Katika kukaribia mwaka wa pili wa Rais Donald
Trump kuwa ofisini, mashirika ya haki za binadamu yamekosoa vikali
utendaji wa serikali ya Marekani na hasa Trump mwenyewe kwa kuvunja haki
za binadamu.
Akizungumzia suala hilo hivi karibuni, Kenneth Roth, mkurugeni
mwandamizi wa shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch
lililo na makao makuu yake mjini New York Marekani, ameutaja utendaji wa
Trump kuhusiana na suala zima la haki za binadamu kuwa janga kubwa na
kusema rais huyo ni dikteta anayeunga mkono tawala zisizo za
kidemokrasia kama Saudi Arabia. Wakati huohuo maripota wasio na mipaka
wametoa taarifa wakiashiria matamshi ya hujuma na dharau ya Trump dhidi
ya vyombo vya habari na kusema kuwa tabia yake hiyo ni tishio kubwa kwa
demokrasia ya Marekani. Zeid bin Ra'ad al-Hussein, Kamishna Mkuu wa Haki
za Biandamu wa Umoja wa Mataifa pia amesema kuwa Donald Trump anatishia
uhuru wa vyombo vya habari nchini humo.
Hata hivyo ni wazi kuwa suala la ukiukaji wa haki za binadamu
halihusiani tu na Rais Trump bali kwa miongo kadhaa sasa marais wa
Marekani wamekuwa wakikiuka wazi haki za binadamu ndani na nje ya mipaka
ya nchi hiyo. Kwa mfano katika utawala wa George W. Bush, ukiukaji
mkubwa wa haki za binadamu ulifanyika ndani na nje ya nchi hiyo kukiwepo
kuanzishwa jela za mateso na za kuogofya za Guantanamo nchini Cuba na
Abu Ghurain huko Iraq na vilevile kuteswa wafungwa kwa kuzamishwa
majini. Katika kipindi cha Barack Obama pia, ukiukaji mkubwa wa haki za
binadamu ulifanywa na askari jeshi wa nchi hiyo katika pembe tofauti za
dunia na hasa nchini Afghanistan ambapo ndege za kijeshi zisizo na
rubani za Marekani zilitumika kuua maelfu ya raia wasio na hatia. Hii ni
katika hali ambayo uungaji mkono wa Marekani kwa nchi na tawala
nyingine zinazokiuka wazi haki za binadamu kama Saudi Arabia, Bahrain na
utawala haramu wa Israel umekuwa ukiendelea kwa miaka hii yote.
Pamoja na hayo lakini vitendo na matamshi ya Trump dhidi haki za
binadamu na uhuru wa vyombo vya habari yameufikisha ukiukaji huo wa haki
za binadamu katika hatua nyingine hatari. Trump anachukuliwa kuwa ni
mtu aliye na chuki kali dhidi ya wahajiri, wageni na Waislamu na
asiyesita kutumia matusi dhidi ya binadamu wenzake. Ni hivi majuzi tu
ambapo Trump aliwataja Wamexico kuwa watenda jinai, Waislamu kuwa
magaidi na Waafrika kuwa shimo la choo. Ushindi wake chini Marekani hivi
sasa umeyapa nguvu mpya makundi yenye misimamo ya kupindukia mipaka, ya
kibaguzi na yenye chuki kali na yanayotumia mabavu dhidi ya wenzao
ndani na nje ya mipaka ya Marekani, makundi ambayo huwa hayasiti hata
kidogo kutenda jinai na kukiuka haki za binadamu pamoja na uhuru wa watu
binafsi na wa kiraia.
Kuhusu siasa za nje pia, hatua ya Trump ya kuichagua Saudia kuwa nchi
ya kwanza aliyoitembelea akiwa Rais wa Marekani, nchi ambayo iko mstari
wa mbele wa kukiuka haki za binadamu na inayohusika moja kwa moja
katika mauaji ya Waislamu katika vita vyake vya kivamizi huko Yemen,
inaonyesha ni kwa kiwango gani Marekani haijali kuhusu suala la
kuheshimiwa haki za binadamu.
Trump pia ameyakasirisha mno mashirika mashuhuri ya kutetea haki za
binadamu kutokana na hatua yake ya kuunga mkono kuendelea kujengwa
vitongoji vya walowezi wa Kizayuni katika ardhi za Wapalestina pamoja na
uamuzi wake wa hivi karibuni wa kutambua rasmi mji mtakatifu wa Quds
eti kuwa mji mkuu wa utawala haramu wa Israel. Pamoja na hayo, lakini
haionekani kuwa malalamiko na ukosoaji huo wote wa mashirika na taasisi
za kimataifa utamfanya Donald Trump ambaye ameipa kipaumbele nara ya
'Marekani Kwanza' katika siasa zake kulegeza msimamo na kuheshimu haki
za binadamu pamoja na uhuru wa kujieleza wa vyombo vya habari.
No comments:
Post a Comment