatta amesema ana malengo mawili katika muhula wake wa mwisho. Kwanza kuimarisha uwiano na umoja miongoni mwa Wakenya. Ameongeza kuwa ameanza kuwasiliana na viongozi wote na kueleza nia yake ya kuendeleza umoja. Halikadhalika amesema lengo la pili ni kuhakikisha huduma ya afya inawafikia Wakenya 100%. Naibu wa Rais William Ruto pia ameapishwa katika sherehe hiyo.
Katika upande mwingine polisi mjini Nairobi waliliazimka kutumia gesi ya kutoa machozi kuwatawanya wafuasi wa Raila Odinga waliokuwa wanakutana katika uwanja wa Jacaranda katika mtaa wa Embakasi walikokuwa wamekusanyika  kuwaomboleza waliouawa katika ghasia za baada ya uchaguzi.

Monday, November 27, 2017

UHURU KUAPISHWA LEO, KAMBI YA UPINZANI YASUSIA, YAITISHA MKUTANO JACARANDA

Uhuru kuapishwa leo, kambi ya upinzani yasusia, yaitisha mkutano Jacaranda
Mivutano ya kisiasa inaonekana kupamba moto zaidi leo nchini Kenya huku vyombo vya usalama vikilinda maeneo muhimu ya jiji la Nairobi kabla ya kuapishwa Rais Uhuru Kenyatta hii leo kwa ajili ya kipindi cha awamu ya pili.
Kenyatta ambaye alishinda uchaguzi wa marudio wa tarehe 26 Oktoba uliosusiwa na kambi ya upinzani, anaapishwa leo huku chama kikuu cha upinzani cha NASA kikiwataka wafuasi wake kususia sherehe hiyo na badala yake wakusanyike katika uwanja wa Jacaranda katika eneo la Embakasi mjini Nairobi kwa kile kinachosemekana ni kuomboleza mauaji ya wafuasi wa kinara wa kambi ya upinzani, Raila Odinga, waliouawa na maafisa wa polisi katika ghasia za uchaguzi wa rais.
Watu zaidi ya 70 waliuawa katika vurugu za kisiasa msimu huu wa uchaguzi, wengi wao wakiwa wameuawa kwa kupigwa risasi na polisi.
Polisi ya Kenya ikikabiliana na waandamanaji
Jumamosi iliyopita kamanda wa polisi mjini Nairobi, Japhet Koome alisema kuwa muungano wa upinzani wa NASA haujaitaarifu polisi kuhusu mkutano huo.
Koome alisisitiza kuwa jeshi la polisi litakabiliana na mtu yeyote atakayefanya mkutano bila ya kuliarifu jeshi hilo.
Rais Uhuru Kenyatta amewataka Wakenya kuungana na kufanya kazi pamoja baada ya ushindani wa kisiasa ili kulijenga taifa hilo.
Viongozi wa nchi kadhaa za kigeni wamealikwa katika sherehe ya kuapishwa Rais Uhuru Kenyatta.

Sunday, November 26, 2017

DURU MPYA YA MAZUNGUMZO YA BURUNDI KUANZIA LEO ARUSHA, TANZANIA

Duru mpya ya mazungumzo ya Burundi kuanza leo Arusha, Tanzania
Duru mpya ya mazungumzo ya amani ya Burundi inaanza leo Jumatatu huko Arusha, kaskazini mwa Tanzania, na itaendelea hadi Disemba 8.
Mazungumzo hayo yanaongozwa na Benjamin William Mkapa, Rais mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye ni mpatanishi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki katika mgogoro wa kisiasa wa Burundi. 
Muungano wa upinzani wa CNARED umesema hautashiriki katika mazungumzo hayo ukisisitiza kuwa, mpatanishi wa mgogoro huo Benjamin Mkapa amekuwa akiegemea upande wa serikali. 
Wawakilishi wa serikali ya Burundi walikataa kushiriki mazungumzo ya moja kwa moja na wawakilishi wa CNARED katika mazungumzo yaliyopita, wakiwatuhumu kuhusika na jaribio lililofeli la mapinduzi dhidi ya serikali ya Rais Pierre Nkurunziza mnamo Mei 14, 2015. 
Benjami Mkapa, rais mstaafu wa Tanzania
Burundi ilitumbukia katika machafuko mwishoni mwa mwezi Aprili mwaka 2015 baada ya chama tawala cha CNDD-FDD kumuidhinisha Nkurunziza kugombea urais katika uchaguzi mkuu uliopita kwa mara ya tatu mfululizo.
Wapinzani waliitaja hatua ya Rais Nkurunziza kushiriki katika uchaguzi huo kwamba ilikiuka katiba na hati ya makubaliano ya amani ya Arusha lakini serikali ya Bujumbura ilisema haijakiuka sheria.
Kwa mujibu wa mashirika mbali mbali ya haki za binadamu, watu zaidi ya elfu 2 wameuawa katika machafuko hayo, kiasi cha majaji wa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC kuruhusu kuanzishwa uchunguzi kuhusu ukatili na jinai dhidi ya binadamu uliofanywa katika kipindi cha kati ya mwaka 2015 na 2017. Ifahamike kuwa, Burundi ilijiondoa kwenye Mkataba wa Roma uliounda mahakama hiyo ya mjini The Hague, Uholanzi.

KILA SIKU WANAWAKE 600 HUFANYIWA VITENDO VYA UKATILI NCHINI MAREKANI

Kila siku wanawake 600 hufanyiwa vitendo vya ukatili nchini Marekani
Vitendo vya ukatili na unyanyasaji dhidi ya wanawake katika nchi za Magharibi na hasa Marekani vimefikia kiwango cha kutia wasiwasi kinyume na inavyodaiwa huku ikiripotiwa kwamba kila siku wanawake 600 hufanyiwa vitendo vya ukatili nchini humo.
Kwa mujibu wa shirika la habari la IRNA jitihada nyingi zinafanywa na makundi na asasi mbalimbali ili kupunguza kiwango cha vitendo vya ukatili na unyanyasaji dhidi ya wanawake nchini Marekani lakini takwimu za mauaji, ubakaji na unyanyasaji dhidi ya wanawake nchini humo zinatia wasiwasi.
Wanaharakati wa haki za binadamu nchini Marekani wanaitakidi kuwa nchi hiyo sio tu inapaswa kuziangalia upya sheria zake kuhusu ukatili dhidi ya wanawake, watoto wadogo wa kike na hata wa kiume lakini pia inatakiwa izingatie na kulipa umuhimu zaidi suala la usalama katika mazingira ya kazi, maskulini, makanisani, kwenye kambi za jeshi pamoja na klabu za michezo na burudani.
Wakati huohuo ripoti kutoka nchini Marekani zinaeleza kuwa bunge la nchi hiyo linaandaa mpango kwa ajili ya wafanyakazi wake wa kike ili waweze kukabiliana na ubakaji na vitendo vya ukatili vinavyowaandama.
John Conyers
Ripoti hiyo imekumbusha kuwa katika kipindi cha chini ya mwezi mmoja, shakhsia kadhaa maarufu wa kisiasa, wa tasnia ya filamu, michezo na vyombo vya habari wamekabiliwa na tuhuma za kuwanyanyasa kijinsia wanawake.
Hayo yanajiri huku John Conyers, mkuu wa kamati ya vyombo vya mahakama ya Baraza la Wawakilishi la Marekani akitangaza kujiuzulu wadhifa wake huo kutokana na kashfa ya masuala ya maadili.../

Saturday, November 25, 2017

HASIRA ZA WATU WA BANGUI BAADA YA GARI LA MINUSCA KUMUUA MWANAFUNZI

Hasira za watu wa Bangui baada ya gari la MINUSCA kumuua mwanafunzi
Wananchi katika mji mkuu wa Jamhuri ya Afrika ya Kati, Bangui wamebainisha ghadhabu zao baada ya mwanafunzi wa shule kupoteza maisha katika ajali iliyohusisha gari la askari wa Mpango wa Umoja wa Mataifa nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati MINUSCA.
Saa chache baada ya ajali hiyo, gari la Umoja wa Mataifa lililokuwa likipita Bangui lilishambuliwa na watu wenye hasira na kuchomwa moto hali iliyohatarisha maisha ya abiria waliokuwemo ambao walinusurika kuuawa.
Pia gari la zimamoto lililotumwa na MINUSCA lilishambuliwa na umati wa watu na kuharibiwa ambapo askari mmoja wa zimamoto alijeruhiwa. Matukio haya mawili kwa mujibu wa MINUSCA yalifuatiwa na mashambulizi mengine kadhaa dhidi ya magari ya mpango huo katika mji mzima wa Bangui.
MINUSCA inashirikiana na serikali, jeshi la polisi la nchi hiyo na wadau wengine kuhakikisha utulivu unarejea katika mji huo mkuu wa Jamhuri ya Afrika ya Kati.
MINUSCA imekaribisha taarifa ya serikali ya CAR baada ya tukio la ajali ya bahati mbaya  iliyokatisha maisha ya kijana mwanafunzi mjini Bangui.
MINUSCA imesikitishwa na kifo hicho na kuungana na serikali kutoa wito wa kudumisha utulivu miongoni mwa wananchi baada ya tukio hilo kuzusha maandamano ya ghasia mjini Bangui dhidi ya Umoja wa Mataifa.
Askari wa MINUSCA
Katika tukio hilo waziri wa habari na msemaji wa serikali ya CAR akaeleza kwamba MINUSCA ingependa kuwafahamisha kuwa gari lililomgonga na kumuua mwanafunzi huyo ni mali yake lakini lilikuwa likiendeshwa  na mwanajeshi wa jeshi la Jamhuri ya Afrika ya Kati (FACA).
Hayo yanajiri katika hali ambayo ukosoaji dhidi ya wanajeshi hao wa MINUSCA wapatao elfu 13  umeendelea kuongezeka kutokana na wananchi kutoridhishwa na utendaji wa vikosi hivyo katika kuwalinda raia wa Jamhuri ya Afrika ya Kati. Askari hao wanalaumiwa kwa kutozuia mauaji ya Waislamu nchini humo.
Machafuko huko Jamhuri ya Afrika ya Kati (CAR) yalizuka mwaka 2013, baada ya waasi wa Seleka kumuondoa madarakani aliyekuwa rais wa nchi hiyo, François Bozizé. Baada ya rais Mwislamu, Michel Djotodia kuchukua mamlaka, waasi na magaidi wa Kikristo wenye misimamo ya kufurutu ada wa Anti-Balaka walianzisha mauaji ya kimbari dhidi ya jamii ya Waislamu, ambapo maelfu ya Waislamu waliuawa na wengine wengi kuwa wakimbizi.

IRAN YALAANI VIKALI HUJUMA YA KIGAIDI MSIKITINI MISRI

Iran yalaani vikali  hujuma ya kigaidi msikitini Misri
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imelaani vikali hujuma ya kigaidi wakati wa Sala ya Ijumaa msikitini katika mkoa wa Sinai Kaskazini nchini Misri.
Katika taarifa kupitia ukurasa wake wa Twitter, Waziri wa Mambo ya Nje ya Iran Mohammad  Jawad Zarif amesema ugaidi hauheshimu thamani za Kiungu na kibinadamu.
Zarif ameongeza kuwa: "Kwa mara nyingine ugaidi umetoa pigo kwa taifa azizi la Misri na kwa mara nyingine kuthibitisha kuwa hautafautishi mahali hata ndani ya msikiti na maeneo mengine ya ibada."
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amelaani vikali hujuma hiyo ya kigaidi na kumuomba Mwenyezi Mungu awarehemu mashahidi na kuwapa majeruhi nafuu ya haraka.
Mohammad Javad Zarif
Jana Waislamu wasiopungua 235 wameuawa na wengine zaidi ya 110 kujeruhiwa katika shambulizi la magaidi wakufurishaji dhidi ya msikiti mmoja wa Twariqa katika Peninsula ya Sinai nchini Misri.
Duru za polisi nchini humo zimesema genge la kigaidi limeushambulia Msikiti wa al-Rawdhah ulioko katika mji wa Bir al-Abd, yapata kilomita 40 kutoka mji wa Al-Arish, makao makuu ya mkoa wa Sinai Kaskazini. 
Rais Abdulfattah al-Sisi wa Misri sanjari na kulaani hujuma hiyo, ameitisha mkutano wa dharura na vyombo vya usalama huku akitangaza siku tatu za maombolezo ya kitaifa, kufuatia ukatili huo wa magaidi.

MAREKANI YAUNGA MKONO JINAI ZA SAUDIA DHIDI YA RAIA WA YEMEN

Marekani yaunga mkono jinai za Saudia dhidi ya raia wa Yemen
Ikulu ya Rais wa Marekani, White House, imetangaza kuunga mkono jinai za utawala wa Saudi Arabia dhidi ya Yemen.
Katika taarifa siku ya Ijumaa, White House, pasi na kuashiria indhari za taasisi za kimataifa kuhusu nafasi ya Marekani na muitifaki wake , Saudia, katika kuleta maafa ya kibinadamu nchini Yemen, kwa mara nyingine ilitangaza uungaji mkono wa Washington kwa Saudia na waitifaki wake katika vita dhidi ya Yemen.
Taarifa ya Ikulu ya White House, kinyume na ukweli wa mambo, ilidai kuwa utawala wa Saudia umefungua Bandari ya Al Hudayda na Uwanja wa Ndege wa Sanaa.
Utawala wa Riyadh,ambao unadhibiti mipaka yote ya kimatiafa ya Yemen, ulikuwa umeahidi kufungua Bandari ya Hudayda na Uwanja wa Ndege wa Sanaa baada ya kufunga maeneo hayo mawili 24 Novemba na kwa msingi hiyo kuzuia misaada ya kibinadamu kuingia katika eneo hilo.
Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula Dunaini, WFP, limeonya kuwa mamilioni ya watu wa Yemen wanakabiliwa na hatari ya mauti kufuatia mzingiro uliowekwa na Saudi Arabia dhidi ya nchi hiyo na hivyo kuzuia misaada kuwafikia wanaohitajia.
Watoto ni waathirika wa jinai za Saudia nchini Yemen
Saudia ilianzisha hujuma yake dhidi ya Yemen mnamo Machi mwaka 2015 kwa uungaji mkono wa Marekani kwa lengo la kuirejesha madarakani serikali kibaraka ya Abdu Rabuh Mansour Hadi aliyejiuzulu urais na kukimbilia mji mkuu wa Saudia, Riyadh. Hivi sasa Saudia inzuia misaada kuwafikia mamilioni ya watu wa nchi hiyo wanaokabiliwa na njaa.
Raia zaidi ya elfu 13  wa Yemen wameuawa, hasa wanawake na watoto, na maelfu ya wengine kujeruhiwa katika uvamizi huo wa kijeshi huku Umoja wa Mataifa ukishindwa kuchukua hatua yoyote ya kuzuia jinai hizo za Saudia huko Yemen. Aidha watu zaidi ya laki sita wameambukizwa ugonjwa wa kipindupindu kote Yemen huku wengine zaidi ya 2,000 wakifarikia dunia tokea mwezi Aprili mwaka huu.

Wednesday, November 22, 2017

KUJIUZULU MUGABE NA MUSTAKABALI WA KISIASA WA ZIMBABWE

Kujiuzulu Mugabe na mustakabali wa kisiasa wa Zimbabwe
Hatimaye baada ya takribani wiki moja ya changamoto, mivutano na uingiliaji wa jeshi hatimaye Rais Robert Gabriel Mugabe wa Zimbabwe ameng'atuka madarakani. Mugabe amechukua hatua hiyo baada ya Bunge kuanzisha mchakato wa kumsaili kwa lengo la kumuuzulu.
Kujiuzulu Mugabe kumehitimisha karibu miongo minne ya utawala wake nchini Zimbabwe. Pamoja na hayo japokuwa kujiuzulu kwake kumewafurahisha Wazimbabwe wengi wakiwemo wanachama na wafuasi wa chama chake tawala cha ZANU-PF lakini wako pia waliohuzunishwa. Ni kama alivyosema Terence Mukupe, mbunge na mwanachama wa Zanu-pf ya kwamba: "wabunge wa chama tawala hawakutaka mwisho wa rais wao uwe kama hivi. Sisi tunampenda rais, lakini wakati ulikuwa umeshafika wa yeye kujistaafisha mwenyewe. Waliomzunguka walikuwa wakimshauri vibaya sana. Tunasikitika sana amefikia ukingoni namna hivi".
Mugabe akihutubia siku ya uhuru wa Zimbabwe mwaka 1980
Robert Mugabe aliingia madarakani nchini Zimbabwe mwaka 1980 akiwa anajulikana kama shakhsia mashuhuri zaidi wa mapambano dhidi ya ukoloni na harakati za kupigania uhuru wa nchi yake. Mugabe alikuwa pia mmoja wa shakhsia wakubwa wa mapambano dhidi ya ubaguzi wa rangi na mfumo wa Apathaidi katika nchi jirani na Zimbabwe ya Afrika Kusini.
Robert Mugabe aliongoza mapambano dhidi ya wakoloni hadi nchi yake ikapata uhuru; na akiwa kiongozi wa mapambano ya ukombozi wa Zimbabwe, akawa waziri mkuu wa kwanza wa taifa hilo changa wakati huo. Mara baada ya kushika madaraka, kwa kutumia kaulimbiu ya umoja alianzisha sera ya kuleta maridhiano nchini. Waziri Mkuu huyo wa Zimbabwe aliamua kukabidhi nyadhifa na vyeo muhimu kwa raia wazungu. Kutokana na hatua yake hiyo, katika kipindi cha karibu muongo mmoja Zimbabwe ilipata mafanikio mazuri kiuchumi, ikapiga hatua kuelekea kwenye ustawi kwa kujenga mashule, vituo vya afya na tiba pamoja na kuwajengea nyumba raia wazalendo weusi ambao ndio wanaounda idadi kubwa ya watu wa nchi hiyo. 
Majenerali wa jeshi walioongoza kampeni ya kumwondoa Mugabe madarakani
Pamoja na hayo, kuwakandamiza wapinzani na kutekeleza sera za chama kimoja zilikuwa miongoni mwa siasa za Mugabe zilizokosolewa sana na wapinzani. Katika hali kama hiyo, umri mkubwa alionao, uingiliaji wa mke wake Grace na kampeni zake za kutaka kutwaa madaraka, hali mbaya ya uchumi  na vilevile kufichuliwa ufisadi uliofanywa na baadhi ya jamaa wa Mugabe na wanachama wa chama chake cha Zanu-pf yote hayo yalishadidisha upinzani dhidi ya kiongozi huyo.
Hivi ndivyo wabunge na maseneta walivyoipokea habari ya kujiuzulu Mugabe
Hivi sasa baada ya Mugabe kuondoka madarakani, hali ya kisiasa nchini Zimbabwe imebadilika. Kwa mujibu wa habari mbalimbali Emmerson Mnangagwa, makamu wa rais ambaye alitimuliwa na Mugabe na ambaye sasa amechaguliwa kuwa mwenyekiti wa Zanu-pf, ndiye atakayeshika hatamu za urais wa nchi. Wachambuzi wengi wanaamini kuwa Mnangagwa ataendeleza siasa za Mugabe, tab'an kwa kutegemea nguvu za jeshi. Pamoja na hayo watu wengi wana wasiwasi wa kutokea hali ya kukomoana na ulipizaji visasi wa ndani ya chama na kuvurugika hali ya kisiasa ya Zimbabwe. Kiasi kwamba kwa kuchelea hali hiyo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ametoa wito kwa Wazimbabwe wote "kudumisha utulivu na uvumilivu".
Wananchi wakipachua picha ya Mugabe baada ya kujua kwamba si rais tena wa Zimbabwe
Kurejesha uthabiti wa kisiasa, kujiepusha na sera za kutawala kijeshi na kidikteta, kustawisha maelewano na nchi za eneo na nje ya eneo, kuboresha hali ya uchumi na kuitishwa uchaguzi mkuu katika mwaka ujao wa 2018 katika mazingira tulivu na kwa kuheshimu sheria ni miongoni mwa matarajio muhimu zaidi waliyonayo wananchi; matarajio ambayo kama hayatotimizwa si hasha yakawafanya Wazimbabwe wengi watamani kurejea tena kwenye enzi za Mugabe.../

MNANGAGWA AREJEA ZIMBABWE, KUPISHWAIJUMAA KUMRITHI MUGABE

Mnangagwa arejea Zimbabwe, kuapishwa Ijumaa kumrithi Mugabe
Makamu wa Rais wa Zimbabwe aliyepigwa kalamu nyekundu hivi karibuni na Rais Robert Mugabe aliyetangaza kujiuzulu hapo jana amerejea nchini akitokea Afrika Kusini.
Emmerson Mnangagwa alifutwa kazi wiki mbili zilizopita na kukimbia nchi akihofia usalama wake. Mwanasiasa huyo alipigwa kalamu kutokana na kile wadadisi wa mambo walikitaja kuwa ni hatua ya Mugabe mweye umri wa miaka 93 kumsafishia njia mkewe Grace Mugabe, arithi kiti chake.
Wananchi wa Zimbabwe mjini Harare wamebeba mabango yenye picha za Mnangagwa zilizoambatana na jumbe zisemazo: Karibu nyumbani shujaa wetu; Uliahidi utarejea na kweli umerejea, karibu sana. Baadhi ya picha za mwanasiasa huyo zilikuwa na jina lake la utani la "Mamba".
Jacob Mudenda, Spika wa Bunge la nchi hiyo amesema maandalizi ya kumuapishwa Mnangagwa Ijumaa ijayo ili kuchukua nafasi ya Mugabe yanaelekea kukamilika.
Mugabe na Mnangagwa katika sherehe ya taifa huko nyuma
Akiongea baada ya kukutana na Rais Jacob Zuma wa Afrika Kusini kabla ya kuondoka nchini humo mapema leo, Mnangagwa amesema: "Taifa hili halipaswi tena kushikwa mateka na mtu mmoja, ambaye yuko tayari kufia ofisini kwa gharama yoyote ile."
Hapo jana Jumanne, Mugabe katika barua yake kwa Spika wa Bunge, alisema amejiuzulu kwa khiari yake mwenyewe ili kupisha mapokezano ya uongozi kwa njia ya amani, baada ya kuiongoza nchi hiyo ya kusini mwa Afrika kwa miaka 37.
Baada ya Spika wa Bunge la Zimbabwe kutoa tangazo la kujiuzulu kwa Mugabe, wananchi wa taifa hilo walijitokeza mabarabarani kwa shangwe, nderemo na vifijo kusherehekea habari hizo.

UMOJA WA MATAIFA WAIKOSOA BURUNDI KWA KUTISHIA MAAFISA WAKE

Umoja wa Mataifa waikosoa Burundi kwa kutishia maafisa wake
Ofisi ya masuala ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa imeikosoa vikali serikali ya Burundi kwa kuwatishia wataalamu wa uchunguzi wa umoja huo.
Rupert Colville, msemaji wa Zeid Ra'ad al-Hussein, Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa ameiandikia barua serikali ya Bujumbura akiitaka iwaonye maafisa wake dhidi ya kutishia maisha ya wajumbe wa Kamisheni ya Uchunguzi ya UN, waliotoa mwito wa kubebeshwa dhima maafisa wa ngazi za juu wa Burundi wanaotuhumiwa kufanya jinai dhidi ya binadamu.
Katika barua hiyo, Colville amesema Burundi kama nchi mwanachama wa Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa inapaswa kushirikiana na kuheshimu maamuzi ya chombo hicho.
Hivi karibuni, Burundi ilitangaza kuwa haitashirikiana na Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) katika uchunguzi wa jinai za kivita na ukatili uliofanyika nchini humo katika kipindi cha miaka miwili iliyopita.
Maafisa usalama wa Burundi wanatuhumiwa kuhusika na mauaji ya raia
Novemba 9 mwaka huu, majaji wa mahakama hiyo waliruhusu kuanzishwa uchunguzi kuhusu ukatili na jinai dhidi ya binadamu uliofanywa katika kipindi cha kati ya mwaka 2015 na 2017 dhidi ya raia wa Burundi ndani au nje ya nchi hiyo. Jinai hizo ni pamoja na mauaji, ubakaji, ukatili na mateso yaliyoanza mwaka 2015 baada ya Rais wa Burundi, Pierre Nkurunziza kutangaza nia yake ya kugombea kiti hicho kwa muhula wa tatu mfululizo. 
Ni vyema kuashiria hapa kuwa, Oktoba 26, Burundi ilijiondoa rasmi kwenye Mkataba wa Roma uliounda ICC.

BAADA YA MUGABE KUJIUZULU, UMOJA WA MATAIFA WAWATAKA WAZIMBABWE KUDUMISHA UTULIVU

Baada ya Mugabe kujiuzulu, Umoja wa Mataifa wawataka Wazimbabwe kudumisha utulivu
Umoja wa Mataifa umewataka wananchi wa Zimbabwe kudumisha amani na utulivu katika kipindi hiki baada ya Rais Robert Mugabe kutangaza kujiuzulu hapo jana.
Antonio Guterres, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amewataka wananchi wa nchi hiyo kudumisha amani na utulivu katika kipindi hiki inachopitia nchi yao baada ya kiongozi wa nchi hiyo kujiuzulu.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amezitaka tawala zote kuheshimu matakwa ya wananchi. Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe hatimaye jana alisalimu amri na kukubali kujiuzulu kufuatia mashinikizo ya kila upande ya kumtaka aachie madaraka. 
Jacob Mubenda, Spika wa Bunge la Zimbabwe alitangaza jana kwamba, amepokea barua ya kujiuzulu kutoka kwa kiongozi huyo mkongwe mwenye umri wa miaka 93.
Robert Mugabe amejiuzulu baada ya kuiongoza Zimbabwe kwa miaka 37
Katika barua hiyo ya kujiuzulu, Mugabe alisema anajiuzulu kwa hiari, ili kupisha mapokezano ya uongozi kwa njia ya amani, baada ya kuiongoza nchi hiyo ya kusini mwa Afrika kwa karibu miongo minne.
Baada ya Spika wa Bunge la Zimbabwe kutoa tangazo la kujiuzulu kwa Mugabe, wananchi wa taifa hilo walijitokeza mabarabarani kwa shangwe, nderemo na vifijo kusherehekea habari hiyo.
Jeshi la Zimbabwe Jumatano lilitangaza Jumatano iliyopita kwamba, Mugabe na familia yake wapo katika kifungo cha nyumbani na kisha kumuondoa uongozini. Jeshi la Zimbabwe lilichukua hatua hiyo kama radiamali kwa hatua ya siku kadhaa zilizopita iliyochukuliwa na Mugabe ya kumuuzulu aliyekuwa Makamu wake Emmerson Mnangagwa ili aweze kumrithisha nafasi hiyo mkewe  Bi Grace Mugabe.

Sunday, November 19, 2017

MUGABE ATIMULIWA NA KAMA KIONGOZI WA ZANU-PF

Rais Robert Mugabe ametimuliwa kama kiongozi wa chama tawala nchini Zimbabwe – ZANU-PF katika hatua ya kulazimisha kufikishwa kikomo miaka yake 37 madarakani kufuatia mapinduzi ya kijeshi
Simbabwe - Kinderkadetten im Harare-Nationalstadion (Getty Images/AFP/A. Joe)
Nafasi yake imechukuliwa na Emmerson Mnangagwa, naibu wake ambaye alimfuta kazi mwezi huu. Hayo ni kwa mujibu wa duru katika mkutano maalum wa ZANU-PF ulioandaliwa leo kuamua hatima ya Mugabe. Mke wa Mugabe, Bi Grace Mugabe, ambaye alikuwa na mipango ya kumrithi mumewe, pia ametimuliwa chamani.
Muda wa yeye kujiuzulu ni Jumatatu 20.11.2017 saa sita za mchana, lasivyo chama kitaanzisha mchakato wa kumvua madaraka bungeni. Chama cha ZANU-PF kimesema kuwa Mnangagwa atarejeshwa chamani kama kama kaimu kiongozi. Hoja ya kumuondoa Mugabe ilipokelewa kwa shangwe na vifijo na wajumbe wa mkutano
Akizungumza kabla ya mkutano huo wa leo, kiongozi wa chama cha maveterani wa kivita Chris Mutsvangwa amesema Mugabe ambaye ana umri wa miaka 93,  anaishiwa na muda  wa kufanya mazungumzo ya kuondoka kwake na anapaswa kuondoka nchini humo mapema iwezekanavyo.
Mutsvangwa amefuatisha na kitisho cha kuitisha maandamano kama Mugabe atakataa kuondoka, akiwaambia wanahabari kuwa "tutarejesha waandamanaji na watafanya shughuli yao”. Mnangagwa, kiongozi wa zamani wa usalama wa taifa, anayefahamika kama "mamba”, sasa ndiye anaonekana atakayeongoza serikali ya mpito ya umoja wa kitaifa baada ya kuondoka Mugabe ambayo itaangazia kujenga upya mahusiano na ulimwengu wan je na kuuokoa uchumi ambao unashuka kwa kasi.

WIMBI LA KAMATAKAMATA SAUDIA KWA MADAI YA UFISADI LAENDELEA, SASA NI VIONGOZI WA KIJESHI

Wimbi la kamatakamata Saudia kwa madai ya ufisadi laendelea, sasa ni viongozi wa kijeshi
Katika muendelezo wa wimbi jipya la kamatakamata ambalo halijawahi kushuhudiwa nchini Saudia kwa madai ya kufanyika mageuzi na kupambana na ufisadi viongozi wa ngazi ya juu wa kijeshi wametiwa nguvuni nchini humo.
Hayo ni kwa mujibu wa baadhi ya magazeti mashuhuri ya Uingereza ambayo yametangaza kwamba, katika hali ambayo Mohammad Bin Salman Al Saud anadai kufanya marekebisho nchini Saudia, uhalisia wa mambo ni kwamba mrithi huyo wa kiti cha ufalme anapambana na wapinzani wake tu.
Mohammad Bin Salman Al Saud akiwa na Rais Donald Trump wa Marekani
Chanzo kimoja ndani ya ukoo wa kifalme wa Aal-Saud ambacho hakikutaka kutaja jina lake kimefichua kwamba, hadi sasa viongozi 14 wa ngazi ya juu wa gadi ya taifa na Wizara ya Ulinzi ya Saudia ambao wamestaafu, wametiwa nguvuni kwa tuhuma za kushiriki katika kutia saini mikataba ya kifedha inayotia shaka. Kukamatwa viongozi hao wa kijeshi kumeifanya idadi ya watu waliokamatwa katika wiki za hivi karibuni ndani ya taifa hilo, kupindukia 200 ambapo kati yao ni mawaziri wanne na wanamfalme 11 akiwemo Mrithi wa Kiti cha Ufalme wa zamani wa nchi hiyo.
Jinai za Saudi Arabi nchini Yemen
Baadhi ya maafisa wa jeshi wamefichua kwamba kutiwa mbaroni kwa makamanda hao wa kijeshi kumetokana na kushindwa kwao katika vita dhidi ya Yemen. Gazeti la Wall Street Journal limeandika kwamba, Mohammad Bin Salman Al Saud ambaye ameanzisha kile kinachotajwa kuwa ni kupambana na ufisadi wa kiuchumi nchini humo, mbali na kuwatia mbaroni mamia ya shakhsia wakubwa wakiwamo wanamfalme na matajiri wakubwa wa nchi hiyo, pia amefunga maelfu ya akaunti za watu hao. Baadhi ya vyanzo vya habari vimeandika kwamba, Bin Salman ametoa sharti la kuingizwa karibu asilimia 70 ya utajiri wao serikalini kama njia ya wao kuachiliwa huru.

DURU ZA ZANU-PF: CHAMA TAWALA ZIMBABWE KINAPANGA KUMTIMUA MUGABE

Duru za ZANU-PF: Chama tawala Zimbabwe kinapanga kumtimua Mugabe
Viongozi wa chama tawala nchini Zimbabwe cha ZANU-PF wanatazamiwa kupitisha uamuzi wa kumuondoa uongozini Rais wa nchi hiyo na kiongozi wa chama hicho Robert Gabriel Mugabe, ambaye amekuwa akiiongoza nchi hiyo tangu ilipopata uhuru wake miaka 37 iliyopita. Hayo ni kwa mujibu wa duru mbili kutoka ndani ya chama hicho.
Kikao cha dharura kamati kuu ya ZANU-PF kilitazamiwa kufanyika mapema leo kufikiria uamuzi wa kumuondoa kwenye uongozi Mugabe mwenye umri wa miaka 93, siku chache baada ya jeshi kutwaa madaraka kwa lengo la kile kilichotajwa kama kuwachukulia hatua "wahalifu" waliomzunguka kiongozi huyo.
Wakati huohuo, ikimnukuu kiongozi wa Kanisa Katoliki ambaye ni mpatanishi katika mazungumzo na Mugabe, televisheni ya taifa ya Zimbabwe imetangaza kuwa kiongozi huyo atakutana na makamanda wa jeshi hii leo.
Kamati kuu ya chama tawala Zanu-pf inatazamiwa kumrejesha tena kwenye wadhifa wake makamu mwenyekiti wa chama Emmerson Mnangagwa, ambaye kutimuliwa kwake kama Makamu wa Rais na makamu mwenyekiti wa chama hicho kulipelekea jeshi kuingilia kati na kutwaa madaraka ya nchi.
Mke wa Mugabe Grace, yeye anatazamiwa kuvuliwa uongozi wa tawi la wanawake la chama cha Zanu-pf.
Robert Mugabe akiwa na mkewe Grace
Hayo yanajiri huku Rais Mugabe akiendelea kukataa kung'atuka madarakani licha ya kushuhudia kwa macho yake kutokea nyumbani kwake alikowekwa kizuzini jinsi uungaji mkono aliokuwa nao kutoka kwenye chama, vyombo vya ulinzi na usalama pamoja na wananchi ukiyeyuka ndani ya muda wa chini ya siku tatu tu.
Mpwa wa kiongozi huyo Patrick Zhuwao amevieleza vyombo vya habari kuwa Mugabe na mkewe "wako tayari kufa kwa kile wanachokiona kuwa ndio sahihi" kuliko kuachia ngazi ili kuhalalisha kile alichokielezea kama mapinduzi ya kijeshi.
Hayo yanajiri huku makumi ya maelfu ya wananchi wakimiminika kwenye barabara za miji ya nchi hiyo hususan mji mkuu Harare kushinikiza kiongozi huyo ang'atuke madarakani sambamba na kusherehekea kile wanachokieleza kama mwisho wa enzi za miaka karibu 40 ya utawala wake…/

KUSAMBARATISHWA KIKAMILIFU DAESH (ISIS) NCHINI IRSQ

Kusambaratishwa kikamilifu DAESH (ISIS) nchini Iraq
Mabadiliko yanayojiri kwenye medani za vita nchini Iraq yanabainisha kusambaratishwa na kutokomezwa Daesh (ISIS) nchini humo; na kushindwa kikamilifu kundi hilo la kigaidi na kitakfiri ambako ni sawa na kupata mafanikio makubwa Wairaqi katika mapambano dhidi ya magaidi kumeakisiwa sana na duru mbalimbali za habari.
Vikosi vya jeshi la Iraq siku ya Ijumaa viliukomboa mji wa Rawah kutoka kwenye makucha ya magaidi wa Daesh. Kufuatia kukombolewa mji huo kulikochukua muda wa saa kadhaa tu, Waziri wa Mambo ya Ndani wa Iraq Qasim Al-Araji alitangaza kuwa kundi la kigaidi na ukufurishaji la Daesh limesha sambaratishwa kikamilifu nchini humo. Rawah ilikuwa miongoni mwa ngome za mwisho za Daesh ndani ya ardhi ya Iraq. Hivi sasa magaidi wa kundi hilo la ukufurishaji hawana mji mwengine wowote muhimu wa Iraq wanaoushikilia na kuukalia kwa mabavu isipokuwa wanaishia kuzunguka zunguka na kuranda randa kwenye maeneo ya mbali na katika baadhi ya vijiji.
Waziri wa Mambo ya Ndani wa Iraq, Qassim Al-Araji
Mnamo mwaka 2014, kwa uungaji mkono wa kifedha na kijeshi wa Marekani na waitifaki wake wa Magharibi na wa Kiarabu ikiwemo Saudi Arabia, kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh liliishambulia Iraq, likayavamia na kuyakalia kwa mabavu baadhi ya maeneo ya kaskazini na magharibi mwa nchi hiyo. Lakini tangu wakati huo hadi sasa, jeshi la Iraq lilkisaidiwa na vikosi vya kujitolea vya wananchi limeweza kuyakomboa maeneo hayo kutoka kwenye makucha ya kundi hilo; na kimsingi kundi hilo limeshasambaratishwa kikamilifu nchini humo.
Wapiganaji wa jeshi la kujitolea la wananchi la Al Hashdu-Sha'abi
Hata hivyo baada ya kushindwa kijeshi kundi la kigaidi na ukufurishaji la Daesh, suali la kujiuliza hivi sasa ni je, kwa ushindi huo, Wairaqi sasa wataweza kupumua na kupata salama ya kuepukana na shari ya ugaidi? Au kundi hilo la kigaidi na kitakfiri litaanzisha mbinu nyengine mpya na kuendelea kuwaandamana wananchi wa Iraq kwa hujuma na jinai zake za kinyama? Kwa kuzingatia kuwa mashambulio ya kigaidi yalishadidi hivi karibuni katika nchi za Iraq na Syria, tunaweza kusema kuwa baada ya kushindwa kijeshi na kupoteza maeneo waliyokuwa wakiyashikilia kwa mabavu, magaidi wa kundi la kitakfiri la Daesh wameshaainisha mkakati wanaokusudia kuutekeleza mnamo siku zijazo. Ili kufifisha kushindwa kwake kijeshi, kundi la Daesh (ISIS) limeanzisha mbinu na mkakati wa kuvuruga usalama, kwa kushadidisha mashambulio ya kujitoa mhanga ya miripuko ya mabomu pamoja na mauaji ili kuvuruga amani na uthabiti nchini Iraq, sambamba na kupanua wigo wa harakati zake katika nchi nyengine ikiwemo Afghanistan, Libya na kwengineko. Harakati za aina hiyo ni muendelezo wa njia na misimamo ya kufurutu mpaka iliyoanzishwa mwaka 2004 na Abu Mus'ab Az-Zarqawi kwa njia ya kuanzisha mauaji na kuwalenga raia; na baada ya kushadidi hitilafu baina ya Wairaqi ikaandaa mazingira ya kuzaliwa Daesh kutoka kwenye tumbo la Al-Qaeda na kupelekea hatimaye mwaka 2014 kushambuliwa na kukaliwa kwa mabavu kirahisi miji mbalimbali ya ardhi ya Iraq.
Magaidi wa kundi la ukufurishaji la Daesh
Leo hii baada ya miaka mitatu ya vita na mapigano makali ya kujitolea mhanga, yaliyowagharimu roho nyingi za watu na kuwasababishia pia uharibifu mkubwa, Wairaqi wameweza kuyakomboa maeneo yote ya ardhi yao yaliyokuwa yamevamiwa na kushikiliwa kwa mabavu na Daesh; hata hivyo ushindi huo wa kijeshi dhidi ya magaidi wenye misimamo ya kufurutu mpaka sio mwisho wa mapambano, bali inapasa ifanyike kazi ya kuing'oa na kuitokomeza mizizi ya misimamo hiyo hatari. Katika hali kama hiyo, inavyoonekana, baada ya kulisambaratisha kijeshi kikamilifu kundi la Daesh nchini Iraq, vita na mapambano yajayo yatakuwa ni ya kitaarifa na kiintelijinsia ambayo hayatotegemea askari na vifaru pekee; bali yatategemea zaidi unasaji wa taarifa za kiintelijinsia. Katika mazingira ya sasa ambapo magaidi wa kundi la kitakfiri la Daesh wamesha sambaratishwa kikamilifu nchini Iraq, Marekani, ambayo inahisi njama na mipango yake iliyokuwa imepanga dhidi ya Iraq na eneo kwa jumla imevurugika, hivi sasa inashughulika kupanga njama na mikakati mingine mipya ya kiadui. 
Mji wa Rawah uliokuwa ngome ya mwisho muhimu ya Daesh nchini Iraq
Ukweli ni kwamba kundi la kigaidi na ukufurishaji la Daesh limeshafutwa kwenye ramani ya Iraq, na hilo limewezekana kwa baraka na nafasi ya uongozi wa juu wa kidini na kwa kujitolea mhanga vikosi vya Iraq hususan vya jeshi la kujitolea la wananchi la Al Hashdu-Sha'abi. Na hii ni katika hali ambayo jeshi hilo la wananchi lingali linaendelea kuandamwa na njama na tuhuma za Marekani. Kutokana na matukio yaliyojiri huko Iraq wananchi wanapaswa kuwa macho zaidi katika kipindi kinachoanza hivi sasa cha baada ya kusambaratishwa Daesh nchini humo.../

WAFUNGWA WA KISIASA BAHRAIN WAZUILIWA KUWA NA MAWASILIANO YOYOTE NA NJE YA JELA

Wafungwa wa kisiasa Bahrain wazuiliwa kuwa na mawasiliano yoyote na nje ya jela
Duru zenye uhusiano na familia ya Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kitaifa ya al-Wifaq nchini Bahrain, zimeeleza kuwa utawala wa Aal-Khalifa umemwekea vizuizi vikubwa Sheikkh Ali Salman na shakhsia wengine mashuhuri wanaoshikiliwa katika jela za nchi hiyo.
Kwa mujibu wa habari hiyo, Sheikh Ali Salman na shakhsia wengine wakubwa wanaoshikiliwa katikka jela za Bahrain wamezuiliwa kufanya mawasiliano na watu wa familia zao, kupiga simu au hata kusoma magazeti. Katika kuendelea kutolewa hukumu za kidhalimu za utawala wa Aal-Khalifa dhidi ya Sheikh Ali Salman anayeendelea kutumikia kifungo cha miaka tisa jela, utawala huo umewasilisha mahakamani mashitaka mapya dhidi ya shakhsia huyo ya kile kinachotajwa kuwa eti ni kufanya ujasusi kwa maslahi ya Qatar.
Shakh Ali Salman, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kitaifa ya al-Wifaq nchini Bahrain
Katika uwanja huo, mwendesha mashtaka wa Manama amewasilisha mashtaka hayo dhidi ya Sheikh Ali Salman, Hassan Sultwan na Ali al-Usud, ambao nao pia ni wanachama wa Jumuiya ya Kitaifa ya al-Wifaq kwa tuhuma hizo hizo za kufanya ujasusi kwa ajili ya Qatar kwa lengo la kile alichokisema kuwa eti ni kutaka kuiondoa madarakani serikali ya Bahrain. Kwa mujibu wa taarifa hiyo, hukumu dhidi ya shakhsia hao itatolewa tarehe 27 Novemba mwaka huu.
Maandamano ya Wabahrain
Sheikh Ali Salman alikamatwa mwaka 2014 na utawala wa kidikteta wa Aal-Khalifa na kuhukumiwa kifungo cha miaka minne jela mwaka 2015 kwa tuhuma za uchochezi na kuivunjia heshima Wizara ya Mambo ya Ndani ya nchi hiyo. Hata hivyo mahakama ya rufaa ya nchi hiyo na katika njama za kutaka kumfunga miaka mingi zaidi shakhsia huyo ilimbadilishia mashitaka na kuyafanya ya tuhuma za kutaka kubadilisha utawala na hivyo ikamuhukumu kifungo cha miaka tisa jela.

Friday, November 17, 2017

UMASIKINI UNACHOCHEA MIMBA ZA UTOTONI TANZANIA

Utafiti: Umasikini unachochea mimba za utotoni Tanzania
Imeelezwa kuwa, umasikini na kipato cha chini cha baadhi ya familia nchini Tanzania ndicho chanzo cha mimba za utotoni katika jamii ya nchi hiyo ya Afrika Mashariki.
Hayo yameelezwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Jukwaa la Utu wa Mtoto (CDF), Koshuma Mtengeti katika warsha ya siku moja ya kutambulisha mradi na shirika hilo kwa wadau iliyofanyika mkoani Dodoma. Kwa mujibu wa shirika hilo, utafiti uliofanywa na shirika hilo kwa kusaidiana na mashirika mengine, umebaini kwamba, umasikini wa familia husababisha familia zenye maisha magumu kupambana kwa bidii kutafuta chakula na mavazi ya watoto wao.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Jukwaa la Utu wa Mtoto ameeleza kuwa, utafiti wa Demografia ya Afya Tanzania wa 2016 (TDHS) unaonesha kwamba, asilimia 36 ya wasichana wa umri wa kati ya miaka 20-24 waliolewa kabla ya kufikia miaka 18. 
Maandamano ya kupinga ndoa za utotoni nchini Nigeria
Hayo yanajiri katika hali ambayo, kumekuweko na kampeni ya kimataifa ya kukabiliana na ndoa za utotoni hasa barani Afrika.
Mwezi uliopita nchi ya Senegal ilikuwa mwenyeji wa mkutano uliokuwa na lengo la kuongeza hatua za kutokomeza ndoa za utotoni katika nchi za Afrika Magharibi na Kati. Inaelezwa kuwa, wazazi ambao hali zao ni duni kimaisha, mara nyingi huwaozesha watoto wao mapema ili kupunguza mzigo wa ulezi, wakati huo huo, baadhi ya mila na desturi zinatajwa kuwa nazo zina mchango katika hilo.

Thursday, November 16, 2017

WAMAREKANI WAZIDI KUPIGANA RISASI KIHOLELA, MAKUMI WAUAWA NA KUJERUHIWA

Wamarekani wazidi kupigana risasi kiholela, makumi wauawa na kujeruhiwa
Watu 16 wameuawa na wengine 24 kujeruhiwa katika matukio 56 ya kupigana risasi kiholela yaliyotokea katika kipindi cha masaa 24 kwenye maeneo tofauti ya Marekani.
Kituo cha kutoa takwimu za mashambulizi ya silaha nchini Marekani kimetangaza habari hiyo na kuongeza kuwa mauaji na mashambulizi hayo yametokea katika kipindi cha masaa 24 yaliyopoita katika majimbo ya Florida, Michigan, Texas, Ohio na Pennsylvania. 
Kwa mujibu wa kituo hicho cha Marekani, katika kipindi cha masaa 48 yaliyopita, kumeripotia matukio 164 ya kupigana risasi kiholela katika kona mbalimbali za Marekani ambayo yamepelekea watu 45 kuuawa na wengine 88 kujeruhiwa.
Umilikaji silaha ovyo, mgogoro mkubwa kwa Marekani

Takwimu zinaonesha kuwa, jamii ya Marekani ndiyo yenye silaha nyingi zaidi zinazomilikiwa na watu majumbani kuliko jamii nyingine yoyote duniani kiasi kwamba kati ya kila watu 100, 90 kati yao wana silaha nyepesi majumbani mwao.
Takwimu zinaonesha pia kuwa makundi ya utengenezaji silaha yana nguvu sana nchini Marekani na ndiyo yanayodhibiti vyama vya Democrats na Republican, hivyo serikali yoyote inayoingia madarakani haina nguvu ya kupiga marufuku umilikaji silaha ovyo nchini Marekani.